Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, wanatarajiwa kukutana Jumamosi, Februari 8, 2025, jijini Dar es Salaam kujadili mgogoro unaoendelea DRC.
Akitoa taarifa hiyo leo Jumatatu, Februari 3, 2025, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Rais wa Kenya, William Ruto, amesema mkutano huo utahusisha marais wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) na EAC.
“Rais Samia Suluhu Hassan amekubali kwa ukarimu kuandaa mkutano huo kujadili hali ya Mashariki mwa DRC,” amesema Rais Ruto.
Ruto ameongeza kuwa Rais Tshisekedi wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda ni miongoni mwa waliothibitisha kuhudhuria mkutano huo utakaotanguliwa na mkutano wa mawaziri Ijumaa, Februari 7, 2025.
Pia, amesema wengine waliothibitisha kushiriki ni pamoja na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Mkutano huo wa dharura unafanyika wakati DRC ikiishutumu Rwanda kuhusika na mgogoro unaoendelea nchini humo ukiongozwa na waasi wa M23, huku Rwanda nayo ikiishutumu DRC kutaka kuipindua Serikali yake.
Hali ya usalama ilianza kuyumba DRC baada ya kundi la waasi wa M23 kuanza uvamizi na kuyashikilia maeneo ya mashariki mwa DRC ikiwemo Mji wa Goma.
Kwa mujibu wa Rais Mnangagwa, suala la ulinzi wa raia nchini humo si la hiari, bali la kisheria kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa na nchi wanachama wa SADC.
“Ni kwa bahati mbaya nasema kwamba tangu mkutano wetu wa mwisho hali ya amani imetetereka nchini DRC.
“Mashambulizi ya M23 yamegharimu maisha ya wanajeshi wetu wanaolinda amani DRC chini ya SAMIDRC na kuwaacha wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya,” amesema Dk Mnangagwa.