Mapya yaibuka wachimbaji walionasa mgodini, miili miwili yaopolewa

Kahama. Miili miwili ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Nkandi, eneo la Mwime, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, kati ya watatu waliofukiwa na kifusi, imeopolewa, huku wachimbaji wa eneo hilo wakiiangukia Serikali kuhusu ubovu wa duara hilo lililogharimu maisha ya wenzao.

Miili hiyo imeopolewa leo, Jumatatu, Februari 3, 2025. Baadhi ya wachimbaji, akiwemo Masanja Maige, amesema amesikitishwa na tukio hilo kwani chanzo ni ubovu wa maduara ambayo yameanzishwa muda mrefu, akiiomba Serikali kupitia kwa wakaguzi wa maduara hayo kuhakikisha yanakaguliwa mara kwa mara.

“Chanzo ni ubovu tu wa maduara, kwa sababu yale maduara ni ya zamani sana, yale maduara yameanzishwa mwaka 2018, kwa hiyo nachoiomba Serikali na maispekta wake wawe wafanye juu chini ili kila duara wawe wanakagua mara zote, kwa sababu hii inaweza ikaathiri tukapoteza nguvu nyingi ya Taifa,” amesema Maige.

Naye Kelvin Jonas amesema siku ya tukio vijana hao waliwaazima tochi ili waingie duarani, lakini kesho yake walipokea taarifa za wenzao kuzama.

“Tukawaazima tochi wakaja huku maduarani, kesho yake tukasikia wale vijana wamepondwa duara, lile duara mazingira yake ni mabovu, lile duara sio zima kule ndani ina maana lile duara nguvu yake yameshaoza.

“Lile duara lilitakiwa lifanyiwe ukarabati kabla ya kuingia wale vijana; lilitakiwa lifanyiwe ukarabati. Sasa wanaendekeza tu kuingia kwa utaratibu huu watawamaliza vijana wengi sana,” amesema Jonas.

Ernest Maganga, mkaguzi mkuu wa migodi ya wachimbaji wadogo wilaya ya Kahama, amesema kilichotokea ni kwamba wakati wa shughuli za uchimbaji walikuwa wanarekebisha pampu kwa ajili ya kuvuta maji ndipo duara lilipomeguka kutoka juu na kuwaponda vijana hao.

“Mazingira ya tukio ni katika shughuli za uchimbaji walikuwa wanarekebisha pampu kwa ajili ya kuvuta maji ndipo Gema likafyatuka kutoka juu na kuwadhu,” amesema Maganga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Zimamoto wilaya ya Kahama, Stanley Luago, amethibitisha kupatikana kwa mwili wa mwanaume ambaye jina lake halikutambulika, huku jioni mwili mwingine ukiopolewa, na kufanya idadi ya miili hiyo kufikia miwili.

Jitihada za maokozi zinaendelea kumpata mchimbaji mmoja anayesadikiwa kunasa ndani ya duara hilo.

“Kazi inaendelea na matarajio ni makubwa na tupo hapa mpaka tuhakikishe ndugu zetu wote wamepatikana na wametoka katika hali zote, kama wamepoteza maisha au ni wazima, lakini tuko hapa mpaka tuhakikishe wametoka,” amesema Luago.

Related Posts