Dar es Salaam. Wakati wimbi la wachuuzi wanaowasha moto na kupika kwenye hifadhi za barabara likiongezeka, imebainika hali hiyo si hatari tu kwa barabara bali inaweza kuleta madhara kwa miundombinu mingine inayowekwa kwenye hifadhi hiyo kama inavyoelezwa kwenye sheria.
Kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya Mwaka 2007 Sheria Namba 13, Kifungu Namba 29, hifadhi ya barabara, ndani yake kunaweza kupitishwa miundombinu mingine ya umeme, simu, majisafi na majitaka, miundombinu ya gesi, mabango ya matangazo na mitaro ya majitaka.
Hifadhi nyingi za barabara za Jiji la Dar es Salaam zina miundombinu ya umeme na uchunguzi wa Mwananchi umebaini wapo wafanyabiashara wa vyakula wanaowasha moto na kupika chini au jirani kabisa na miundombinu hiyo inayohusisha nguzo na transfoma.
Katika eneo la Tazara kuna wafanyabiashara wanaopika vitafunwa na aina nyingine za vyakula jirani kabisa na miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) iliyopo kwenye hifadhi ya barabara.
Mmoja wa wafanyabiashara eneo hilo ambaye hakutaka kutaja jina lake, amekiri wanafahamu hawaruhusiwi kufanya biashara hapo lakini wanalazimika kutokana na kuwepo mzunguko wa biashara asubuhi.
“Hapa ni kama center, wafanyakazi wa kampuni nyingi katika maeneo ya jirani wanapita hapa asubuhi kuchukua vitafunwa na kama unavyofahamu ukiwa barabarani utawapata wateja wengine ambao ni wapita njia, ndiyo maana biashara inafanyika asubuhi tu,” amesema.
Kuhusu kufanya upishi jirani na miundombinu ya umeme, amesema hilo hutokea pale panapokuwa na jua kali lakini mara nyingi anajitahidi kuwa pembeni.
Alipoulizwa kama anafahamu kufanya biashara inayohusisha moto kwenye hifadhi ya barabara na miundombinu ya umeme ni hatari, amesema anazingatia hatua zote za tahadhari.
“Hata kama nawasha moto siwezi kuwasha jirani kabisa na waya wa umeme, lazima jiko niweke pembeni, halafu huku niliko ni ngumu kusema gari inaweza kufika labda awe amedhamiria kusababisha ajali,” amesema.
Hali kama hii inaonekana pia eneo la Mbagala Mzinga, wachuuzi wa vitoweo wanawasha moto na kupika jirani na ilipo miundombinu ya umeme ambayo ipo kwenye hifadhi ya barabara.
Mfanyabiashara eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Rajabu amesema:“Kinachonifanya niwe hapa ni wateja, watu wakishuka kwenye daladala ndiyo wanaangalia mboga, sasa ukisema nikajiweke pembeni unafikiri nani atanifuata, halafu hapo unaposema kuna umeme nisipokaa mimi atakuja mwingine atakaa.”
Mmoja wa maofisa wa Tanesco ambaye hakutaka kuandikwa jina lake, amekiri kuwepo changamoto ya miundombinu yao kuvamiwa na watu wanaofanya shughuli mbalimbali.
Amesema kwa mujibu wa nyaraka ya kimataifa ya uhandisi (Engineering instruction document) ambayo imethibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), umbali ambao miundombinu ya umeme inapaswa kuwa mbali na watu.
Mwongozo huo unaonesha kwenye miundombinu inayopitisha umeme kv11 unapaswa kuachwa umbali wa mita 5 sawa na mita 2.5 kila upande, kv33 ni mita tano kila upande, kv66 mita 10 kila upande wakati kv132 mita 20 kila upande.
Katika miundombinu inayopitiwa na umeme kv 220 inapaswa kuachwa umbali wa mita 30 kila upande, kv 330 umbali wa mita 40 kila upande na 400kv mita 40 kila upande.
“Kuna umbali ambao unaelekezwa na vitabu vya kimataifa kwamba wapi miundombinu ya umeme inapita kulingana na umbali na kiwango cha msongo wa umeme unapopita na watu wanapovamia upo uwezekano wa kutokea hatari.
“Kutokea kwa hatari kunasababishwa na vihatarishi vilivyopo, kwanza umeme wenyewe ni hatari, sasa kama mtu anapoweka moto jirani na miundombinu ya umeme hatari yake inaweza kuwa kubwa zaidi, uzuri ni kwamba hazitokei ajali mara kwa mara ila pale inapotokea ndiyo inaonekana kuna uzembe umefanyika,” amesema.
