Dodoma. Bunge la Tanzania limeiagiza Serikali kutumia vyombo vingine ikiwemo Jeshi la Polisi, kudhibiti utapeli na uharifu wa kimtandao, jambo ambalo limetajwa bado ni janga kubwa linalohitaji hatua madhubuti ili kulidhibiti.
Mbali na hilo, kamati hiyo imetaja mzigo mkubwa wa madeni kwenye mashirika ikiwemo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) inayoidai Serikali Sh64 bilioni, Shirika la Posta na madeni mengine kwa makandarasi na wazabuni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Selemani Kakoso amebainisha hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Februari 3, 2025 wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025.
Kakoso amesema suala la utapeli na uhalifu mwingine wa kimtandao, limeendelea kuwepo nchini akisema jambo hilo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kina kwani linatokana na maendeleo ya Tehama hivyo linaathiri uchumi, jamii, ustawi na maadili.
Kutokana na hilo, Bunge limeazimia mambo matano ikiwemo kuhakikisha TCRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inaweka mikakati madhubuti inayozihusisha kampuni za simu kukabiliana na uhalifu wa kimtandao.”
“Iimarishe udhibiti wa uhuru wa mitandao kwa kuzingatia umuhimu wa demokrasia yenye mipaka. Serikali ihakikishe Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi ya eGA (Mamlaka ya Serikali Mtandao) wanashirikiana kwa pamoja kutatua matatizo ya Tehama nchini,” amesema Kakosa.
Maazimio mengine ni Serikali kuwekeza katika kukuza teknolojia ya Tehama kwa vijana na kuifundisha kwa lugha ya Kiswahili na Serikali ihakikishe kampuni za simu zinawajibika ipasavyo kutoa nafuu za kisheria kwa waathirika wa uhalifu wa kimtandao.
Bunge limefikia hatua hiyo kipindi ambacho yamekuwapo matukio kadhaa ya uhalifu mtandaoni ambayo yameripotiwa. Takwimu zinaonyesha matukio ya utapeli yamekuwa yakiongezeka huku hatua zikiendelea kuchukuliwa kuudhibiti.
Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mwaka 2023 inaonyesha matukio ya uhalifu mtandaoni yaliongezeka, huku zaidi ya Sh5.06 bilioni zikitapeliwa kutoka kwa wananchi kupitia mitandao ya simu ikihusisha kuhamisha fedha kutoka benki au kutoa fedha taslimu.
Suala la utapeli mitandaoni limekuwa likizungumzwa ndani na nje Bunge. Novemba 22, 2024 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanaendelea kutapeliwa na watu wachache ambao wamedhamiria kujinufaisha kupitia teknolojia.
“Kama kuna mtu yeyote anafikiria anaweza kutumia teknolojia kufanya ujanja wa kutapeli na kujipatia kipato kwa gharama ya nguvu za watu wengine, wakati huo umekwisha,” alisema Masauni ambaye sasa ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Kwa nyakati tofauti, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alizungumzia suala hilo bungeni, ikiwemo kutangaza kiama kwa matapeli hao akisema watashughulikiwa ili Watanzania wabaki salama.
Nape alisema hapo mwanzo usajili wa laini za simu ulikuwa holela hivyo ilikuwa ni rahisi uhalifu kufanyika, lakini Serikali ikaamua kubadili utaratibu wa usajili wa alama za vidole ambao ulikuwa mkakati wa kuzuia uhalifu huo kufanyika.
“Tulichofanya tumezisajili laini zile kwa kutumia alama za vidole na penyewe ukawa na utapeli na ndio maana juzi tukafanya uhakiki, baada ya uhakiki tunaamini laini zote zilizoko mtaani zina mwenyewe na baada ya hapa nataka nitangaze kiama cha matapeli kwenye mitandao,” alisema.
Nape ambaye ni Mbunge wa Matama alisema kazi ya kuwakamata wahalifu ni ya Jeshi la Polisi na TCRA iwezeshe Polisi kupata taarifa za wahalifu. Hata hivyo, alisema kazi ya kufungia laini za simu zilizofanya uhalifu ni ya TCRA kwa kushirikiana na watoa huduma.
Alisema Septemba 2023 kulikuwa na laini za uhalifu 23,328 lakini Desemba 2023 laini hizo za uhalifu zilifikia 21,000, Machi 2024, laini za uhalifu zilikuwa 17,318.
Kutokana na maazimio hayo ya Bunge, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jelly Silaa ameahidi kuwa Serikali imechukua maoni yote ya wabunge na wanakwenda kuzungumza na TCRA ili kuongeza nguvu katika kupambana na uhalifu wa mtandaoni.
Akichangia kwenye hoja hiyo, Mbunge wa Kyela (CCM), Ally Mlaghila amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha mapambano ya kukomesha utapeli, yanapewa kipaumbele kwani ni tatizo kubwa hivi sasa nchini.
Kuhusu changamoto ya uwepo wa madeni ya ATCL, Kamati imetaja Sh64 bilioni ambazo zinatokana na madai kwa taasisi nyingine za Serikali.
