Manchester, England. Mshambuliaji Marcus Rashford, amefurahia kutua kwenye kikosi cha Aston Villa akisema kuna timu nyingi zilimtaka lakini hii ilikuwa chaguo lake la kwanza.
Rashford ametua Aston Villa akitokea Manchester United kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu na kama timu hiyo itaridhishwa naye itamnunua moja kwa moja kwa kitita cha pauni 40 milioni.
Staa huyo amekuwa hana uhusiano mzuri na kocha mpya wa Manchester United, Ruben Amorim, kuanzia kocha huyo alipotua kwenye timu hiyo.
“Nimefurahi sana kutua kwenye kikosi cha Aston Villa. Nilikuwa na bahati ya timu nyingi kunitaka, lakini Villa lilikuwa chaguo langu rahisi sana, napenda jinsi wanavyocheza msimu huu, nifuraha kuwa hapa na nasubiri kwa hamu kubwa siku ya kuingia uwanjani,” alisema Rashford wakati anatambulishwa.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa mshambuliaji huyo ambaye ameitumikia timu ya Taifa ya England mechi 60 anatarajiwa kuendelea kupokea kitita chake kilekile cha mshahara cha pauni 350,000 kwa wiki na mkataba wake na United unatarajiwa kumalizika Juni 2028.
Makubaliano ni kwamba Villa watalipa asilimia 70 ya mshahara huo, huku mambo mengine yakiwa makubaliano yao na Man United.
“Nina huzuni kwa jinsi Rashford alivyoondoka United, alikuwa pale kuanzia akiwa na miaka minane, amefunga mabao mengi, lakini maisha yake kipindi cha mwisho na timu hiyo hayakuwa mazuri, kwangu siyo jambo la furaha,” alisema staa wa zamani wa United, Gary Neville.
Rashford hajafanikiwa kuitumikia United kuanzia Desemba mwaka jana baada ya kuanza kuvurugana na kocha Ruben Amorim.
Staa huyo mwenye miaka 27 amekosa michezo 12 msimu huu baada ya kocha wake kulalamika kuwa staa huyo hajitumi mazoezini.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Rashford kuitumikia timu nyingine tofauti na United baada ya kukaa kwenye timu hiyo kuanzia akiwa na miaka nane.
Rashford amefanikiwa kufunga mabao 138 akiwa na United baada ya kucheza michezo 426 na sasa anaangana na timu hiyo.