MSHAMBULIAJI wa Simba, Leonel Ateba Mbida anaendelea kuonyesha kiwango bora hadi sasa katika michezo ya Ligi Kuu Bara na timu hiyo, huku akiwa kwenye mazingira mazuri ya kuandika rekodi mpya ya kumaliza msimu kwa kufunga zaidi ya mabao 10.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba Agosti 15, mwaka jana akitokea USM Alger ya Algeria, tayari amecheza michezo 12 kati ya 16, ya timu hiyo msimu huu ambapo ametumika dakika 811 na kufunga mabao saba sawa na nyota mwenzake, Jean Charles Ahoua.
Lakini kwa kasi anayokwenda nayo kitakwimu, kuna jinsi anaweza kupindua rekodi za wenzie katika miaka ya hivikaribuni na kisha kuisaka rekodi iliyowekwa na mastaa wengine ndani ya miaka 10 Msimbazi.
Kitendo cha kufunga mabao saba, kinamuweka katika nafasi nzuri ya kufikisha mabao 10 na kuendelea na kuifukuzia rekodi hiyo katika Ligi Kuu Bara, kwa sababu tangu msimu wa 2021-2022, hakuna mshambuliaji wa Simba aliyefunga zaidi ya hayo.
Msimu wa 2021-2022, nyota wa Simba aliyemaliza na mabao mengi ni Kibu Denis aliyecheza michezo 22, ambapo alifunga mabao manane na kuchangia manne ‘Assisti’, huku kinara alikuwa ni nyota wa zamani wa Geita Gold, George Mpole aliyefunga 17.
Msimu uliofuatia wa 2022-2023, mshambuliaji pekee aliyemaliza na mabao mengi alikuwa ni John Bocco ambaye kwa sasa yupo JKT Tanzania aliyefunga 10, huku aliyekuwa kiungo wake, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, akimaliza kinara na mabao yake 17.
‘Saido’ raia wa Burundi aliibuka mfungaji bora baada ya kuzichezea timu mbili, akianzia na Geita Gold kisha dirisha dogo la Desemba 2022 kutua Simba, huku akiwa idadi sawa na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Fiston Mayele.
Msimu uliofuata, Saido akaendeleza kiwango bora ndani ya kikosi hicho akimaliza kinara wa mabao Simba baada ya kufunga 11, huku mshambuliaji pekee aliyemfuatia alikuwa ni Mkongomani Jean Baleke, aliyekifungia kikosi hicho mabao manane tu.
Stephane Aziz KI wa Yanga ndiye aliyeibuka kinara wa ufungaji bora msimu huo, baada ya kufunga mabao 21, akifuatiwa kwa ukaribu na kiungo mshambuliaji nyota wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga 19.
Kwa msimu huu wa 2024-2025, tayari Ateba ameonyesha anaweza kuzivuka rekodi za watangulizi wake ndani ya timu hiyo jambo linaloongeza matumaini makubwa kwa Kocha, Fadlu Davids kwenye mbio za ubingwa ambao Simba imeukosa kwa misimu mitatu.
Ateba hakutua tu Simba kwa bahati mbaya bali ilipitia mchakato mkubwa baada ya awali kudaiwa skauti wa timu hiyo, Mels Daalder kumpendekeza Mzambia Ricky Banda, lakini ikashindikana kumpata ndipo hesabu zikahamia kwa Muethiopia Abubeker Nassir aliyekuwa anaichezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa wakati huo.
Abubeker ambaye kwa sasa anaichezea SuperSport United ya Afrika Kusini pia, uongozi wa Simba uliona ingekuwa rahisi kwao kumpata kutokana na kutopata nafasi ya kucheza wakati huo akiwa Mamelodi, ila majeraha ya mara kwa mara wakaachana naye.
Uchambuzi ukaendelea hadi kwa Mrundi Elvis Kamsoba aliyekuwa mchezaji huru wakati huo baada ya kuachana na Perserikatan Sepakbola Sleman ya Indonesia huku akiwahi kuzichezea timu mbalimbali za Melbourne Victory FC na Sydney FC za Australia.
Uzoefu wa mchezaji huyo ukawavutia mabosi wa Simba ila mwishoni wakaachana naye baada ya kujiridhisha hana fitinesi ya kutosha na atakapotua nchini itabidi apewe programu maalamu ya wiki moja hadi mbili, jambo ambalo hawakukubaliana nalo.
Baada ya machaguo hayo kugonga mwamba, ndipo Simba ikafikia makubaliano na USM Alger ya kumpata Ateba ambaye haikuwa rahisi pia, japo kitendo cha yeye mwenyewe kuomba kuondoka ili akatafute changamoto sehemu nyingine kilirahisisha dili.
Kitendo cha Simba kumtaka Ateba, kikachochea kuomba kuondoka hususani baada ya kutopenda kuchezeshwa namba 10, nyuma ya aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Mali Abdoulaye Kanu, hivyo kurahisisha dili la nyota huyo kujiunga Msimbazi.
Ateba alijiunga na USM Alger Januari 2024 akitokea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon ambapo msimu uliopita nyota huyo alihusika katika mabao tisa akiwa na kikosi hicho, baada ya kufunga moja tu na kuasisti manane kwenye michezo 16.
Nyota huyo aliyezichezea timu za Coton Sport na PWD Bamenda, anakumbukwa zaidi mwaka 2023, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi ya Cameroon baada ya kufunga mabao 21, yaliyomfanya kuitwa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kocha wa Simba, Fadlu Davids anasema siri kubwa ya kiwango kinachoonyeshwa na nyota huyo ni kutokana na ushirikiano na wenzake.
“Kila mmoja katika nafasi yake anafanya vizuri hivyo siwezi kuelezea mchezaji mmoja mmoja zaidi ya kuwapongeza wote kwa kile wanachokifanya, wachezaji wanategemeana ndio maana jambo la umuhimu ni kudumisha ushirikiano baina yao uwanjani.”