Rukwa. Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linawashikilia watu wanne wa familia moja, kwa tuhuma za kumuua kwa kumchinja shingoni na panga ndugu yao, anayejulika kwa jina la Mashaka Michael Sichone (30) mkazi wa Wilaya ya Kalambo na kisha kuondoka na kichwa chake.
Marehemu huyo alikuwa ni Katibu wa CCM tawi la Migomba Kijiji Kalipula, Kata ya Ulumi Tarafa ya Mwimbi Wilaya ya Kalambo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3, 2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoani Rukwa, ACP Shadrack Masija amesema tukio hilo la kikatili lilitokea usiku wa Januari 27 mwaka huu nyumbani kwa marehemu.
Amedai kuwa mauaji hayo yamefanywa baada ya ndugu wa marehemu huyo, kudai kuwa ndugu yao ndiye aliyemuua baba yao mzazi kwa kutumia uchawi.
“Chanzo cha mauaji haya ni imani za kishirikina, kwamba hawa watu tunaowashikilia waliamini kwamba huyo Mashaka ambaye ni ndugu yao, alimuua baba yao kwa kumroga, kwa hiyo walipanga nao wamuue ikiwa ndio njia ya kulipiza kisasi,” amesema.
Baada ya kutekeleza mauaji hayo, RPC Masija amedai kuwa walikimbia kwenda kujificha maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa jitihada tulizofanya polisi, hatimaye wote wanne tumewakamata na wameonyesha katika mahojiano walipotupa kile kichwa, tumekitafuta na hatimayte tumekipata,” amesema.
Kamanda amewataka wananchi kujiepusha na imani za kishirikina, kwani si kila anayekufa amerogwa.
“Hata maandiko yanatuambia, kila aliyezaliwa na mwanamke, ataonja mauti, kwa hiyo tuwahimiza wananchi, endapo kuna mgonjwa tumpeleke hospitali akapate tiba, la Mungu akiamua, ndio itakuwa njia yake ya kuondoka duniani,” amesema.
Amewataka pia wananchi kuwa tayari kutoa taarifa kwa polisi zitakazowezesha kufanikisha ukamataji na upelelezi wa kina.
Akielezea tukio hilo, Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Kalipula wilayani Kalambo, Agatha Pius amesema alifika kwenye eneo la tukio baada ya kupata taarifa.
“Nilipofika eneo hilo nikakutana na mke wa marehemu, akanieleza kwa ufupi kuwa, aliamka asubuhi hakumkuta mumewe na alipofuatulia kwa muda akaona mume wake harudi, ndipo ikabidi atoe taarifa kwa wakwe zake,” amesema.
Amesema wakwe zake nao walianza kumtafuta mtoto wao na ndipo walipoupata mwili wake ukiwa hauna kichwa.
“Marehemu alikutwa amefariki kwa kukatwa na kichwa kikiwa hakipo, utararatibu wa kutafuta kichwa ukaanza, lakini hakikupatikana. Ndipo nilipotia taarifa Polisi kituo cha Mwimbi ndio wakafika kwenye tukio,” amesema.
Devotha Makambi anayeishi kijijini hapo, amesema kuwa Mashaka alikuwa mtu mzuri asiye na mambo mengi.
“Tuliishi naye vizuri tu alikuwa mtu wa watu mwenye upendo, lakini imani za kishirikiana zimeondoa uhai wake,” amesema.