Athari za kiafya maduka ya chini ya ghorofa Kariakoo

Dar es Salaam. Maduka ya chini ya majengo ya ghorofa (underground) yanayozunguka Soko la Kariakoo yanaweza kuleta changamoto mbalimbali za kiafya na kiusalama kwa wauzaji na wateja.

Mwananchi imefanya uchunguzi kwenye majengo ya biashara ya ghorofa yanayozunguka eneo la Soko la Kariakoo, baada ya kuanguka jengo la ghorofa kutokana  mmiliki wake kudaiwa kuongeza kuchimba eneo la chini ili kupata nafasi ya kibiashara.

Hata hivyo, Mwananchi imebaini uwepo wa maduka mengi yamechimbwa ya chini ya majengo ya ghorofa.

Maduka haya yameibua hisia tofauti miongoni mwa wafanyabiashara na wateja ikiwamo fursa za kibishara, lakini hoja ya kiafya kwa kuwa maeneo hayo hayana mifumo bora ya hewa wala mwanga wa kutosha.

Mtaalamu wa magonjwa ya upumuaji, Dk Elisha Osati, alipoulizwa kuhusu hali ya kiafya kwenye maduka ya chini ya majengo ya Kariakoo, amesema hatari iliyopo hewa inaweza kuwa nzito na kusababisha magonjwa mbalimbali ikiwamo athma.

Amesema tatizo la pili ni mwanga halisi, wanaokaa kwenye maduka hayo ya chini, wanaweza kupata tatizo la uoni hafifu kutokana na mwanga kuwa mdogo.

“Mtu anayekaa muda mrefu huko chini anaweza kuja kupata matatizo ya uoni hafifu kwa kuwa kibinadamu anapaswa kupata mwanga wa asili,” amesema Dk Osati.

Licha ya maelezo ya kitaalamu ya Dk Osati, mmoja wa wafanyabiashara kwenye duka lililopo chini ya jengo hapo Kariakoo, amesema kutoka na joto analazimika kutumia feni zaidi ya moja kwa wakati wote anaokuwepo humo.

“Mfano hapa kwangu nimefunga feni sita ilimradi kila kifaa kilichopo kiweze kupata upepo huo, kwani pia huwa kuna tv na redio tunaziwasha kwa ajili ya kuvutia wateja, hivyo zikipata moto zinapoozwa na feni,” alisema mfanyabiashara huyo Isman Kajura.

Mwananchi imebaini maduka hayo yanakabiliwa na ukosefu wa mifumo bora ya hewa.

Kutokana na kuwa chini ya majengo, maduka hayo hayana madirisha wala njia za asili za kupitisha hewa safi, jambo ambalo linafanya wauzaji na wateja kutegemea feni kwa muda wote ili kupunguza hali ya hewa nzito.

Hata hivyo, Dk Osati ameielezea hali hiyo inaleta athari za kiafya hasa kwa upande wa upumuaji, kwa kuwa ukosefu wa mzunguko wa hewa safi unaweza kusababisha matatizo ya kupumua na kuongeza uwezekano wa magonjwa ya mfumo wa hewa kama vile pumu na mzio.

“Kwa hiyo wakati mwingine mtu anaweza kupoteza umakini au saa zingine vichwa vinauma, kupata mafua, yote haya yanaweza kuwa madhara kwa namna moja,” ameeleza daktari huyo ambaye amewahi kuwa Rais wa Chama cha Madaktari nchini.

Ushauri wake kwa wajenzi wa majengo hayo ni kuhakikisha wanayabuni kuwezesha kupitisha hewa halisi na mwanga, kwa kuwa vyote hivyo vina umuhimu katika afya ya binadamu.

Mfanyabiashara Mage Kyara, akizungumzia kuhusu hewa nzito amesema huwalazimu mara kwa mara kutoka nje ili kupata hewa safi.

“Huwa najikuta natoka nje kupumua hewa safi, hasa nikiwa na mtu wa kunisaidia kuangalia bidhaa zangu zisije zikaibwa,” amesema.

Kwa upande wake, Mrisho Karim, mfanyakazi wa duka la urembo, amesema hali ni mbaya zaidi kwao kwa kuwa,  bidhaa anazouza zinahitaji mwanga mkali wa taa.

“Bosi wangu amelazimika kufunga taa nyingi kubwa ili kuwezesha biashara, lakini nazo zinazidisha hali ya hewa kuwa nzito na joto kuwa kali. Tunaumia, lakini hatuna jinsi kwa sababu kazi lazima ifanyike,” amesema.

Naye Shamsa Kim, anayeuza nguo za jumla na rejareja, amesema mara nyingi hukaa nje ya duka lake na huingia tu mteja anapofika.

“Mbali na hewa nzito, hata nguo zenyewe huathiriwa na vumbi ambalo huwezi kuliona kwa macho, jambo linalochangia hali hii kuwa mbaya zaidi,” alisema.

Iqram Kitivo ameeleza kuwa upepo pekee wanaoutegemea ni ule wa feni, lakini wakati wa jua kali, mashine hizo hazisaidii.

“Nimefunga feni nne, lakini jua likiwa kali ni kama hazifanyi kazi. Nadhani kuna haja ya wahusika wa majengo haya kutafuta namna bora ya kuhakikisha hewa inazunguka vizuri ili nasi tujisikie kama waliopo ghorofani badala ya kuhisi tupo shimoni,” amesema.

Mfanyabiashara wa maduka hayo, Mwamvita Amir ameeza ugumu wa kuweka viyoyozi kwamba itawalazimu pia kuweka milango, hali itakayofanya wateja wasione bidhaa zao kwa urahisi.

 “Yaani ukiona mtu hapa Kariakoo hasa ‘underground’ kaweka na milango, jua huyo biashara yake anategenmea zaidi wateja wa mtandaoni, na hapa ni kama ofisi tu, lakini wakina siye tunaotegemea hawa wanapita hapa ni lazima kuwe wazi ili waone unachokiuza,” alisema Amir.

Rajabu Kazimoto amesema mamlaka husika zinapaswa kusimamia na kudhibiti ujenzi wa aina hii ili kuhakikisha usalama wa wananchi.

Pia, amesema maduka hayo ya Kariakoo yaliyo chini yanatakiwa kuwekwa mifumo ya kupooza hewa ili kudhibiti joto na unyevunyevu, na hivyo kuboresha faraja ya wafanyabiashara na wateja.

Naye Rehema George ambaye ni mfanyabiashara wa Kariakoo amesema kuna umuhimu kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuboresha mazingira yao ya kazi kwa kutumia vifaa vinavyosaidia kupunguza athari za kiafya, kama vile feni za kisasa zinazosaidia kuboresha mzunguko wa hewa bila kuongeza joto.

Pia, ameiomba Serikali kupitia mamlaka zake kuhakikisha kuwa ujenzi wa maduka haya unazingatia sheria na kanuni za ujenzi wa maeneo ya biashara ili kuepuka matatizo yanayoweza kuepukika.

“Wamiliki wa majengo wanapaswa kufunga mifumo bora ya uingizaji na utoaji wa hewa safi ili kuboresha mazingira ya kazi na kupunguza athari za kiafya kwa wauzaji na wateja.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa maduka haya yanakuwa na njia mbadala za dharura ili kuepusha maafa endapo kutatokea dharura kama vile moto au mafuriko,” alisema.

Related Posts