Mpanzu: Msijali, mabao yatakuja | Mwanaspoti

MECHI saba tu zimetosha kwa kiungo wa Simba Ellie Mpanzu kuweka wazi kuhusu kile kilichompeleka katika kikosi hicho, huku akiweka wazi kuwa hana presha kabisa ya kufunga.

Mpanzu ambaye alianza kucheza baada ya dirisha dogo, amecheza mechi nne za ligi na kutoa asisti mbili(dakika 220) tatu za kimataifa sawa na dakika 258.

Tangu atue kwenye kikosi hicho cha kocha Fadlu David, amekuwa akianza kikosi cha kwanza katika mechi za ligi na kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mpanzu alisema, kwa sasa hana presha hasa ya kufunga kwani hilo sio lengo lake la kwanza ndani ya timu.

Alisema, jambo la muhimu zaidi kwake ni timu kupata ushindi si yeye awe miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye mechi husika na amefanya juhudi za mafanikio hayo.

“Wala siwazi sana kuhusu kufunga kwani najua magoli yatakuja, lengo langu hasa ni kuhakikisha timu inapata ushindi na sio kupoteza, ila furaha yangu siku zote ni pale ninapohusika katika mafanikio. Bado muda upo na mapambano yanaendelea, licha ya ushindani mkubwa wa namba uliopo ila naiona nafasi ya kufanya vizuri ipo,” alisema Mpanzu na kuongeza;

“Wachezaji wote wa Simba ni bora na wana viwango vikubwa kupata nafasi haimaanishi wewe ni mkali ila tu ni machaguo ya mwalimu kutokana na mechi husika na ninamshukuru Mungu kwa hilo. Naelewa mashabiki wanachotaka ila mafanikio ya timu ni ya kila mchezaji na ndio maana tunapambania kuhakikisha inapata matokeo kabla ya kuangalia mchezaji mmoja mmoja ana rekodi gani kwanza.”

Mwishoni mwa mwezi uliopita, kocha wa Simba, Fadlu Davids aliwatoa hofu mashabiki wa Simba baada ya Mpanzu kutokufunga bao lolote katika mechi tatu za ligi, huku akisema ni swala la muda na winga huyo ni mchezaji bora.

Katika eneo la kiungo cha ushambuliaji wanaofanya vizuri kwa sasa ni Jean Charles Ahoua mwenye mabao saba na asisti tano, Awesu Awesu aliyefunga mabao mawili na kuasisti moja, Ladack Chasambi mwenye asisti tatu na Edwin Balua aliyefunga mabao mawili pia.

Related Posts