Amesema madeni ya nyuma yaliyolimbikizwa kabla ya ufufuaji wa ATCL, yanayathiri mizania ya vitabu vya hesabu za kampuni, kutopatikana kwa baadhi ya vipuri kama vile injini za ndege, uhaba wa marubani viongozi na wahandisi na kutopata kibali cha kusafirisha mizigo nje ya nchi kwa wakati, na kwamba yote hayo yamesababisha athari kubwa.
“Serikali iharakishe kufuta deni la TGFA (Wakala wa Ndege za Serikali) la Sh429 bilioni, isimamie taasisi nyingine za Serikali kulipa Sh64 bilioni kwa ATCL na kulipa madeni ya wazabuni Sh18 bilioni ili kuondoa changamoto ya madeni ya nyuma yanayolikabili shirika,” amesema.
Madeni mengine ni kwa upande wa makandarasi ambayo yanatokana na kukosekana kwa fedha za kuwalipa makandarasi, wazabuni, madeni ya fidia kwa wananchi yanayotokana na kutwaliwa kwa ardhi katika kupisha miradi.
“Bunge linaazimia, Serikali ilipe madeni ya makandarasi na wazabuni kwa wakati ili kuondoa ongezeko la gharama zinazosababishwa na riba lakini ilipe fidia kwa wananchi, tathimini za mali na ardhi kwa ajili ya kupisha ujenzi,” amesema.
Agizo lingine kutoka kwenye kamati hiyo ni kuitaka Serikali iongeze kasi ya kutekeleza ujenzi wa minara ya mawasiliano, hasa maeneo yaliyoanishwa kuwa na mahitaji maalum kama vile katika barabara kuu, mbuga za wanyama, mipakani na mapori tengefu ili kukuza shughuli za utalii na kuboresha usalama.
Nalo Shirika la Posta Tanzania limebainika kuwa na mzigo wa madeni unaofikia Sh54.7 bilioni lakini wakiwa na mtaji mdogo wa kuweza kujiendesha hivyo wanashindwa kukopesheka.
Kamati imependekeza Serikali ibebe deni inalodaiwa Shirika la Postaili kusafisha mizania ya shirika na kuliwezesha.
Wajumbe wa kamati pia wamezungumzia katikakatika ya umeme nchini kwamba licha ya uwepo wa umeme wa ziada, lakini suala la kukatika limekuwa ni kero wakisema linatokana na ubovu wa miundombinu, uchache wa mashine umba na vituo vya kupoza umeme, jambo linalochangia kukosa nguvu ya umeme kwenye kwenye baadhi ya maeneo.
“Hali hiyo inaathiri shughuli za kiuchumi na kijamii na hivyo kuzua malalamiko miongoni mwa wananchi. Serikali itatue changamoto hizo kwa kuanza na utekelezaji wa miradi ya gridi imara ya muda mfupi itakayotatua changamoto ya kukatika umeme na kukosa nguvu katika eneo kubwa.
Kamati ya Nishati na Madini
Mwenyekiti wa kamati ya Nishati na Madini, Dk Mathayo David amesisitiza Shirika la Madini (Stamico) kuwezeshwa kimtaji ili liongeze uzalishaji kwani mradi wa makaa ya mawe Kiwira – Kabulo umeanza kuleta manufaa kiuchumi kwa kuzalisha faida baada ya kupitia katika kipindi kigumu.
Dk Mathayo ameitaka Serikali iendelee kuiwezesha Stamico kimtaji na kiteknolojia sambamba na kutatua changamoto zilizopo ili mradi wa Kiwira – Kabulo na miradi mingine, iongeze uzalishaji na hivyo kuongeza mapato ya shirika na Serikali.
Kamati imezungumzia pia matatizo ya wachimbaji wachimbaji wadogo wa madini nchini, kwamba bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji inayowawezesha kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Taarifa ya kamati hiyo imetaja hali hiyo imewalazimu kutegemea mitaji kutoka nje ya nchi ambayo inaweka masharti magumu ikiwamo kuwauzia madini wawekezaji wa nje, jambo linalosababisha viwanda vya kusafisha dhahabu vya ndani kukosa malighafi.
“Bunge linaazimia kwamba, Serikali iweke mikakati ambayo itawawezesha wachimbaji wadogo wa ndani kupata mitaji kutoka taasisi za fedha za ndani, ili wawe huru kuuza dhahabu wanayozalisha kwa viwanda vya ndani, na kunufaika na unafuu wa kodi na tozo zilizopo,” amesema Dk Mathayo.
Kamati hiyo pia imetaja jitihada za kutatua changamoto ya umeme wa gridi ya taifa kukatika mara kwa mara.
Dk Mathayo alisoma azimio la kuitaka Serikali ikamilishe malipo ya makandarasi na wananchi wote wanaodai mapema na kwa ukamilifu ili kuzuia ongezeko la riba ya ucheleweshaji wa malipo; na itekeleze na kumaliza ujenzi wa miradi 22 ya gridi imara iliyobakia katika awamu ya kwanza kabla ya Aprili, 2026.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angelina Mabula amesisitiza Serikali kusimamia miradi ya wachimbaji wadogo, ikiwemo kuongeza mitambo ya kufanyia kazi kutoka mitano iliyopo ambayo kwa sasa inaonekana kama inatolewa kwa upendeleo.