Italia yajitosa kuzalisha umeme kutoka kwenye takataka Tanzania

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya nishati safi nchini yakipigiwa chapuo, ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Italia umetua Tanzania kuangalia fursa mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa nishati hiyo kutoka kwenye takataka.

Maeneo mengine yatakayotazamwa na kampuni hizo ni uwekezaji katika teknolojia za kilimo, uchumi wa buluu, sekta ya afya, na dawa.

Hayo yamesemwa leo, Jumatatu, Februari 3, 2025, na Balozi wa Italia nchini, Giuseppe Coppola,alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la nne la uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, linalotarajiwa kufanyika Februari 11 na 12 mwaka huu upande wa Tanzania Bara, kisha Zanzibar Februari 14, 2025.

Coppola amesema kongamano hilo litaangazia fursa za uwekezaji ambazo ni kipaumbele cha Tanzania katika ujenzi wa uchumi wake.

Amesema, katika eneo la uchumi wa kijani na miundombinu endelevu, wataangalia namna wanavyoweza kufanya uzalishaji wa nishati safi kutoka kwenye takataka.

“Pia tutaangazia uzalishaji wa nishati mbadala, hili litaenda sambamba na uzalishaji wa kemikali za kusafishia maji, usafirishaji, miundombinu endelevu, maendeleo ya kidigitali, na madini,” amesema Coppola.

Amesema Italia ni moja ya nchi zinazotumia nishati mbadala kwa sehemu kubwa katika uzalishaji wake wa nishati, hivyo nia yao ni kushiriki maarifa hayo na kushirikiana uzoefu na Tanzania.

Hili linakuja ikiwa ni siku chache tangu kumalizika kwa mkutano wa nishati Afrika, ulilenga kuhakikisha Waafrika milioni 300 wanafikiwa na umeme  hadi kufikia mwaka 2030, huku nishati mbadala ikiwa ni moja ya maeneo yaliyopendekezwa kwa uwekezaji kutokana na fursa zilizopo.

Katika kilimo, amesema uwekezaji utalenga teknolojia za kilimo, uchumi wa buluu, ikiwa ni pamoja na masuala ya mbolea, mifumo ya umwagiliaji, ufugaji, matumizi ya ngozi, ufugaji wa samaki, na usambazaji.

Kwa upande wa sekta ya afya na dawa, amesema watalenga teknolojia za afya, mashine, huduma za kiafya, vifaa vya meno, vifaa vya michezo, na huduma nyingine.

Coppola amesema kongamano hilo linalenga kukuza biashara baina ya pande mbili, kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji, na kujenga mitandao ya kibiashara kupitia mijadala ya wazi.

Pia, amesema hiyo itajumuisha warsha za kitaalamu na ziara kibiashara zenye lengo la kutoa mafunzo na kushirikishana ujuzi na maarifa, jambo linalosaidia wadau kuelewa hali ya uchumi, mitazamo ya kibiashara, na kuimarisha mahusiano thabiti na wadau wa ndani huku wakitafuta fursa za uwekezaji katika sekta tofauti.

“Pia, uhusiano wa kiuchumi kati ya Italia na Tanzania umeendelea kukua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni. Biashara baina ya nchi hizi mbili zimeimarika kwa kiasi kikubwa katika sekta mbalimbali, zikiwemo viwanda, kilimo, utalii, ushirikiano wa kiufundi, mashine, kemikali, vifaa vya umeme, dawa, na bidhaa za chakula,” amesema.

Amesema Tanzania inasafirisha bidhaa za kilimo, madini, na maliasili kama vile kahawa, chai, pamba, samaki, madini, na vito vya thamani kwenda Italia, jambo ambalo limefanya Italia kuona uwepo wa haja ya kuwekeza Tanzania, hasa katika sekta za utalii na kilimo.

Italia iliuza bidhaa za Sh380.99 bilioni, huku ikinunua bidhaa za Sh2143.09 bilioni kutoka Tanzania mwaka 2023.

Pamoja na urari wa biashara kuwa hasi kwa upande wa Tanzania, kati ya mwaka 2020 hadi 2024, Italia imewekeza Sh318.85 bilioni kupitia miradi tisa waliyowekeza.

Kwa upande wake, John Mnali, Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), amesema katika kongamano hilo, kampuni 45 zimethibitisha ushiriki, huku wakifanikiwa kuhamasisha Watanzania 500 watakaoshiriki katika kongamano hilo.

“Sekta ambazo zimelengwa ni kilimo, uvuvi, na masuala ya bahari sambamba na dawa za binadamu,” amesema Mnali.

Related Posts