Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, amekiri kukunwa na kiwango kikubwa cha soka alichonacho kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyedai kama akikaza kidogo tu anaweza kufika mbali zaidi.
Staa huyo aliyeanza soka jijini Arusha alikozaliwa na kukulia akiitumikia AFC Arusha kabla ya Simba kumbeba na baadae kutua Yanga, alisema kwa kipaji cha Fei anamuona akifika mbali kwani anajua kitu gani anachotakiwa kukifanya uwanjani na amemtabiria kuendelea kupiga pesa ndefu.
“Kimafanikio ya Yanga inaizidi Azam, ila wakati Fei Toto yupo Yanga kulikuwepo na wafalme wengi, hivyo asingepata nafasi kama aliyonayo kwa sasa kipaji chake kuendelea kuonekana kwa ukubwa zaidi,” alisema Nurdin Bakar na kuongeza;
“Sio mfuatiliaji sana wa mpira, lakini Fei Toto anashawishi kumtazama, kitu kizuri ni kwa zama hizi wao wanabebwa na mifumo zaidi, tofauti na kipindi chetu uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ulizingatiwa zaidi.”
Hata hivyo, Nurdin alimtaka Fei Toto kutolewa sifa bali apambane na atambue soka lina muda wake, hivyo kabla umri haujamtupa mkono anaweza akapiga pesa ndefu kutokana na mikataba atakayoipata iwe ndani au njue ya nchi, kwa sababu dunia ya sasa soka ni biashara inayolipa vizuri.
“Mbali na Fei naona juhudi za kina Mudathir Yahya anayefanya kazi kubwa ya kumsaidia Khalid Aucho ambaye akiwepo uwanjani timu inatulia, hiyo inaweza ikawa sababu ya Jonas Mkude kukaa benchi, japo ni vizuri akapewa nafasi ataisaidia timu hiyo.”
“Kwa upande wa Simba wakati ligi inaanza msimu huu, Fabrice Ngoma hakuwa na nafasi badala yake akawa anacheza Debora Mavambo, Augustine Okajepha au Mzamiru Yassin, kocha alipompa nafasi Ngoma kiwango chake kimewaka akiwa na pacha kali zaidi akicheza na Yusuf Kagoma.”
Mkongwe huyo aliyewahi kuzitumikia timu za taifa za Vijana U17, U20 na Taifa Stars kwa vipindi tofauti, alisema wachezaji wanaopata nafasi ya kucheza Simba na Yanga wanapaswa kuongeza nidhamu akitolea mfano wa Ibrahim Ajibu licha ya ukubwa wa kipaji alichokuwa nacho kimepotea kirahisi.
“Ajibu angakuwa anasimuliwa kwa viwango vya juu kwa sasa, chini ya aliyekuwa kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alitoa asisti nyingi na alifunga mabao, kitendo cha kurudi Simba akakutana na Clatous Chama ikawa mwanzo wake wa kutoka katika ramani ya soka,” alisema Nurdin aliyezitumikia pia timu za Villa Squad, Rhino Rangers na Lipuli baada ya kutamba awali na AFC Arusha (2003), Simba (2004-2007) na Yanga (2007-2013).