Marekani yairuhusu PEPFAR kuendeleza huduma hizi…

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) umejumuishwa katika msamaha wa misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha wakati wa kusitishwa kwa msaada wa kigeni kwa siku 90.

Miongoni mwa shughuli zilizoruhusiwa ni pamoja na utunzaji wa watu wenye VVU kwa lengo la kuokoa maisha, upimaji na ushauri, kuzuia na matibabu ya maambukizi ya kifua kikuu, huduma za maabara, ununuzi na usambazaji wa bidhaa za afya na dawa.

Pamoja na hayo, PEPFAR imeruhusiwa kutoa huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.

Licha ya Marekani kuwa mfadhili mkubwa zaidi wa misaada duniani, saa chache baada ya kuingia madarakani Januari 20, Rais Donald Trump aliamuru kusitishwa kwa misaada ya kigeni ili kuchunguzwa ikiwa inalingana na sera yake ya kigeni ya “Marekani Kwanza.”

Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, awali alitoa msamaha kwa misaada ya chakula cha dharura na kisha Jumanne kwa dawa za kuokoa maisha, huduma za matibabu, chakula, makazi na msaada wa kujikimu.

Hata hivyo, ukosefu wa maelezo katika agizo la Trump na misamaha iliyofuata umeyaacha makundi ya misaada bila uhakika kuhusu ikiwa kazi yao inaweza kuendelea.

Idara ya Afya ya Kimataifa na Usalama wa Kidiplomasia ya Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa taarifa ambayo imeonekana na Reuters, ikifafanua kuwa PEPFAR ilijumuishwa katika taarifa ya Januari 28 na kueleza shughuli gani zinaruhusiwa.

Shughuli hizo ni pamoja na huduma za matibabu na utunzaji wa watu wenye VVU kwa lengo la kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na upimaji na ushauri, kuzuia na matibabu ya maambukizi kama vile kifua kikuu (TB), huduma za maabara na ununuzi na usambazaji wa bidhaa za afya pamoja na dawa.

Pia inaruhusu huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwa mtoto.

“Shughuli nyingine zozote ambazo hazikutajwa waziwazi katika mwongozo huu, haziwezi kuanza tena bila idhini maalumu,” ilieleza taarifa hiyo.

Wauguzi wanatembelea baadhi ya maeneo maskini ya jiji ili kutoa huduma za msingi za afya kwa watu walio hatarini.

Zaidi ya watu milioni 20 wanaoishi na VVU, ambao ni theluthi mbili ya watu wote wanaoishi na ugonjwa huo na wanaopata matibabu duniani, wanasaidiwa moja kwa moja na PEPFAR.

Chini ya kusitishwa kwa msaada wa kigeni kwa Trump, malipo yote kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) yalisimama Januari 28 kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa fedha ulipoanza Oktoba mosi na hayajaendelea.

Kulingana na takwimu za Hazina ya Marekani, Jumatatu, Januari 27, USAID ililipa Dola milioni 8, na wiki iliyopita jumla ya Dola milioni 545.

Utawala wa Trump pia unachukua hatua za kupunguza mamlaka ya USAID na kuiweka chini ya Wizara ya Mambo ya Nje, kwa mujibu wa vyanzo viwili vilivyo na ufahamu wa majadiliano hayo siku ya Januari 31, katika kile ambacho kitakuwa mabadiliko makubwa ya jinsi Washington inavyotenga msaada wa kigeni wa Marekani.

Imeandikwa na Herieth Makwetta kwa msaada wa Mashirika

Related Posts