Bei za petroli, dizeli zapaaa Februari

Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto watatakiwa kuongeza bajeti za ununuzi wa mafuta kwa ajili ya vyombo vyao baada ya bei kikomo za mafuta kuongezeka.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo Februari 5, 2025, bei ya petroli kwa rejareja katika Jiji la Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 0.957, dizeli kwa asilimia 2.18 na mafuta ya taa kwa asilimia 1.25.

Bei hizo zinaongezeka wakati ambao gharama za uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi zikipungua kwa wastani wa asilimia 4.9 kwa petroli, asilimia 14.94 kwa dizeli na wastani wa asilimia 0.81 kwa mafuta ya taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Japo hakuna mabadiliko ya gharama za uagizaji mafuta katika bBandari ya Tanga, kwa Mtwara zimepungua kwa wastani wa asilimia 6.34 kwa mafuta ya petroli na dizeli.

Hii ikiwa na maana kuwa sasa wanunuzi wa mafuta kwa bei ya rejareja katika Jiji la Dar es Salaam watanunua lita moja kwa Sh2, 820 kwa petroli, dezeli Sh2, 703 na mafuta ya taa kwa Sh2, 710.

Bei hizo ni kutoka Sh2, 793 kwa bei ya petroli ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa Januari mwaka huu, dizeli Sh2, 644 na mafuta ya taa kwa Sh2, 676.

Kwa wakazi wa Tanga sasa watanunua petroli rejareja kwa Sh2, 825, dizeli kwa Sh2, 746 na mafuta ya taa kwa Sh2, 756.

Bei ya Januari ilikuwa Sh2, 800 kwa lita moja ya petroli, dizeli Sh2, 656 na mafuta ya taa kwa Sh2, 722.

Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.88 kwa petroli, dizeli asilimia 3.27 na mafuta ya taa asilimia 1.23.

Kwa watumiaji wa mafuta yanayopitia Bandari ya Mtwara na viunga vyake watanunua petroli kwa Sh2, 892, dizeli kwa Sh2, 775 na mafuta ya taa kwa Sh2, 782.

Kwa Januari lita moja ya petroli iliuzwa kwa Sh2, 866, dezeli Sh2716 na mafuta ya taa kwa Sh2, 748.

Taarifa hiyo ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi wake mkuu, Dk James Mwainyekule imezitaka kampuni za mafuta kuuza bidhaa hio kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura.

Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

 “Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imesema Ewura.

Taarifa hiyo imesema wauzaji wanakitakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wakitakiwa kuchukua stakabadhi hizo.

Stakabadhi hizo zinatakiwa kuonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

“Stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa.

“Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli,” imeeleza taarifa hiyo.

Related Posts