Trump aigeukia Afrika Kusini, kuinyima misaada

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema bila kutaja ushahidi, kwamba “tabaka fulani za watu” nchini Afrika Kusini walikuwa wakitendewa ‘vibaya sana’ na kwamba atakata ufadhili wa nchi hiyo hadi suala hilo litakapochunguzwa.

Trump amebainisha hilo jana, Februari 2, 2025 katika mtandao wake wa Truth akisema kuwa baadhi ya wananchi amekuwa wakifanyiwa ukatili.

“Afrika Kusini inanyakua ardhi, na inawatendea watu wa tabaka fulani vibaya sana,” amesema Trump na kuongeza;

“Marekani haitasimama kwa hilo, tutachukua hatua. Pia, nitakata ufadhili wote ujao kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili wa hali hii utakapokamilika!” amesema.

Haijulikani ni nini kilisababisha hadi Trump kuchapisha ujumbe huo na hata ulipotafutwa Ubalozi wa Afrika Kusini mjini Washington DC haukujibu chochote kuhusu hilo.

Kwa mujibu wa data ya hivi karibuni, Marekani imetoa misaada ya zaidi Dola milioni 440 Afrika Kusini kwa mwaka 2023.

Mapema Januari, mwaka huu, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa alisema hana wasiwasi kuhusu uhusiano wa nchi hiyo na Trump. Alisema alizungumza na Trump baada ya ushindi wa uchaguzi na anatazamia kufanya kazi na serikali yake.

Wakati wa utawala wake wa kwanza, Trump alisema Marekani itachunguza mauaji makubwa ambayo hayajathibitishwa ya wakulima wazungu nchini Afrika Kusini na unyakuzi wa ardhi kwa nguvu.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts