Simba yaweka kambi ya muda Dodoma

Dar es Salaam. Baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Tabora United, juzi Jumapili, Simba imeamua kuweka kambi ya muda ya siku mbili Dodoma kabla ya kuelekea Babati siku moja kabla ya mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate, Februari 6 katika Uwanja wa Kwaraa.

Msafara wa timu hiyo uliondoka jana asubuhi Tabora na kufika Dodoma ambako utakaa hadi kesho asubuhi na kuanza safari ya Babati ambako sio mbali sana na kabla hata jua halijawa kali itakuwa imeshawasili.

Sababu mbili zimechangia Simba ifanye uamuzi huo ambazo ni kupunguza umbali wa safari ili isiwachoshe wachezaji lakini nyingine ni kukosekana kwa viwanja bora vya mazoezi Babati.

Hesabu za kwanza za Simba zilikuwa ni kuweka kambi Arusha lakini ikagundua kwamba safari ingekuwa ndefu zaidi tofauti na iwapo ikiweka kambi Babati.

Kama kambi ingekuwa Arusha, Simba ingelezimika kutembea zaidi ya kilomita 829 ambazo zinajumuisha umbali wa kutoka Tabora hadi Arusha lakini pia umbali wa kutoka Arusha hadi Babati.

Kwa mujibu wa vipimo vya wakala wa taifa wa barabara Tanzania (Tanroads), umbali wa Tabora hadi Arusha ni kilomita 661 na ule wa Arusha kwenda Babati ni kilomita 168 hivyo ingesafiri kilomita 829 hadi itakapocheza mechi hiyo.

Lakini kwa kukaa Dodoma, Simba inapunguza umbali wa safari wa kilomita 194 hivyo itatembea umbali mfupi kuliko ule ambao ingepita ikiwa ingeamua kuweka kambi Arusha.

Simba imesafiri kwa kilomita 378 kutoka Tabora hadi Dodoma na baada ya hapo itasafiri kwa kilomita 636, kutoka Tabora hadi Babati ambako mechi hiyo itachezwa.

Ukiondoa hilo, Simba pia imeamua kubaki Dodoma kwa vile uchunguzi wao umebaini kuwa hakuna kiwanja cha mazoezi chenye ubora hivyo wanahofia kuwa wanaweza kuathiri maandalizi ya mechi iliyo mbele yao.

Kwa kwenda siku moja kabla, Simba itapata fursa ya kufanya mazoezi katika kiwanja ambacho mechi hiyo itachezwa.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alikiri kuwa wataweka kituo kwa muda Dodoma huku akieleze maendeleo ya afya ya Kibu Denis aiyeumia dhidi ya Tabora United juzi.

“Ni kweli tunaelekea Dodoma na hali sio mbaya kwa wachezaji baada ya mechi. Kibu Denis yeye ndio pekee ambaye yupo kwenye uangalizi,” alisema Rweyemamu.

Related Posts