Mwanza. Mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU) Kampasi ya Sengerema utakaoanza Februari 15, 2025, katika Kijiji cha Kalumo, Kata ya Nyamatongo, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh15 bilioni.
Akizungumza leo, Jumatatu, Februari 3, 2025, wakati wa hafla ya kukabidhi eneo kwa mkandarasi Kampuni ya Comfix & Engineering Limited, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa John Lupola, amesema baada ya kukamilika, chuo kitatoa elimu katika fani mbalimbali ikiwemo ukadiriaji majenzi, ubunifu wa majengo, utafiti wa maji, upangaji ardhi, utatuzi wa migogoro ya ardhi, na uzalishaji wa nishati mbadala.
Chuo hicho kinachotarajiwa kukamilika Juni 15, 2026, kitakuwa cha kwanza cha Serikali kujengwa Sengerema, mkoani Mwanza, na kitaongeza udahili wa wanafunzi kutoka 2,300 kwa mwaka hadi kufikia 10,000 ifikapo mwaka 2035.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la ARU, Balozi Salome Sijaona, amewataka wakazi wa Sengerema kutohujumu mradi huo na kutumia fursa hiyo kunufaika kiuchumi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Comfix & Engineering Limited, Hashim Lema, asema mradi huo utahusisha ujenzi wa majengo matano muhimu, ikiwa ni pamoja na madarasa, mabweni, na zahanati.
Wananchi wa kijiji hicho, wakiongozwa na Gaudensia James na Kulwa Msuka, wameeleza furaha yao kwa kuanzishwa kwa mradi huo, wakisema utaboresha uchumi wa eneo hilo na kutoa fursa za elimu kwa watoto wao.
Chuo hicho kinajengwa takriban kilometa sita kutoka Kivuko cha Kamanga na kilometa 20 kutoka katikati ya Jiji la Mwanza.