Hata hivyo, ofisa huyo amesema hali hiyo ya uvamizi wa maeneo yenye miundombinu ya umeme ni matokeo ya kukosekana kwa maeneo sahihi ya kufanyia biashara.
“Huwa hatuendi moja kwa moja kwenye kuchukua hatua, tunawapa elimu huku tukiangalia hawa watu wanakwenda wapi wakati hakuna maeneo ya kufanyia shughuli zao, kwa hiyo kinachofanyika ni elimu kwa umma.”
“Pia, huwa tunachukua hatua ya kuweka alama za hatari, unapojenga ‘line’ ni lazima uweke ‘signs,’ kuna maeneo ambayo alama zinawekwa lakini bado watu wanavamia ndiyo maana tunaweka msisitizo kwenye elimu,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tanesco, Irene Mwangomo amekiri ni kweli yapo maeneo ambayo miundombinu ya umeme inavamiwa na watu na shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa umma.
Irene amesema moja ya maadili ya msingi ya Tanesco ni usalama, hivyo inafanya jitihada zote kuhakikisha miundombinu inakuwa salama kwa umeme salama kwa wateja, kwani inapotokea wateja wetu pia huathirika hata kwenye suala la kukatika katika kwa umeme.
Amesema kupitia vyombo vya habari kama vile runinga, redio na yanapofanyika maonesho mbalimbali ambayo shirika hilo hushiriki, watalaamu huzungumza na watu kuhusu umuhimu wa kukaa mbali na miundombinu.
“Katika hili tumekuwa tukishirikisha jamii kama sehemu ya kutengeneza uwajibikaji. Kushirikiana na serikali za mitaa na vijiji kuwaondoa watu hao kwa kuwapa sehemu mbadala. Na kuna maeneo ambayo watu wameondolewa ili kuhakikisha usalama wao.
“Mbali na hilo, hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuweka alama za tahadhari kwenye miundombinu na sehemu hatarishi. Kuhusu hatua, kuna watu walishachukua hatua lakini kuna mambo mengi yanafanyika katika kulitekeleza hilo, hivyo hiyo huwa ni hatua ya mwisho,” amesema Irene.
“Hatua zinachukuliwa na huangalia mambo mbalimbali na kabla ya kuchukua hatua shirika limehakikisha muhusika amepewa elimu ili kupima dhamira hasa ya kufanya vitendo hivyo.”
Hata hivyo, ameeleza kuna changamoto ya watu kutafuta sehemu za kufanyia biashara, hivyo kujikuta wanafanya biashara chini au pembeni ya miundombinu na kuleta athari.
“Kuna ajali ambazo zimeripotiwa zinazohusiana na watu kufanya shughuli za kijamii chini au karibu na miondombinu kama vile gereji ambako vyuma kama nondo vikigusa nyaya za umeme na kusababisha vifo au magari marefu yaliyopaki chini ya miundombinu na watu kufanya kazi juu, hivyo kunaswa na umeme,” amesema Irene.
Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Puyo Nzalaiyimisi amesema hawajawahi kukutana na tukio la moto kwa wafanyabiashara barabarani kwa kuwa wanatoa elimu kutoka ngazi ya chini.
“Mradi wetu wa kwanza wa elimu ni mwananchi wa kawaida kwa hiyo wapika chipsi, vyakula, kuchomelea na gereji wote wanufaika wa elimu hii na tunachokazania ni kuhusu usalama wa muhusika mwenyewe,” amesema Nzalaiyimisi.
Amesema hata ujenzi wa vibanda na maeneo wanayofanyia biashara wamesogeleana na hawaruhusu mtu kutokuwa na mtungi wa kuzimia moto na wamekuwa wakifanya doria za mara kwa mara kuhakikisha wafanyabiashara wanafahamu namna ya kujiokoa linapotokea tatizo.
Katika maeneo hayo, amesema kuna wazima moto wa kujitolea na vilabu vya zimamoto vilivyojikusanya maeneo husika ambavyo vinafahamu namna ya kudhibiti moto unapotokea.
“Hatuwezi kufanya mambo hayo wenyewe, hivyo tunashirikiana na mamlaka nyingine kama halmashauri za miji kuhakikisha hata maeneo madogo madogo yanakuwa salama,” amesema.
Amesema kati ya Aprili na Septemba 2024 jeshi hilo lilitoa elimu dhidi ya majanga ya moto na tahadhari zake na kuwafikia wanufaika 607,714.
Elimu hiyo ilitolewa kupitia runinga, redio, mikusanyiko katika masoko, vituo vya mabasi, nyumba za ibada, shule za msingi na sekondari pamoja na vikundi vya skauti na klabu za zimamoto.
Usikose sehemu ya pili ya habari hii kesho