Leo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefikisha miaka 48 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, kikiwa miongozi mwa vyama vichache vya ukombozi vilivyopo madarakani barani Afrika, huku kikipigania kuendelea kubaki madarakani.
Februari 5, 1977, vyama vya TANU na Tanganyika na Afro Shiraz (ASP) cha Zanzibar viliungana na kuunda chama kimoja—CCM. Chama hicho ndicho kinaongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Licha ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, CCM kimeendelea kushinda chaguzi na kuongoza Serikali, huku vyama vya upinzani vikilalamikia hila zinazofanyika kila uchaguzi unapofanyika.
Oktoba, mwaka huu, CCM kitashiriki uchaguzi wa saba wa vyama vingi, huku kikitarajiwa kuibuka na ushindi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuwa na ngome kubwa mashinani, hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na wapinzani.
Katika kipindi cha miaka 48 tangu kuanzishwa kwake, CCM kimepitia nyakati tofauti, huku kikijibadilisha kwa kujisahihisha ili kuendana na mahitaji ya wakati na pia kuendelea kubakia madarakani.
Katika makala haya, Mwananchi limefanya mahojiano na wadau mbalimbali wa siasa ambao wanasimulia mapito ya CCM katika kipindi hicho na wanatoa ushauri nini wafanye ili chama kiendelee kulinda maslahi ya wananchi.
Balozi mstaafu, Francis Mndolwa anasema CCM bado ni chama kilichothibitisha duniani kama chama cha kisiasa na kiukombozi na kimepitia matatizo na misukosuko kadhaa tangu kuanzishwa kwake.
“CCM ingekuwa inashughulika na matatizo ya wananchi wake, inawezekana mafanikio yangekuwa makubwa zaidi, lakini CCM, katika kipindi chake cha ujana na uchanga, kimekuwa kikipambana na matatizo ya Afrika Mashariki na nchi za Afrika kwa jumla,” anasema.
Anasema mwendo wa CCM kukua hadi kufikia miaka 48, umekuwa mgumu, lakini uimara wa viongozi wanaokiongoza na ushupavu wao, umekuwa ukikibeba kwa kupata mafanikio pamoja na magumu wanayopitia.
“CCM imekuwa na viongozi wazuri tangu mwanzo hadi sasa, ndiyo maana kumekuwa na mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu yake,” anasema.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anasema pamoja na kwamba inajivunia kuwa madarakani kwa muda wote huo, lakini maisha yake hayajawahi kuwa rahisi.
“Kuna kipindi kulikuwa na panda shuka, kipindi cha pili cha Rais Jakaya Kikwete, watu walikuwa wakivaa sare za chama wanazomewa na walio wengi walikuwa wanashindwa kuvaa,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alilazimika kutumia nguvu kubwa kuzunguka mikoani kukinadi chama na kusaidia shughuli za ujenzi wa chama.
“Chama kilikuwa kinapoteza mvuto, ni kipindi ambacho upinzani ulikuwa umepata nguvu na CCM ilishindwa kuisimamia Serikali vizuri, kulikuwa na tuhuma nyingi za ufisadi hadi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alienda kutaja orodha ya mafisadi viwanja vya Mwembeyanga,” anasema.
Dk Mbunda anasema kuna wakati walipitisha mkakati wa kujivua gamba kuna baadhi ya viongozi wa chama walilazimika kujiuzulu kama sehemu ya kujisafisha na makandokando.
“Maisha ya CCM yanabaki kuwa somo kwao, kuna wakati walifurahia maisha, lakini kuna wakati walikosa uungawaji mkono, kinachowasaidia ni vile chama hakijakomaza shingo, kipindi kinachotakiwa kuwa kikali kinafanya hivyo,” anasema.
Anasema kuna wakati mawaziri walikuwa wanaitwa mizigo, ni kauli za kishujaa ambazo viongozi wa CCM walizichukua ili kukinasua katika anguko madarakani.
“Kuna kipindi CCM, ilituhumiwa kama chama cha watu fulani, viongozi na watoto wao, lakini waliligundua hilo na wakaanza kufungua milango, hasa kipindi cha hayati Rais John Magufuli, kuwaingiza wenye uwezo na kufanikiwa,” anasema.
