Katika matoleo yaliyopita, tulichunguza chimbuko la kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na athari zake zilizosababisha taharuki nchini humo.
Pia, tuliona baada ya juhudi za jumuiya ya kimataifa, jioni ya Desemba 12, 2013, DRC ilisaini mkataba wa amani na M23 uliolenga kuleta maridhiano, uthabiti na maendeleo eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Mkataba huo ulisainiwa Ikulu ya Nairobi nchini Kenya mbele ya mashuhuda wakiwamo marais Yoweri Museveni wa Uganda, Joyce Banda wa Malawi, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Joseph Kabila wa DRC, lakini haukutekelezwa ipasavyo.
Kati ya Desemba 2013 na Desemba 2016, waasi wa M23 hawakuonekana kwa kiwango kikubwa kama awali, hivyo hofu waliyoleta ilianza kupungua.
Wakati huo, mwanzilishi wa kundi hilo, Bosco Ntaganda alikuwa amekamatwa akikabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague nchini Uholanzi.
Kesi ya Ntaganda ilianza kusikilizwa Septemba 2, 2015, alishtakiwa kwa makosa 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa watoto waliokuwa wanajeshi ndani ya jeshi lake mwenyewe.
Wakati ikionekana kana kwamba hali imetulia, Januari 16, 2017 waasi hao waliingia tena DRC kutoka nchi jirani ya Uganda na kuzusha hofu upya iliyokuwa imeonekana kukoma tangu Desemba 2013.
Waasi waliwasili kutoka Uganda na kukamata kijiji kimoja kaskazini mwa Jimbo la Kivu ya Kaskazini.
DRC ilisema jenerali wa zamani wa jeshi, Sultani Makenga, aliongoza mojawapo ya batalioni za waasi hao.
Januari 17, Jeshi la Uganda lilikanusha taarifa kwamba takriban waasi 200 wa Kundi la M23 waliopewa hifadhi nchini humo wamevuka mpaka na kuingia tena DRC.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Uganda, Meja Henry Obbo alisema wapiganaji hao bado wako katika kambi ya kijeshi ya Bihanga iliyoko kilomita 320 magharibi mwa Mji Mkuu wa Kampala.
Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende aliwaambia waandishi wa habari kuwa, waasi hao wa Kitutsi waliingia nchini humo na kukiteka kijiji kimoja Jimbo la Kaskazini la Kivu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Henry Okello Oryem alisema DRC haipaswi kutafuta visingizio kwa kuihusisha Uganda na waasi hao wa M23.
Baada ya kurushiana maneno kati ya Uganda na DRC kwa zaidi ya mwezi mmoja, Februari 24, 2017 Uganda iliwakamata wapiganaji 57 wa M23 waliokimbia DRC baada ya kukabiliana na wanajeshi wiki hiyo na kuwahifadhi katika kambi moja ya kusini magharibi mwa Mji wa Kisoro.
Siku tatu baadaye, Februari 27, 2017 Serikali ya Uganda ilianza kuwarejesha DRC wapiganaji wa zamani wa kundi la M23 pamoja na familia zao, ikiwa ni sehemu ya makubaliano kati ya waasi hao wa zamani na Serikali ya Uganda na DRC kurejea nyumbani kwa hiari.
Uganda ilianza kwa kuwarejesha wapiganaji zaidi ya 70, na Serikali ya Uganda ikasema wengi wa wapiganaji hao walikubali kwa hiari kurejea pamoja na familia zao ikiwa ni miaka mitano tangu kundi hilo lishindwe vita mashariki mwa DRC.
Walisafirishwa kwa ndege ya Umoja Mataifa (UN) kutoka Uwanja wa Ndege wa Entebbe kwenda DRC.
Hatua ya kuwarejesha ilichukuliwa chini ya mpango wa utekelezaji wa makubaliano yaliofanyika mwaka 2013 ikiwa moja kati ya mikakati ya kutatua mzozo wa vita eneo la maziwa makuu.
Wakati mzozo kati ya waasi wa M23 na Serikali ya DRC ukiendelea, Agosti 28, 2018 majaji ICC walianza kusikiliza hoja za mwisho katika kesi dhidi ya Ntaganda.
Julai 8, 2019 ICC mjini The Hague ilimtia hatiani Ntaganda ambaye kwa muda wote wa miaka mitatu wa kesi dhidi yake alishikilia kuwa hana hatia.
