Samia awaonya majaji, mahakimu wanaogeuka ‘miunguwatu’

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka majaji na mahakimu wa mahakama mbalimbali, kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano ya kisheria na kikatiba, badala ya kuwa miunguwatu.

Amelifafanua neno miunguwatu, akilihusisha na binadamu wanaotekeleza wajibu wao kwa kujipa ukubwa unaofanana na ule wa Mwenyezi Mungu, jambo alilosema watumishi wa taasisi za haki jinai na madai hawapaswi kuwa nalo.

Rais Samia ameyasema hayo jijini Dodoma leo, Jumatatu Februari 3, 2025 wakati akuhutubia sherehe za maadhimisho ya siku ya sheria nchini.

Ameitoa kauli hiyo kukazia kile kilichoibuliwa na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi ambaye awali aliwataka mahakimu na majaji wasitengeneze mazingira ya kuchelewesha kesi mahakamani (Legal Engineering).

 “Kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu, ambayo mbali ya kutoa haki ana kudra na jaala, anaweza kuamua akupe au akunyime sasa hiyo ni kazi ya Mungu,” amesema.

Kwa upande wa majaji na mahakimu, amesema wao ni mawakala wa utoaji haki duniani, lakini mmenyimwa jaala na kudra hivyo hawa uwezo wa kuamua kutoa au kumnyima binadamu.

 “Kwa hiyo mnafanya kazi yenu kwa kufuata makubaliano yetu kikatiba na sheria za nchi kama tulivyoziweka,” amesema.

Kwa sababu hiyo, amewataka wasiwe miunguwatu kwa kuwa hawana jaala wala kudra, hivyo watoe haki kwa kufuata misingi waliyokubaliana na iliyowekwa kisheria na kikatiba.

Amewasisitiza wanapouanza mwaka mpya wa Mahakama wadhamirie kukaa upande wa haki na waizingatie wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.

Ameyasema hayo akirejea hotuba ya mwaka 1984 iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyewaambia majaji kuwa kazi yao inahitaji uadilifu na nidhamu isiyotiliwa shaka.

Mkuu huyo wa nchi ametumia jukwaa hilo, kujibu hoja mbalimbali za Mwabukusi ikiwemo maboresho ya masilahi bya mahakimu, akisema linaendelea kufanyiwa kazi.

“Maombi haya yalikuja katika mwaka huu wa fedha hayakuwa kwenye bajeti tumejitahidi kubana na kuanza na yale yanayowezekana kuanza, lakini mengi yatakuja Julai mwaka huu wakati wa bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja,” amesema.

Kuhusu pendekezo la Mwabukusi lililotaka sheria zitungwe kwa kuwashirikisha wananchi wote, Rais Samia amesema ndivyo inavyofanyika na ataendelea kuboresha.

Jambo lingine alilogusia kutoka ka Rais huyo wa TLS ni kutungwa kwa sheria zinazolinda rasilimali za nchi, akisema ni suala muhimu na litafanyiwa kazi.

Amemtaka Mwabukusi akae na Wizara ya Katiba na Sheria, kuangalia namna ya kuboresha sheria ya TLS ili kuikipa mamlaka chama hicho cha kusimamia maadili ya mawakili.

Amegusia pia suala la kueleweka kwa kazi ya mawakili, akisema ni jambo linalohitaji elimu ya kisheria na alimtaka Mwabukusi ashirikiane na wenzake kuitoa.

Amesema anafanya namna kuhakikisha wanauwezesha mfuko wa TLS ili itekeleza majukumu yake bila changamoto.

Kwa kuwa Mwabukusi aliahidi kuendelea kupokea msaada wowote utakaowezesha kutekeleza wajibu wa TLS, Rais Samia amemwambia ataangalia linalowezekana kukipatia chama hicho gari lingine, mbali na lile kilichopewa na Wizara ya Katiba na Sheria.

Related Posts