Kwa upande wake, Waziri wa zamani na mwanasiasa mkongwe nchini, Paul Kimiti anasema CCM inapaswa kujikita kutoa elimu kwa wanachama wake ili wajue masharti na taratibu zake, tofauti na ilivyo sasa, wengi wanapoteza watu.
“Ni lazima tutengeneze mfumo wa kuwa na wanachama, si wingi, lakini ubora wa wanachama tunapaswa kutumia muda mwingi kutoa maelezo na mafundisho, wajue majukumu yao,” anasema.
Anasema kwa sasa hakuna wanachama wanaojua masharti ya CCM na walio wengi wanakutana kwenye majukwaa na wakimaliza, jambo linakuwa limeisha.
“Kuna siku moja nilitoa falsafa yangu ya Ta, Te, Ti, To, Tu (Tangaza sera ya chama chako, Tetetea sera ya chama chako, Timiza wajibu wako, Toa ushauri pale inapohitajika na Tubu kama umekisaliti chama,” anasema.
Kimiti, ambaye alikuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini kwa miaka 15, anasema suala la elimu linapaswa kurejeshwa na wasije wakadanganywa kwa mihemko ya mitaani, kwani kipindi cha sasa ni kuwa makini.
“Wanachama lazima wajue chama chao kinafanya nini na madhumuni yake ni nini na wao wajibu wao nini na si kwa wanachama tu, bali hata kwa viongozi. Ni lazima kuwe na mafunzo ya uongozi ya kusema uwazi kwa kuangalia tulikokwama,” anasema.
Aliyekuwa kada wa Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye Chadema, Profesa Abdallah Saffari anasema jambo ambalo CCM hawajawatendea haki wananchi katika miaka 48 ya utawala wao, ni kushindwa kuwapatia Katiba mpya.
“Kulikuwa na michakato, ikakwama, mfano, kwenye Bunge Maalumu la Katiba lililovunjika, kulikuwa na suala la Serikali tatu, kuna kiongozi mkubwa alisema hajaridhishwa nalo,” anasema.
Anaeleza kuwa suala la Katiba limekuwa gumu kutekelezwa, licha ya kwamba kulikuwa na Tume mbalimbali zilizokuwa zimeundwa kupendekeza, mathalani katika Bunge la Katiba lililovunjika waliondoka bila kujali wanalipwa posho.
“Kungekuwa na umakini, tungekuwa na Katiba na tungekuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, ingawaje kulikuwa na Tume ya Jaji ya Warioba, naweza kusema hata nayo pia haikuwa huru vilevile na nilishaandika makala,” anasema.
Anasema haikuwa huru kwa sababu wajumbe wengi walikuwa CCM, huku akisisitiza kwamba kutowapatia Watanzania Katiba kumeifikisha nchi hapa ilipo, labda kungelikuwa hakuna falsafa ya “No Reform No Election” kama mchakato ule ungekwenda vizuri.
“Hilo ni tatizo lililopo, kushindwa kupatikana kwa Katiba ambalo si jambo dogo, kungekuwa na Katiba mambo mengi yangebadilishwa, kwani katika mapendekezo ya upinzani tulikuwa tunahitaji kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court),” anasema.
Anasema Tanzania ni nchi pekee duniani ambayo hadi sasa haina mahakama ya juu na rasimu ya Jaji Warioba ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama hiyo.
“Tunahitaji kuwa na Mahakama hii, hata kufanya mabadiliko madogo kama tulivyoanzisha Mahakama ya Rufani. Tunatakiwa kuwa na Mahakama ya Juu kama Kenya yenye jukumu la kuangalia maamuzi yanayotolewa na mahakama ya rufani,” anasema.
Pamoja na mafanikio kiliyoyapata, Balozi Mndolwa anashauri chama hicho kirejeshe utaratibu wake wa awali wa kuwa na vyuo vya kuandaa vijana kuwa viongozi.
