Bunge laazimia vituo vya kura karibu na makazi

Dodoma. Bunge limeazimia vituo vya kuandikisha wapigakura na vile vya kupiga kura viwekwe karibu na makazi ya wananchi ili washiriki na kutekeleza haki yao ya kikatiba.

Mbali na hilo, pia limeazimia Serikali ihakikishe inapeleka watumishi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura wasimamia kazi hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuwasilisha mapendekezo hayo ilipowasilisha taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa shughuli zake kwa kipindi cha kati ya Februari, 2024 hadi Februari 2025.

Baada ya mapendekezo hayo, Naibu Spika, Mussa Zungu aliwahoji wabunge ambao waliyapitisha kwa wingi wa sauti. “Ndiyoooo.”

Awali, akiwasilisha taarifa hiyo leo Jumatano Februari 5, 2025, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Joseph Mhagama amesema wamebaini uwepo wa changamoto ya umbali wa vituo vya kujiandikishia wapigakura na vya kupiga kura kwa maeneo ya vijijini pamoja na uchache wa watumishi wa kusimamia kazi ya uandikishaji.

Amesema changamoto hiyo inasababisha wananchi wengi kushindwa kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura, hivyo kukosa kushiriki katika kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi.

“Kwa hiyo, Bunge liazimie kwamba, vituo vya kuandikisha wapigakura na vituo vya kupiga kura viwekwe karibu na makazi ya wananchi ili waweze kushiriki na kutekeleza haki yao ya kikatiba. Serikali ihakikishe inapeleka watumishi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kusimamia zoezi hilo,” amesema Dk Mhagama.

Akizungumza na Mwananchi nje ya ukumbi wa Bunge, Dk Mhagama amesema maeneo ya vijijini wapo baadhi ya watu hutembea kilomita tatu hadi tano kufuata kituo cha kujiandikishia kupiga kura.

Amesema kwa mazingira hayo, mtu huyo hatatembea umbali huo kwenda kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

“Wapo watu hutembea hadi kilomita tano kwenda kituo cha kujiandikisha kupiga kura, hilo halileti hamasa ya watu kwenda kujiandikisha na kwenda kupiga kura kwa sababu mara nyingi ndiyo vinageuka vituo vya kupigia kura,” amesema Dk Mhagama.

Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amesema wanachohitaji ni kila mmoja afikiwe na kituo cha kupigia kura kwa sababu kila mtu anahitaji kupiga kura.

“Sisi ni tofauti na nchi nyingine kama vile Marekani ambayo ina miaka 200, ina mifumo lakini sisi tunaendelea kujifunza kila baada ya uchaguzi kwa kujua hapa tumepatia hapa tumekosea,” amesema Mwakagenda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, ndogo Jasson Rweikiza akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo leo Februari 5, 2025 Bungeni Jijini Dodoma.

Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka taasisi ya kuwajengea uwezo vijana ya Bridge For Change (BFC), Ocheck Msuva amesema ongezeko la vituo vya uandikishaji wapigakura litaongeza idadi ya watakaojiandikisha kwa mikoa iliyobaki.

“Nafikiri hapa wanagusa jamii nyingi za wafugaji na wakulima ambao vijiji vyao viko mbalimbali. Kwa uzoefu wangu vituo viko kwenye maeneo ya makazi au shule,” amesema Msuva.

Amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), iliongeza idadi ya vituo vya kujiandikishia wapigakura.

Katika hatua nyingine, Bunge limeazimia Serikali ihakikishe inawachukualia hatua za kinidhamu watumishi ambao watabainika kukosa maadili na kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Akisoma pendekezo la kamati, Dk Mhagama amesema kamati imebaini uwepo wa changamoto ya ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa Mahakama nchini.

Amesema changamoto hiyo inasababisha wananchi kutokuwa na imani na Mahakama na vyombo vya utoaji haki nchini.

“Kwa hiyo basi, Bunge liazimie Serikali ihakikishe inawachukualia hatua za kinidhamu watumishi ambao watabainika kuwa na ukosefu wa maadili na kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo,” amesema Dk Mhagama.

Akichangia taarifa hiyo, mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Oscar Kikoyo amesema Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria aliwaasa majaji na mahakimu wasiwe miungu watu.

“Niombe Wizara ya Katiba na Sheria ikazichunguze na kumulika jicho katika Mahakama za Mwanzo katika hatua ya utoaji wa haki,” amesema Kikoyo.

