Vyama vya siasa vyaonywa kampeni za mapema

Dar es Salaam. Vyama vya siasa nchini vimetahadharishwa kuepuka kuvunja sheria za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kunadi wagombea kabla ya muda wa kampeni.

Hivi karibuni, baadhi ya vyama vya siasa vimeonekana kunadi wagombea wake kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 2025, jambo ambalo Baraza la Vyama vya Siasa limekosoa, likieleza kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu,  Februari 3, 2025, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ally Khatibu, amesema si vibaya kwa wagombea wa nafasi mbalimbali kutangaza nia wakati huu, lakini akibainisha kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria kuanza kuwanadi wagombea.

“Nimeona baadhi ya vyama vinawanadi wagombea wao hivi sasa wakati INEC na ZEC hazijatangaza muda wa kampeni. Vyama vya siasa ni vema kuwa waangalifu ili visivunje sheria za Tume,” amesema Khatibu.

Amesema kuwanadi wagombea kabla ya pazia la kampeni kutangazwa ni kosa kisheria na lina adhabu zake.

 “Sheria inasema baada ya kuvunjwa kwa Bunge na Baraza la Wawakilishi ndipo tume itatangaza muda wa kampeni, huu si wakati wake,” amesema.

Amesema baada ya INEC na ZEC kutangaza muda wa kampeni, ndipo kila chama kitaanza kuwanadi wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani na kwamba kinyume na hapo ni kuvunja sheria.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, baadhi ya vyama kuanza kuwanadi wagombea hivi sasa, ni kupoka uamuzi wa kufanya kazi wa tume kwa mujibu wa Katiba.

“Vipo vyama vimeshawanadi wagombea, basi tuheshimu kuwa hao ndio wagombea wao, lakini nivikumbushe visubiri muda wa kampeni ufike na si hivi sasa. Kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

“Kisheria, tume itatangaza tarehe ya kuanza kwa mikutano ya kampeni kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, tusivunje sheria zetu ambazo zipo kwa mujibu wa Katiba na adhabu zake zipo,” amesema.

Related Posts