Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu raia wa Burundi Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu Chuma cha Chuma, kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh500,000 baada ya kupatikana na hatia ya kuwepo nchini bila vibali.
Chuma ambaye ni msanii wa muziki na mkazi wa Mbezi Louis, jijini Dar es Salaam anadaiwa kutenda kosa hilo, Septemba 18, 2024 eneo la Upanga, Las Vegas Casino, lililopo Wilaya ya Ilala.
Uamuzi huo umetolewa leo, Jumatano Februari 5, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Yusto Ruboroga baada ya kumtia hatiani kama alivyoshtakiwa.
Hakimu Ruboroga amesema upande wa mashtaka ulileta mashahidi wawili na vielelezo viwili kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.
Amesema mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya pili, hivyo anahitaji kupewa adhabu kali.
“Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa na upande wa mashtaka umethibitisha pasina kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria,” amesema Hakimu Ruboroga.
Awali, Wakili wa Serikali, Hadija Masoud amedai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu na upande wa mashtaka upo tayari kusikiliza.
Pia ameomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kwa kuwa ni mkosaji kwa mara ya pili.
“Mshtakiwa alishawahi kutiwa hatiani katika kesi ya jinai namba 83 ya mwaka 2023 katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni mbele ya Hakimu Rahim Mushi kwa kosa kama hili na alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita” amedai wakili Masoud na kuongeza
“Mshtakiwa aliingia nchini mwaka 2022 kupewe viza ya matembezi ya siku 60 na ilivyoisha hakurudi Idara ya Uhamiaji, kuomba tena kama sheria inavyotaka,” amedai Masoud.
Katika mahojiano na mshtakiwa, amesema ilibainika aliishi nchini kinyume cha sheria kwa sababu viza yake iliisha muda wake Agosti 11, 2022.
Na baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje, mahakama hiyo ilimuelekeza mshtakiwa afuatilie vibali vya kuishi nchini katika ofisi za uhamiaji, lakini hakufanya hivyo.
“Kutohalalisha vibali vya kuishi nchini na kuwepo kwa mshtakiwa nchini ni wazi mshtakiwa sio mtiifu kwa mahakama na sio mtiifu kwa Nchi ya Tanzania na kwa makusudi ameonyesha jinsi ambavyo hakujali sheria zetu za nchi.
“Suala la uhamiaji haramu ni mtambuka na limekuwa likiigharimu Serikali katika kuwatunza, kuwahudumia, hivyo linatakiwa kukomeshwa kwa mahakama yako kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kwani sio mara yake ya kwanza kutiwa hatiani kwa kosa kama hilo,” amedai Wakili Masou.
Wakili Masoud ameomba mahakama, ijielekeze katika kifungu 42(2) cha Sheria ya Uhamiaji Sura 54.
Kabla ya kuadhibiwa, Chuma cha Chuma alipewa nafasi ya kujitetea kwanini asiadhibiwe vikali mbele ya mahakama hiyo na katika utetezi wake, ameomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ana mtoto wa miezi tisa anayeumwa na anatakiwa kufanyiwa upasuaji haraka.
“Mheshimiwa hakimu, nimekaa rumande miezi mitano sasa, polisi nilikaa miezi miwili na mahabusu ya gerezani nimekaa miezi mitatu, hivyo naomba katika hukumu unayokwenda kuitoa unipunguzie adhabu” amedai mshtakiwa.
Mshtakiwa huyo amedai ameoa mtanzania aliyezaa naye mtoto, hivyo anaomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa wameshaunganisha damu kwa nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.
“Huyu mwendesha mashtaka anaomba nipewe adhabu kali kwa kuwa anafuata sheria lakini hajafuata utu anaona kama ananikomoa, lakini yeye ni mama na uchungu wa mwana aujuaye mzazi, hivyo anaona ananikomoa mimi kumbe anamkomoa ndugu yake,” amesema.
Ameongeza:”Wakati kesi hii ikiendelea na usikilizwaji, mke wangu na mtoto walikuwa wanakuja kushinda uhamiaji, lakini mwendesha mashtaka ameshindwa kuwa na utu na badala yake anaomba nipewe adhabu kali.”
Katika utetezi wake huo, amedai ili kuthibitisha ndoa yake anacho cheti halali, kadhalika cheti cha kuzaliwa cha mwanawe aliyezaliwa katika Hospitali ya Serikali.
Sababu za mshtakiwa kupewa adhabu hiyo:
Hakimu Ruboroga baada ya kusikiliza shufaa ya mshtakiwa pamoja na maombi ya upande wa mashtaka, ametupilia mbali ombi hilo la kupunguziwa adhabu.
Amesema mshtakiwa alikwenda Kituo cha Polisi kuchukua hati yake ya kusafiria ili aishi nchini kwa kigezo kuwa ameoa Mtanzania, badala ya kuhuisha vibali vyake.
“Na pia sio kosa lake la kwanza, mshtakiwa alishawahi kuhukumiwa kwa kosa la kuwepo nchini bila kuwa na kibali, licha ya hati yake ya kusafiria ilikuwa bado haijaisha muda wake,” amesema na kuongeza.
“Hakuna ubishi kuwa mshtakiwa ulikuwa unaishi nchini kinyume cha sheria na wala huna ushahidi wala nyaraka au kielelezo chochote kinachoonyesha kuwa uliomba kibali uhamiaji na ukanyimwa wala hakuna ubishi kuwa ulijua viza yako ilikuwa imeisha muda wake na wewe ukaendelea kuishi nchini,” amesema.
Hakimu Ruboroga amesema mashahidi wawili waliotoa ushahidi wao kutoka Polisi na Idara ya Uhamiaji, walieleza namna ulivyokamkamata mshtakiwa kwa mara ya kwanza na mara ya pili, baada ya viza kuisha muda wake.
“Mshakiwa kwa makusudi, uliamua kuishi nchini bila nidhamu na kinyume cha sheria na wala hukuenda kuhuisha kibali chako Idara ya Uhamiaji.
“Mshtakiwa ulikuwa unaishi unavyotaka wakati ukijua kuwa ni kinyume cha sheria, hivyo mahakama imeona wewe ni mkosaji wa mara ya pili na ina wajibu wa kutoa adhabu kali,” amesema Hakimu Ruboroga kisha kutoa adhabu.
Wakati akitoa adhabu hiyo, amesema mshtakiwa anahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh500,000, lakini anayo haki ya kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na uamuzi.
Chuma anadaiwa kutenda kosa hilo, Septemba 18, 2024 eneo la Upanga, Las Vegas Casino, Ilala, Dar es Salaam.
Inadaiwa kuwa, mshitakiwa akiwa eneo hilo, alibainika kuwepo nchini bila kuwa na kibali, wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya jinai namba 31005 ya mwaka 2024.