Dar es Salaam. Yalikuwa ni mauaji ya kikatili, ndivyo unaweza kuelezea mauaji ya askari watatu wa Jeshi la Polisi waliokuwa lindo katika benki ya CRDB jijini Dar es Salaam, kuuawa kwa kupigwa risasi na kuporwa bunduki mbili, ikiwamo AK-47.
Ni kutokana na mauaji hayo yaliyotokea Agosti 23, 2016 katika eneo la benki ya CRDB Mbande katika wilaya ya Ilala, Januari 30, 2025 mahakama imemtia hatiani Mbwana Suleiman Puga, na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Hussein Mtembwa wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, ambaye alisema mikono yake imefungwa na kiapo alichoapa kulinda Katiba na sheria za nchi, hivyo anamhukumu adhabu stahiki ya kifo kwa kosa hilo.
Maelezo ya upande wa mashtaka ni kuwa siku ya tukio, polisi wawili walikuwa lindo katika benki hiyo na wakati wanakabidhiana zamu na wenzao wawili, kundi la watu wenye silaha liliwavamia kwa kuwashtukiza na kuwashambulia kwa risasi.
Katika shambulizi hilo, polisi watatu G.9996 konstebo Gaston, E.5761 Koplo Yahaya na F.4666 koplo Khatibu waliuawa papo hapo kwa risasi wakati mwenzao G.9524 Kostebo Tito alijeruhiwa vibaya na kufariki akipatiwa matibabu hospitalini.
Ilielezwa kuwa katika shambulio hilo, bunduki moja aina ya Avtomat Kalashnikov (AK-47) na nyingine aina ya Semi-Automatic Rifle (SAR) ziliporwa na watu hao.
Haikuishia hapo kwani watu hao walikwenda kituo kidogo cha polisi kilichopo jirani cha Mbande na kuiba sare za Polisi na kwa msaada wa wananchi, miili ya askari hao pamoja na aliyejeruhiwa, ilipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Uchunguzi wa miili ya marehemu, ilibaini vifo vyao vilitokana na majeraha mabaya ya risasi na kupoteza damu nyingi na baada ya uchunguzi wa kina wa polisi, Mbwana Suleiman Puga alikamatwa na Polisi Agosti 11, 2017.
Ilielezwa baada ya kuhojiwa na makachero wa Jeshi la Polisi, alikiri kuhusika na tukio hilo na aliwaongoza polisi mahali alipokuwa amehifadhi bunduki mbili aina ya SAR na moja SMG, risasi 31 na waya 69 za kulipuliwa mabomu. Puga alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka manne ya mauaji ya askari hao na kuyakanusha, ambapo upande wa mashtaka ukalazimika kuita mashahidi 13 na kuwasilisha vielelezo halisi na nyaraka 14 kuthibitisha mashtaka hayo.
Shahidi wa kwanza aliyepewa jina la “P” alieleza Agosti 23, 2016 saa 1:00 usiku, akiwa kituo cha polisi Mbande, alipokea simu kutoka kwa askari mwenzake aliyekuwapo zamu CRDB Mbande kuwa wameshambuliwa na watu wenye silaha.
Wakati akitoa taarifa hiyo, polisi huyo alikuwa ametoroka kutoka eneo la tukio na alikuwa amejificha mahali, ndipo alikusanya polisi wengine na kwenda eneo la tukio wakitumia gari la kiraia na alipofika alishuhudia miili ya askari watatu.
Alijulishwa pia polisi mwingine, Konstebo Tito alikuwa amejeruhiwa vibaya na alikuwa amepelekwa MNH na raia wema na hapo alimfuata polisi aliyekuwa amejificha akiwa na hofu na katika tukio hilo baya, walipoteza askari wanne.
Shahidi wa pili aliyepewa jina la “P1”, alieleza siku ya tukio, aliripoti kituo cha Polisi Mbagala na walikuwa wamepangiwa zamu CRDB Mande yeye na Koplo Hatibu na kama ilivyokuwa utaratibu, wote walichukua bunduki aina ya AK 47.
Waliingia katika gari la polisi na kwenda hadi eneo la kazi na kufika salama lakini wakiwa pale walivamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana na yeye alikuwa amesimama karibu na Koplo Hatibu na muda kidogo alimuona amelala chini.
