Simon Msuva ataja siri ya ubora wake

WINGA wa Tanzania, Simon Msuva anayekipiga katika klabu ya Al Talaba ya Iraq amesema uzoefu alioupata kucheza ligi mbalimbali Afrika unamfanya kuwa bora kila siku.

Ukiachana na kucheza Yanga, Al Talaba inakuwa timu ya sita kwa Msuva kuichezea nje ya Tanzania baada ya kuitumikia Difaa El Jadida ya Morocco aliyojiunga nayo Julai 2017, kisha Wydad AC (Morocco), Al-Qadsiah (Saudi Arabia), JS Kabylie (Algeria) na Al Najma ya Bahrain.

Akizungumza na Nje ya Bongo, Msuva alisema kinachomfanya awe bora na kukilinda kiwango chake hadi sasa ni uzoefu wa kimataifa.

“Nashukuru Mungu kila ninapopita basi napata uzoefu kwenye klabu mbalimbali na hicho ndio kinanifanya hadi leo kuisaidia timu na taifa langu,” alisema Msuva na kuongeza:

“Nakutana na Ligi tofauti na wachezaji tofauti, kuna muda nakutana na wachezaji niliocheza nao sehemu mbalimbali na kila ligi ina uzito wake. Hilo linachangia ubora, natamani kuendelea kupambana kwa ajili yangu na taifa langu.”

Ikiwa zimechezwa mechi 17 za Ligi ya Iraq chama la Msuva liko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi na pointi 33 ikitofautiana pointi mbili na kinara Al Zawraa zenye 35.

Related Posts