“Msukumo katika eneo hilo umepungua kwa sababu vyuo vingine vimeacha kufanya shughuli ya kuandaa watu kuwa viongozi baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi ambavyo vimekuwa vikipenyeza mamluki na kuwapambanisha wananchi,” anasema.
Anasema CCM inaendelea, lakini maadui wanazidi kuongezeka kwa sababu hata maadui kutoka nje nguvu zao zinaongezeka, hasa katika kuleta vurugu, jambo ambalo wanajitahidi kudhibiti kwa kuwa wanaona.
“Viongozi wa zamani na wale wapya ni lazima washirikishwe kwa ukaribu kwa sababu adui mara nyingi anaangalia viongozi waliopita kuwa mahasimu wa viongozi waliopo madarakani,” anasema.
Balozi huyo anasema ni lazima CCM ichukue hatua za haraka zaidi kuhakikisha wanawaenzi viongozi wa zamani ili wawe pamoja katika mapambano hayo kwa kushirikiana na waliopo madarakani.
Kwa upande wake, Dk Mbunda anasema CCM wanapaswa kuongeza nguvu katika kuisimamia Serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa sababu ni vigumu kutokana na namna kofia zilivyoungana.
“Rais wa nchi amekuwa mwenyekiti wa chama na viongozi wengi wakuu na imekuwa ngumu kwa viongozi wa chama kujisimamia na kungekuwa na mtu anayependa mabadiliko angeliangalia hilo,” anasema.
Dk Mbunda anashauri kuwa mtu anayetakiwa kubaki Serikalini basi aendelee na shughuli hizo, ili asimamiwe vizuri na chama na chama kinatakiwa kutetea ridhaa kilichopewa na wananchi kwa wivu mkubwa bila kuacha watu wakivuruge.
“Demokrasia ya ndani imekuwa ikipigiwa kelele na hasa katika chaguzi za ndani umekuwa ukikumbwa na rushwa nyingi, labda uongozi wa Magufuli walikuwa na fursa kubwa ya kufanya mabadiliko ndani ya chama kuzuia rushwa, lakini walishindwa,” anasema.
Anasema kwa kuwa hatua hazikuchukuliwa ipasavyo, katika uchaguzi ujao, hususan wanaogombea nafasi za ubunge na udiwani, unaweza kuwa hatari kwa maana ya watu kutembeza rushwa.
“Mtu anayetumia fedha nyingi kuingia madarakani haendi pale kwa ajili ya kuwatumikia watu, isipokuwa anaenda kulinda maslahi yake na huo ni upungufu mkubwa na sijui watafanyaje,” anasema Dk Mbunda.
Kwa upande wake, Profesa Saffari anasema pamoja na kuanzisha Mahakama ya Juu ili kuisimamia Mahakama ya Rufani katika kutenda haki, CCM wanatakiwa kuja na sera itakayosaidia kuhakikisha watu wanalipwa kulingana na uwezo wao.
“Tatizo hili linasababisha wengi wenye fani ya Profesa wanataka kuwa wabunge kwa sababu kule wengi wanapiga fedha, ni lazima tuwe na sera ya ajira kwa kuwa wafanyakazi wa kweli wanafanya kazi kwa shingo upande,” anasema.
Profesa Saffari anasema hali ilivyo sasa, Bunge linaifilisi Serikali na kuna ripoti ya Jaji Nyalali ilizungumzia sheria 40 kandamizi ambazo zinapaswa kuondolewa lakini bado hazijaondolewa.
“Ilipendekeza tusiende kwenye uchaguzi bila Tume Huru, na inasema nyumba zote zilizopatikana chini ya chama kimoja zirudi serikalini, hakuna kilichofanyika, ndiyo kwanza CCM wanachukua viwanja vya mpira,” anasema.
Kwa upande wake, Kimiti anashauri kuangalia viongozi wenye uwezo na uhakika wa kuwavusha kwenye nyakati ngumu na si kutegemea kupeana chochote (rushwa).
“Tuogope watu wanaopenda kutoatoa vitu kwa ajili ya kupata uongozi, ni lazima tuwe na wanachama wanaoomba nafasi za uongozi, tuseme kweli huyu anafaa,” anasema.