Naye alilala chini wakati anaandaa bunduki yake aina ya AK-47 ambazo hujulikana pia kama Sub Machine Gun (SMG), alibaini ilikuwa haifanyi kazi sawa sawa na wakati huo huo wauaji hao waliendelea kuwashambulia kwa mvua ya risasi.
Alifanikiwa kutoroka eneo hilo na kwenda kujificha nyumba ya jirani huku milio ya risasi ikiendelea kusikika na ndipo alipoweza kumpigia simu shahidi wa kwanza na kumjulisha nini kimetokea, na milio iliendelea kusikika na baadae ikakoma.
Alieleza baadaye shahidi wa kwanza alifika akiwa na askari wengine wakiwa na gari ya kiraia ambapo kwa pamoja walikwenda hadi eneo la tukio na kushuhudia miili ya askari wenzako watatu wakiwa wamekufa.
Shahidi wa tatu, “P2”, alieleza siku ya tukio alikuwa akitengeneza gari lake nje ya benki ya CRDB Mbande na akiwa pale, lilikuja gari la polisi aina ya Leyland Ashork namba PT 38889 likiwa na askari kwa ajili ya kulinda benki hiyo.
Alieleza polisi mmoja alishuka katika gari hiyo na alipigwa risasi na watu asiowajua na mwingine aliyeshuka katika gari hilo naye alipigwa risasi na mwingine naye aliposhuka kwenye gari naye alishambuliwa kwa risasi.
Polisi mwingine alichukua bunduki na kujaribu kufyatua risasi lakini haikufanya kazi na ndipo alipoamua kujificha na aliwashuhudia watu hao wakielekea kituo kidogo cha Polisi cha Mbande na aliporudi eneo la tukio alikuta miili mitatu.
Shahidi wa nne “P3”, alieleza Agosti 24, 2016 alipewa jalada la mauaji ya askari wenzake wanne ambapo alikwenda eneo la tukio la kuchora ramani ya eneo hilo na kwenda MNH na kushiriki uchunguzi wa miili ya askari hao wanne.
Takribani baada ya kupita mwaka mmoja, alipata taarifa za mahali alipomshukiwa wa mauaji hayo aitwaye Puga na Aprili 12, 2017 akiwa na kikosi kazi walifanikiwa kumkamata mshukiwa huyo na kumweka mahabusu kituo cha Mbagala.
Siku iliyofuata alipangiwa kuchukua maelezo ya mtuhumiwa huyo na alipotaka kutoa maelezo hayo kama kielelezo upande wa mashitaka ulipinga, lakini baada ya kesi ndani ya kesi kusikilizwa, mahakama iliyapokea maelezo hayo kama kielelezo.
Alieleza Aprili 14, 2017 akiwa na askari wenzake pamoja na mtuhumiwa, walikwenda eneo la Kisiju huko Mkuranga, Mkoa wa Pwani ambapo mtuhumiwa alionyesha silaha mbalimbali zikiwamo bunduki mbili zilizokuwa zimeporwa katika eneo la tukio.
Mashahidi wengine ambao ni askari polisi katika idara mbalimbali ikiwamo uchunguzi wa milipuko (ballistic expert) walieleza namna walivyoshiriki kuchunguza tukio hilo, kutunza vielelezo na miili ya wenzao ilivyochunguzwa.
Katika utetezi wake, mshtakiwa aliyejitambulisha kama anajishughulisha na kuuza duka katika eneo la Mbagala Zakhiem, jijini Dar es Salaam, alisema siku ya tukio alikuwepo kazini kwake kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 4:00 usiku.
Akaeleza Aprili 11, 2017, alikuwepo kazini kwake kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku na siku iliyofuata ratiba yake ilikuwa hiyo hiyo lakini siku hiyo aliondoka kazini kwake mapema saa 1:00 usiku na kurudi nyumbani anakoishi.
Akiwa nyumbani, alipokea mgeni aitwaye Athman Usonzo ambaye ni mtoto wa shangazi yake ambapo ilipofika saa 2:00 usiku, alisikia mlango wake ukigongwa na akaenda kuufungua, ndipo alipogundua waliokuwa wakigonga ni askari polisi.
Waliwakamata wote wawili na kuwapeleka kituo cha Polisi Tazara na kuwaweka mahabusu tofauti ambapo siku iliyofuata, alifika polisi ambaye hakujitambulisha akiwa na karatasi mkononi na kumlazimisha aweke saini yake lakini alikataa.
