M23 wanavyowavuruga viongozi Afrika | Mwananchi

Kufuatia kutekwa kwa Mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kundi la waasi la M23 wiki iliyopita, baadhi ya viongozi wa Afrika wameingia kwenye mvutano, huku vita hivyo vikihofia kuambukiza mataifa mengine.

Kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda limekuwa kwenye mapigano ya muda mrefu na Serikali ya DRC, ambapo sasa limeapa kusonga kuelekea mji mkuu Kinshasa umbali wa takriban kilomita 2,600 Magharibi mwa nchi.

Mgogoro Mashariki mwa DR Congo ulianza tangu miaka ya 1990 lakini umekuwa ukiongezeka kwa kasi katika wiki za hivi karibuni. M23, kundi linalojumuisha waasi wa kabila la Watutsi, linasema linapigania haki za wachache, huku serikali ya DR Congo ikidai kuwa waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wanajaribu kuchukua udhibiti wa utajiri mkubwa wa madini uliopo mashariki mwa nchi hiyo.

Wakati Jumuiya za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika zikiketi kujadili mzozo huo hivi karibuni, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye ameonya kuwa mgogoro huo unaweza kuzua vita vya kikanda, huku Shirika kuu la Afya barani Afrika likionya kuwa mapigano hayo yanaweza kusababisha milipuko mipya ya magonjwa hatari.

Askari wa M23 mwaka 2012 wakati kikundi hicho kinaanza

Akihutubia nchini humo Februari mosi, 2025, Rais Ndayishimiye ametoa wito vita hivyo kudhibitiwa.

“Ikiwa hali itaendelea hivi, vita vinahatarisha kuenea kote katika ukanda huu. Siyo Burundi pekee, ni Tanzania, Uganda, Kenya – ni ukanda mzima, ni tishio,” amesema katika video rasmi iliyochapishwa kwenye YouTube Jumamosi.

Burundi ina wanajeshi wanaokadiriwa kufikia 10,000 Mashariki mwa DR Congo waliopelekwa chini ya makubaliano ya kijeshi ya awali na Kinshasa na wamepelekwa tena katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bukavu.

Wakati huo huo, jeshi la Uganda nalo lilitangaza Ijumaa iliyopita kuwa litachukua msimamo wa “ulinzi wa mstari wa mbele” mashariki mwa DR Congo.

Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa Julai ilisema kuwa Rwanda ina takriban wanajeshi 4,000 Mashariki mwa DR Congo, na kuituhumu Kigali kuwa na “udhibiti wa moja kwa moja” wa waasi wa M23.

Hata hivyo, Rwanda inakanusha kuhusika kijeshi katika eneo hilo, ikidai kuwa lengo lake Mashariki mwa DR Congo ni kuwaangamiza waasi wa Kihutu walioanzisha kundi la wapiganaji baada ya mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda.

Serikali ya DR Congo inaituhumu Rwanda kwa kutaka kunufaika na madini adimu kutoka mashariki mwa nchi hiyo, madini yanayotumika katika teknolojia kama simu janja kote duniani – madai ambayo Rwanda pia inakanusha.

Katika mazungumzo ya dharura mjini Harare Februari mosi, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) ilithibitisha kuendelea kuisaidia DRC.

“Vita vinavyozidi kuongezeka Mashariki mwa Congo vimeleta hali mbaya. Tunakutana hapa kutafuta suluhisho la kudumu ili kumaliza changamoto zinazokumba watu wa DRC.

“Watu wa Mashariki mwa Congo wameteseka kwa muda mrefu sana. Wakati tunapojisikia kuomboleza kwa hasara yetu, dhamira yetu ya kuhakikisha usalama wa pamoja haiwezi kutetereka,”amesema amesema Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Sadc.

Amesema jumuiya hiyo itajitolea kutafuta amani katika DRC, huku akisisitiza jinsi mzozo katika eneo lenye rasilimali za madini umeanza kuathiri uhusiano wa kidiplomasia katika eneo zima.

Ingawa mapigano yamesimama kwa kiasi kikubwa Goma, waandishi wa AFP wameripoti kuwa bado kuna uhaba mkubwa wa pesa taslimu na mafuta, huku mamlaka ya Congo ikisita kuipa kipaumbele Goma, mji ulioko chini ya udhibiti wa M23.

Katika maeneo waliyoyateka, waasi wa M23 wameanza kuanzisha utawala mbadala na kuwateua maofisa wanaowaunga mkono.

Hata hivyo, baadhi ya masoko yalifunguliwa katikati ya Goma Jumamosi, huku wafanyabiashara wakianza biashara zao na wanawake wakibeba mafungu ya majani ya mihogo kwenye mabega yao.

Umoja wa Mataifa (UN) unasema takriban watu 700 wameuawa katika mapigano makali mjini Goma, jiji kubwa zaidi Mashariki DRC tangu Jumapili.

Msemaji wa UN, Stéphane Dujarric, amesema kuwa watu 2,800 wamejeruhiwa huku waasi wa M23 – wanaoungwa mkono na Rwanda – wakiteka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Kwa sasa, inaripotiwa kuwa waasi hao wanaelekea Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini. Ijumaa, Dujarric alisema kuwa takwimu za vifo zinatokana na tathmini iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na washirika wake, kwa kushirikiana na serikali ya DR Congo, kati ya Jumapili na Alhamisi.  Msemaji wa UN pia alionya kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezeka zaidi.

Ili kuzuia maendeleo ya M23, jeshi la DR Congo limeweka mstari wa ulinzi barabarani kati ya Goma na Bukavu, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP. Mamia ya raia wamejitolea kusaidia kulinda Bukavu.

Kijana mmoja aliambia AFP: “Niko tayari kufa kwa ajili ya nchi yangu.”

Jean-Jacques Purusi Sadiki, gavana wa Kivu Kusini – jimbo ambalo waasi wa M23 wanalisogelea – ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa jeshi la Serikali na washirika wake wanawazuia waasi hao, ingawa madai hayo hayajathibitishwa kwa uhuru.

Waziri wa Mambo ya Nje wa DR Congo, Thérèse Kayikwamba Wagner, aliambia BBC kuwa Rwanda inakalia kwa nguvu sehemu ya nchi yake na inajaribu kuipindua serikali.

Wagner alisema kuwa jumuiya ya kimataifa imeiruhusu Rwanda, chini ya Rais Paul Kagame, kuendelea kukiuka sheria za kimataifa bila kuchukuliwa hatua kwa miongo kadhaa.

Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alikanusha madai hayo, akisema wanajeshi wa Rwanda wako mpakani ili kuzuia mzozo huo kuenea katika ardhi yao.

 “Hatuna nia ya vita, hatuna nia ya kuteka ardhi, wala kubadilisha serikali,” Makolo aliiambia BBC.

Shelley Thakral, kutoka Shirika la Chakula Duniani la UN (WFP), alisema kuwa wakazi wa Goma wanakabiliwa na uhaba wa chakula, maji safi na vifaa vya matibabu.

“Ugavi wa bidhaa muhimu umeathirika sana kwa sasa. Ikiwa ardhi na anga vimefungwa, basi kila kitu kimesimama,” alisema Thakral katika mahojiano na AFP.

Tangu mwanzo wa mwaka huu, zaidi ya watu 400,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la UN.

DR Congo ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika – ikiwa na takriban theluthi mbili ya eneo la Ulaya Magharibi – na inapakana na nchi tisa tofauti.

Related Posts