NYOTA mpya wa KenGold, Bernard Morrison ‘BM3’, huenda akakosa baadhi ya michezo ya kikosi hicho baada ya kupewa programu maalumu za mazoezi na kocha mpya wa timu hiyo, Mserbia Vladislav Heric, kabla ya kuungana na mastaa wenzake kikosini.
Akizungumza na Mwanaspoti, daktari wa timu hiyo, Amina Iddy Turusa alikiri nyota huyo kupewa program maalumu za mazoezi, huku akishindwa kuweka wazi kama ni majeruhi na anaweza akakosa michezo ijayo ya kikosi hicho hususani ujao wa Yanga.
Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa KenGold, Joseph Mkoko alisema wachezaji wote wako fiti kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Yanga, huku akikiri ni kweli nyota huyo amepewa programu na benchi la ufundi na anaendelea pia vizuri.
“Mambo mengine ni ya ndani na nisingependa kuyaweka wazi, itoshe kusema ni kweli anaendelea na mazoezi binafsi na suala la yeye kucheza au kutocheza dhidi ya Yanga, hilo litabakia maamuzi ya benchi la ufundi ila nyota wetu wote wako fiti.”
Hata hivyo, Mwanaspoti lilipewa taarifa nyota huyo wa zamani wa timu za Yanga na Simba bado hayuko fiti kucheza michezo ya hivi karibuni kutokana na majeraha aliyokuwa nayo, baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti na kukaa nje kwa muda mrefu.
Morrison ni miongoni mwa nyota waliobeba matumaini ya kikosi hicho baada ya kusajiliwa dirisha dogo akiungana na mastaa wengine waliotamba na Yanga na Simba wakiwemo beki, Kelvin Yondani, kiungo, Zawadi Mauya na mshambuliaji, Obrey Chirwa.
KenGold inayoburuza mkiani na pointi sita tu katika michezo 16 iliyocheza, itacheza dhidi ya Yanga Jumatano ya Februari 5, kwenye Uwanja wa KMC Complex, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mechi ya kwanza bao 1-0, Septemba 25, mwaka jana.
Nyota huyo wa zamani wa Simba na Yanga aliyewahi pia kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini, DR Congo na Morocco ni kati ya mwa wachezaji 24 waliosajiliwa na kutambulishwa hivi karibuni waliobeba matumaini ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza ikitoka Ligi ya Championship.