Geita yatajwa kusuasua uibuaji wagonjwa wa kifua kikuu

Geita. Mkoa wa Geita umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa tisa yenye uibuaji mdogo wa wagonjwa wa kifua kikuu (TB) kwa mwaka 2024, ambapo asilimia 11.46 ya waliolengwa, hawakuibuliwa hivyo kuendelea kuambukiza wengine.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Geita una watu zaidi ya milioni 2.9 ambapo kwa mwaka 2024 mkoa huo uliibua wagonjwa 3,643 sawa na asilimia 88.54 ya kadirio la wagonjwa 4,144 waliolengwa kuibuliwa.

Akizungumza na mwananchi leo Februari 5, 2025 Mratibu wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Mkoa wa Geita, Michael Mashala amesema mapema wiki hii mkoa huo ulizindua mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa kifua kikuu katika halmashauri sita za mkoa huo ili kuhakikisha walengwa waliopaswa kuibuliwa wanaibuliwa.

Mashala amesema kutoibuliwa kwa wagonjwa hao 825 kulitokana na sababu mbalimbali, ikiwemo upungufu wa vitendanishi na kusema kutoibuliwa kwa wagonjwa hao ipo hatari ya maambukizi kuongezeka kwa kuwa bado wanaishi na jamii.

“Hawa 825 tunawatafuta, hizi takwimu tunazipata baada ya kufanya uchunguzi. Na maeneo yenye maambukizi kwa wingi ni yale yenye machimbo ya madini na kambi za uvuvi, maeneo haya yanakuwa na msongamano mkubwa wa watu na hata makazi yao siyo rafiki, hivyo ni rahisi kuambukizana,” amesema Dk Mashala.

Akizungumzia njia zitakazotumika kuwapata wagonjwa 825 ambao hawajaibuliwa, amesema wamelenga kwenda kwenye maeneo yenye mikusanyiko ikiwemo maeneo ya machimbo, kambi za uvuvi na maeneo yote yenye mikusanyo ili kutoa elimu na kufanya uchunguzi, kuwabaini na kuwaanzishia matibabu.

Amesema pindi anapogundulika mgonjwa hufuatiliwa hadi kwenye familia, na kufanya uchunguzi ili kubaini kama yupo mwenye maambukizi, ili aweze kuanzishiwa dawa.

Kwa mwaka 2024 Tanzania ilikadiriwa kuwa na wagonjwa wapya 122,000 sawa na asilimia 183 kwa kila watu 100,000 na walioibuliwa na kuanzishiwa dawa ni wagonjwa 92,720 sawa na asilimia 76.

Aidha kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2024 kulikuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu milioni 10.8 duniani kote, kati ya hao wagonjwa milioni 1.25 sawa na asilimia 12 walipoteza maisha.

Akizungumzia ugonjwa wa kifua kikuu mkazi wa Geita, Method Makungu amesema bado elimu inahitajika ili wananchi waweze kujua dalili za ugonjwa huo.

Makungu ameshauri Serikali kuangalia ‘gesti bubu’ zilizopo maeneo ya machimbo na kutoa elimu, kwakuwa chumba kimoja hutumiwa na vijana zaidi ya 10, hivyo endapo atatokea mwenye maambukizi itakuwa rahisi kueneza ugonjwa huo kwa wengi zaidi.

Adam Batholomeo, mchimbaji mdogo wa madini Rwamgasa, amesema mara nyingi hubanwa na vifua kutokana na kazi ngumu na mazingira wanayoishi na kuiomba Serikali kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara, badala ya kuwasubiri waugue wafike hospitali wakati ambao wanakuwa wameshaambukiza wengine.

Hali ilivyo Tanzania na Kifua kikuu

Takwimu za Wizara ya Afya nchini Tanzania inaonyesha  kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 wagonjwa wa kifua kikuu walioibuliwa ni 400,031, kati yao watoto wakiwa 67,000.

Watu 132, 000, wanaambukizwa ugonjwa huo kila mwaka, huku wengine 25, 800 wakiripotiwa ambao ni wastani wa watu 70 kupoteza maisha kila siku takwimu zinazoipa Tanzania nafasi ya 30 duniani miongoni mwa nchi yenye wagonjwa wengi duniani.

Pamoja na idadi hiyo kubwa changamoto inayotajwa na Wizara ya Afya ni upatikanaji wa wagonjwa wanaoambukizwa kifua kikuu, bado ni tatizo kwa kuwa asilimia 35 ya wagonjwa hawagunduliki hivyo hukaa nyumbani bila matibabu.

Related Posts