Dar es Salaam. Kiongozi wa Idara ya Ufanisi wa Serikali (Doge) Elon Musk, ametangaza kuwa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) linapaswa ‘kufa’ huku kukiwa na ripoti kuwa maofisa wawili waandamizi wa usalama wa shirika hilo wamepewa likizo kwa kukataa kuwapa wawakilishi wake ufikiaji wa nyaraka za siri.
Taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa, maofisa wote wa juu waliosimamia miradi kutoka nchi mbalimbali zilizopokea ufadhili, nao wamerudishwa Marekani kwa sasa.
Kwa mujibu ya Shirika la Habari la Aljazeera, Musk aliyeteuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump kuongoza idara hiyo ameiita USAID ‘shirika la uhalifu’ baada ya maofisa wa usalama kuripotiwa kuwanyima wanachama wa kikosi chake cha kupunguza gharama, fursa ya kuingia maeneo ya siri katika makao makuu ya shirika hilo jijini Washington, DC.
“Ni wakati wake kufa,” kiongozi huyo wa Doge na tajiri namba moja duniani aliandika kwenye jukwaa lake la mitandao ya kijamii la X.
Mkurugenzi wa Usalama wa USAID, John Voorhees na Naibu wake, Brian McGill, walipewa likizo baada ya kuwakatalia maofisa wa Doge kuingia maeneo salama kwa sababu hawakuwa na idhini ya kiusalama, vyombo kadhaa vya habari vya Marekani viliripoti.
Hata hivyo, wanachama wa Doge, kupitia agizo la kiutendaji la Trump lakini si idara rasmi ya Serikali, waliweza kupata ufikiaji wa maeneo yenye taarifa za siri baada ya mvutano huo, kulingana na ripoti kadhaa, ikiwamo ya kwanza kuripotiwa na CNN.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu ya Marekani, Steven Cheung alikanusha kuwa, maofisa wa Doge walijaribu kuingia katika maeneo yenye usalama wa hali ya juu, akitaja ripoti ya PBS kuhusu tukio hilo kuwa ni ‘habari za uongo’ na ‘si kweli hata kidogo.’
“Hivi ndivyo vyombo vya habari visivyo makini na visivyoaminika,” Cheung aliandika kwenye X.
Hata hivyo, Katie Miller anayehudumu Doge, alionekana kuthibitisha jaribio la kikosi hicho cha kazi kuingia ndani, akiandika kwenye X kwamba, “hakuna nyenzo za siri zilizoangaliwa bila idhini stahiki za kiusalama.”
Tukio hilo limeongeza hofu kwamba Trump, ambaye ameweka kizuizi karibu msaada wote wa kigeni, anapanga kupunguza kwa kiasi kikubwa au hata kulivunja kabisa Shirika la USAID.
Februari mosi, tovuti ya USAID ilizimwa, huku ukurasa wa shirika hilo ukionekana kwa muundo rahisi kwenye tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, jambo lililochochea uvumi kuwa shirika hilo lingefutwa na kuhamishiwa kwenye wizara inayoshughulikia sera za nje.
“Rais Trump ametumia wiki mbili kuwahangaisha na kuwaachisha kazi wafanyakazi wa USAID, na sasa timu yake inajaribu kuliharibu shirika hilo kabisa,” Chris Coons, seneta wa chama cha Democratic kutoka Delaware, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X.
Jeremy Konyndyk aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Ofisi ya Misaada ya Maafa ya USAID kati ya 2013 na 2017, alisema kufuta USAID bila idhini ya Bunge la Marekani ni kinyume cha sheria na ni uvunjaji wa mgawanyo wa madaraka unaolindwa na Katiba ya Marekani.
“Kama jaribio hili litafaulu na iwapo Trump (au Elon) wanaweza kupuuza sheria za Bunge na maagizo ya ufadhili, na Bunge likanyamaza, basi hii ni ishara mbaya sana na haitasimama kwa USAID pekee,” Konyndyk aliandika kwenye X.
Wabunge wa Chama cha Democratic, pia wameeleza wasiwasi wao kuhusu ushawishi mkubwa wa Musk katika Serikali licha ya kutoshikilia wadhifa wa kuchaguliwa.
Mvutano wa Musk na USAID unakuja baada ya The New York Times na Shirika la Habari la Associated Press, kuripoti mwishoni mwa wiki kwamba, Doge ilipata ufikiaji wa mfumo wa malipo wa Serikali kuu, unaoshikilia taarifa nyeti kibinafsi za mamilioni ya Wamarekani.
“Hii ni hatari kubwa,” aliandika Mbunge wa New York Alexandria Ocasio-Cortez kwenye X.
“Watu walimchagua Donald Trump kuwa Rais si Elon Musk. Kuwa na bilionea asiyechaguliwa, mwenye madeni na masilahi binafsi ya kigeni, akiiba taarifa za siri za Marekani ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa. Hili halipaswi kuwa suala la vyama vya kisiasa.”
Jumapili, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa utawala wake utaondoa, “wazimu wa mlengo wa kushoto,” kutoka USAID kabla ya kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake.
Baadaye Trump aliweka msisitizo kwa misaada ya Afrika Kusini, akiahidi kusitisha ufadhili wote wa baadaye kwa nchi hiyo kutokana na unyang’anyi wa ardhi na kwa mujibu wake, kuwaumiza watu wengine.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wiki iliyopita alisaini sheria yenye utata, inayoruhusu unyang’anyi wa ardhi ya wakulima Wazungu bila fidia katika baadhi ya matukio.
Marekani ilitenga takriban Dola 440 milioni kwa msaada wa Afrika Kusini mwaka 2023, kulingana na takwimu za Serikali ya Marekani.
“Marekani haitakubali hili, tutachukua hatua,” Trump aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social, akiongeza kuwa, zuio la ufadhili litadumu hadi uchunguzi kamili wa hali hiyo utakapokamilika.
Marekani ndiyo mfadhili mkubwa zaidi wa misaada ya kigeni duniani, ingawa chini ya asilimia 1 ya matumizi yake huenda kwa misaada hiyo na baadhi ya nchi hutoa misaada zaidi kulingana na asilimia ya bajeti zao.
Washington ilitoa jumla ya Dola 72 bilioni katika misaada ya kigeni kwa takriban nchi 180 mwaka 2023, huku zaidi ya nusu ya fedha hizo zikisambazwa kupitia USAID.
Nyongeza kwa msaada wa Mashirika