Kikoyo amesema ipo kamati ya maadili ya kuwajibisha mahakimu wa Mahakama za Mwanzo lakini jukumu hilo linaonekana wakuu wa wilaya wengi ama hawalifahamu au hawalifanyii kazi.

Ameiomba wizara husika kuandaa waraka mahususi wakawachunguze mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wote, pale wanapotoa haki ili wananchi waipate kulingana na makosa au kesi wanazozipeleka mahakamani.

Kuhusu utafiti wa sheria, Dk Mhagama amesema kamati imebaini Serikali imekuwa ikileta mapendekezo ya maboresho ya sheria ya mara kwa mara bungeni ili kufanyiwa marekebisho na kutatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa sheria hizo.

Amesema changamoto hiyo huweza kuonekana kama kuna upungufu wa tafiti za kutosha kwenye sheria nchini.

“Serikali iiwezeshe Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kuitengea fungu la maendeleo ili iweze kutekeleza jukumu la kufanya tafiti kwa sheria kabla hazijaletwa bungeni,” amesema Dk Mhagama.

Kamati imeitaka Serikali kuhakikisha inatenga bajeti ya kutosha kwa Tume hiyo ili itekeleze majukumu yake kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Dk Mhagama amesema kamati imebaini uwepo wa masharti ya leseni nyingi zinazotolewa na mamlaka tofauti za Serikali nchini kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Amesema masharti hayo yanaweza kuchukuliwa kama usumbufu, hivyo kupunguza kasi ya wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

“Bunge liazimie kwamba, Serikali iratibu utengenezwaji wa mfumo wa pamoja wa ulipaji kodi (Mifumo ya kodi kusomana) kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini,” amesema Dk Mhagama.

Pia, kamati imependekeza kuwepo mfumo mmoja wa utoaji leseni za biashara kwa wawekezaji wazawa na wa kigeni ambao utaratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Kamati imependekeza Serikali kupitia tovuti ya TIC, ibainishe aina ya leseni zote mwekezaji anazotakiwa kuwa nazo kwenye sekta tofauti za uwekezaji nchini na namna anavyoweza kuzipata.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Mipango na Uwezeshaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema wanakubaliana na mapendekezo ya kamati hiyo ya Bunge na kwamba katika muswada mpya wa sheria ambao wamependekeza kuupeleka bungeni, baadhi ya mambo yatashughulikiwa.

Amesema pamoja na hilo, mapitio ya mpango mpya wa kuboresha mazingira ya biashara yatashughulikia mambo yaliyoazimiwa.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema wamepokea maazimio yote ya Bunge.

Amesema akiwa waziri mwenye thamana na haki, watayatekeleza.

Wakati huohuo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imebaini sheria ndogo iliyotungwa na Halmashauri ya Ludewa mkoani Njombe, imeweka sharti la kuomba kibali cha kusarifisha mazao ya uvuvi ikiwamo samaki kwa matumizi ya nyumbani.

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya kamati hiyo, mwenyekiti wake, Jasson Rweikiza amesema matokeo ya uchambuzi wa kamati yanabainisha masharti yaliyowekwa na sheria ndogo ambayo utekelezaji wake hauna uhalisia ikilinganishwa na lengo la sheria ndogo.

“Dosari hiyo imebainika katika Sheria Ndogo ya Ushuru wa Mazao ya Uvuvi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, 2024 (TS Na. 815 la mwaka 2024),” amesema Rweikiza.

Amesema sheria hiyo imeweka sharti la kuomba kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi kwa ajili ya biashara.

Pia, moja ya kifungu kimetaja wahusika wanaopaswa kuomba kibali cha kusarifisha mazao ya uvuvi ikiwamo samaki kwa matumizi ya nyumbani.

“Kwa mantiki ya masharti hayo, mwananchi yeyote aliye katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambaye atahitaji kupata samaki kwa matumizi ya nyumbani atapaswa kuomba kibali cha kusafirisha samaki hao,” amesema Rweikiza.

Amesema masharti hayo hayana uhalisia katika utekelezaji na yanaweza kutafsirika kuwa ni kero kwa wananchi wanaonunua na kusafirisha mazao hayo kwa matumizi ya nyumbani.

“Bunge linaazimia, mamlaka zinazotunga sheria ndogo zilizobainika kuwa na masharti yasiyozingatia uhalisia, zifanye marekebisho ili kuondoa dosari hizo,” amesema Rweikiza.

Related Posts