Alikabiliwa na kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama hiyo.
Hakuonyesha hisia zozote wakati jaji aliyesimamia kesi hiyo, Robet Fremr, alipopitisha hukumu hiyo.
Ntaganda alitiwa hatiani mara ya kwanza mwaka 2006 kwa ishara ya kufanya uhalifu Bara la Afrika, bila hofu ya kuchukuliwa hatua kisheria wakati akihudumu kama jenerali katika Jeshi la DRC kabla ya kujisalimisha mwaka 2013 wakati ushawishi wake katika Kundi la M23 aliloasisi uliposambaratika.
Waendesha mashitaka wa ICC walisema uhalifu huo ulifanyika wakati Ntaganda alipoliongoza Kundi la Patriotic Forces for the Liberation of Congo (FPLC), tawi la kijeshi la Chama cha Union of Congolese Patriots, katika Jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa DRC kati ya mwaka 2002 na 2003.
Ntaganda alielezewa pia, kama kiongozi asiye huruma wa uasi wa Watutsi wakati wa vita vilivyoiyumbisha DRC baada ya mauaji ya Kimbari ya 1994 nchini Rwanda.
Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, zaidi ya watu 60,000 waliuawa tangu machafuko yalipozuka eneo hilo mwaka 1999 wakati waasi walipokabiliana kupigania udhibiti wa rasilimali ya madini.
Ntaganda pia alishirikishwa na vuguvugu la M23, lililosaini mkataba wa amani na Serikali ya DRC Desemba 2013.
Kama ilivyoelezwa katika moja ya makala, alijisalimisha mwenyewe Ubalozi wa Marekani, Mji Mkuu wa Rwanda, Kigali, mwaka 2013 baada ya kuepuka mitego ya kumkamata kwa miaka saba.
Ingawa Ntaganda alikuwa ameshatiwa nguvuni na kuhukumiwa na ICC pamoja na kwamba alikuwa tayari ameshapoteza udhibiti wa kundi lake la M23, bado kundi hilo la waasi liliendelea kuwa kero kwa Serikali ya DRC. Ulifika wakati ambao Wacongo wenyewe waliamua kutafuta namna ya kumalizana na hii vita isiyokwisha.
Agosti 3, 2020 wawakilishi na wajumbe kutoka makabila yote ya Jimbo la Kivu ya Kaskazini DRC, waliafikiana kutafuta suluhisho la hali mbovu ya usalama inayoshuhudiwa jimbo hilo la mashariki mwa nchi.
Jimbo hilo limekumbwa na misukosuko na ukosefu wa usalama kwa zaidi ya miongo miwili.
Raia wake wamekuwa wakiishi katika hali ya vurugu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya makundi ya waasi wanaovichoma vijiji moto.
Wakati huohuo, wawakilishi wa mashirika ya kiraia walidai kuwa, bado eneo hilo litaendelea kukabiliwa na uvamizi mkubwa wa makundi ya wanamgambo kutoka nje na ndani ya DRC kufuatia kile walichokiita ‘uzembe wa Serikali’ kushindwa kugunduwa chanzo kinachosababisha mamia ya vijana kujiunga na makundi hayo ya waasi na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa raia.
Haya yalijiri siku chache baada ya wawakilishi wa asasi za kiraia Mkoa wa Kivu ya Kaskazini kutangaza kurudi upya kwa waasi wa M23 walioanzisha harakati zao wilayani Rutshuru.
Septemba 9, 2020 ilibainika kuwa asilimia 70 ya waasi wa kundi jingine la waasi la FRPI, waliokuwa wamesalimisha silaha DRC walitoroka kwenye Kambi ya Azita, kusini mwa Mtaa wa Irumu, jimboni Ituri walimokuwa wakipewa hifadhi.
Wanamgambo hao walisalimisha silaha mapema mwaka huu kwa amani, kufuatia wito wa Rais Felix Tshisekedi.
Taarifa zinaeleza kuwa, waliamua kurejea msituni baada ya kutopewa chakula na Serikali kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Februari 2020 Serikali ya DRC ilitia saini mkataba wa amani na kundi hilo la FRPI la wapiganaji wa Kabila la Walendu waliotakiwa kujumuishwa katika jeshi la taifa.
Je, usalama ulizidi kuhatarishwa? Tukutane kesho katika toleo lijalo.