Hali ilivyo Dodoma miaka 48 ya CCM, uwanja wafurika

Dodoma. Leo Jumatano, Februari 5, 2025 chama tawala nchini Tanzania – Chama cha Mapinduzi (CCM) kinasherekea miaka 48 ya kuzaliwa kwake na tayari mamia ya wanachama wamejitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma akwa ajili ya maadhimisho hayo.

Watu waliojitokeza ni wengi na magari yamekosa maeneo ya kuegesha, hadi eneo la wazi linalopakana na uzio wa uwanja wa ndege limeruhusiwa kwa ajili maegesho tofautili na ilivyo kawaida.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Polisi wamefunga uzio kuzuia magari na vyombo vingine vya moto kuingia ndani ya viwanja vya Jamhuri, abiria wanatakiwa kushukia uwanja wa ndege ambao uko jirani na uwanja wa jamhuri upande wa Kaskazini.

Magari ambayo yalifika mapema zaidi ni kutoka Wilaya ya Kongwa ambayo yalifika yakiwa yameongozana yakibeba ujumbe ‘Samia sisi Kongwa tumekuelewa, majibu tutakupa Oktoba 2025’.

Magari yaliyobeba wajumbe wa Dodoma mjini mengi yalikuwa ni yale ambayo hubeba wanafunzi wa shule binafsi, na haikujulikana mara moja wanafunzi hao wamefanyiwa mpango gani.

Askari wa Usalama Barabarani wameweka kambi katika eneo hilo wakiwaelekeza wenye magari jinsi ya kuyaegesha, huku mengine baada ya kushusha wajumbe yanageuza kufuata wengine.

Kwa mujibu wa ratiba ya maadhimisho hayo, mageti yamefunguliwa kuanzia saa 11 alifajiri. Saa 3 asubuhi wageni mbalimbali wataanza kuingia uwanjani.

Inatarajiwa saa 3:40 hadi saa 4:00 asubuhi, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia ataingia uwanjani hapo. Kisha atapokea maandamano ya wanaccm waliozaliwa Februari 5, 1977, vijana, bodaboda na baskeli.

Katika maadhimisho hayo, wagombea urais katika uchaguzi mkuu 2025 ambaye ni Rais Samia na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CCM watatambulishwa.

Aidha, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi naye atatambulishwa. Wote hao walipitishwa na vikao vya juu vilivyofanyika Januari 18-19, 2025 kuwa wagombea urais.

Saa 6:545 mchana, Rais Samia atahutubia wanachama waliojitokeza uwanjani hapo na watakaokuwa wakifuatilia vyombo mbalimbali vya habari.

Ratiba inaonyesha shughuli zitatamatika saa 8:10 mchana na Mwenyekiti, Rais Samia kuondoka uwanjani.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali.

Related Posts