Mei 26, 2017 alipelekwa Mahakama ya Wilaya ya Temeke ambapo alichanganywa na washtakiwa wengine wanne na kusomewa mashtaka ya mauaji lakini Aprili 7, 2022 mkurugenzi wa mashitaka (DPP) aliondoa shitaka dhidi ya wanne hao.
Hukumu ya Jaji ilivyokuwa
Katika hukumu yake, Jaji Mtembwa alisema kulingana na ushahidi ikiwamo ripoti ya daktari na maelezo ya onyo ya mshtakiwa mwenyewe akieleza mwanzo mwisho ushiriki wake, ni wazi vifo vya askari hao vilikuwa na mkono wa mtu.
“Kwa kuegemea ushahidi wa shahidi wa 1,2,3,7,13 na vielelezo namba 10 na 14 ninaridhika askari hao kwa sasa ni marehemu. Kulingana na ushahidi wa shahidi wa 7 na 13 na vilelezo P10 na P14 vifo vyao havikuwa vya asili,” alisema.
Lakini Jaji akasema swali linalobakia kwa mahakama kulijibu ni kama upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha shtaka hilo pasipo kuacha mashaka yoyote kuwa ni mshtakiwa na wengine ambao hawajakamatwa, ndio walioua askari hao.
“Hoja ya pili ni kama mshtakiwa ndio aliwajibika na vifo vya marehemu hao na kama ndio, ni je mauaji hayo yalikuwa na dhamira ovu ndani yake?” alisema Jaji katika hukumu yake hiyo iliyopatikana katika mtandao wa mahakama wa TanzLii.
Jaji alisema, kulingana na ushahidi uliotolewa, hakuna mtu aliyeshuhudia au kumuona mshtakiwa akiwaua askari hao, lakini shahidi namba 2 na 11 wanasema waliwatambua wauaji hao kwa jinsia, siyo sura zao.
Jaji alieleza kuwa ungamo linalotolewa na mshukiwa mbele ya mashahidi wanaoaminika, iwe ni raia au polisi, linaweza kutumika kumtia hatiani kwa kuwa ushahidi wa aina hii ni bora katika kesi za jinai, hasa akilitoa kwa hiyari.
Kulingana na maelezo yake ya ungamo, mshtakiwa alisema kuwa Agosti 2016 alialikwa na Amiri waende Kisiju, akiwa na watu wengine aliowataja kuwa ni Hassan, Shujaa, Ibrahim Ultule, Mwalami Amiri, na Ukewa.
Mbali na hao, alikiri kuwa walikuwepo Omary Mpili, Mussa Omary Mpili, Mussa Omary Makongwa, na Shamte Ally. Walipofika, Amiri alieleza kazi waliyoenda kufanya dhidi ya askari Polisi CRDB tawi la Mbande.
Alieleza kuwa mchana wa Agosti 23, 2016 walikwenda katika benki hiyo wakiwa na hijab na silaha za moto, ambapo Amiri aliwataka wavae hijab katika shambulio hilo na wawahi kukutana baadaye katika kambi ya Vigozi.
Aliendelea kueleza kuwa Amiri alikodisha pikipiki aina ya Boxer ambazo zingetumika katika shambulio hilo, na alimpa bunduki aina ya SMG, na kumuelekeza kukaa karibu kabisa na eneo ambalo gari la Polisi lingepita.
Kulingana na Jaji, mshtakiwa alieleza kuwa aliona gari la polisi likija CRDB Mbande majira ya saa moja usiku, alikivaa hijab na kuanza kuwashambulia polisi, ambao walianguka chini na kisha kuchukua silaha zao.
Wakati tukio likiendelea, mshitakiwa alikimbilia kituo kidogo cha Polisi cha Mbande, akachukua sare za Jeshi la Polisi, na baadhi ya washirika walifika wakiwa na pikipiki na wote walielekea Vigozi kukutana na Amiri.
Jaji alisema maelezo haya yalikuwa yanaungana na ushahidi wa mashahidi mbalimbali wa kilichotokea siku hiyo. Kwa hivyo, ushahidi kwa ujumla wake unamtia hatiani mshitakiwa, na adhabu ya kosa hili ni kunyongwa hadi kufa.