KATIBU WA SUKI RABIA "KILICHOFANYWA NA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU HAKIJAVUNJA KATIBA YA CHAMA"


NA WILLIUM PAUL, ROMBO.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi na Katibu wa Nec Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Hamid amesema kuwa kilichofanywa na Wajumbe wa Mkutano mkuu kumpitisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Chama hicho katika uchaguzi mwaka huu ni kwa mujibu wa katiba ya Chama.

Rabia ambaye ni mlezi wa Chama hicho mkoa wa Kilimanjaro alitoa kauli hiyo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi ambapo kimkoa yamefanyika kata ya Katangara mrere wilayani Rombo.

Alisema kuwa, wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wkaipotosha kuwa kilichofanyika na Wajumbe hao ni kukiuka katiba ya chama na kuwataka wanaccm na wananchi kuwapuuza.

“Mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi ndio chombo cha mwisho cha maamuzi na kilichofanywa na Wajumbe wake kimezingatia katiba ya Chama hivyo wapuuzeni hao wanaoibuka na kutoa taarifa za uongo” Alisema Rabia.

Mjumbe huyo wa Nec alisema kuwa, kwa sasa Chama hicho kinaenda kujipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 ili kuhakikisha wagombea wake wanashinda kwa kishindo na Tanzania inaenda kuwa ya kijani.

Alisema kuwa, kwa sasa wameshawahesabu wapiga kura wa ccm na uchaguzi wa mwaka huu Chama kitaenda kushinda kwa kishindo na kuwataka Wapinzani kukaa mkao wa kula.

Rabia alisema kuwa, hakuna chama chenye historia kama CCM na uimara wake ambapo wananchi wamekuwa wakikituma kupitia viongozi wake na wao wapo tayari kutumwa na kuwatumikia wananchi.

Aliongeza kuwa, Kilimanjaro imebadilika katika swala la umoja upo vizuri na hana shaka katika uchaguzi wa 2025 chama kitashinda kwa kishindo ili kukuza nguvu na umoja kama Watanzania.

“Wananchi mnawajibu wa kumuongezea moyo wa kutafuta fedha nyingi zaidi za maendeleo kwa kumpa kura nyingi za kishindo pamoja na kuilinda na kuitunza miradi inayotekelezwa ili iweze kudumu muda mrefu.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Seleman Mfinanga alisema kuwa, miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho yapo mafanikio makubwa ya kujivunia katika kipindi chote hicho.

“Miaka 48 ya CCM tumeshuhudia ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali za elimu, Afya, Barabara, maji na hili ni jambo la kujivunia katika miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi” Alisema Mfinanga.


Related Posts