Jela maisha kwa kubaka mtoto wa miaka mitano

Mbeya. Mahakama ya Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya, imemhukumu kutumikia kifungo cha maisha Kiswigo Mwakalinga (20) mkazi wa Kijiji cha Ibale kwa kosa la kubaka mtoto wa miaka mitano.

Hukumu hiyo imesomwa Januari 28, 2025 mbele ya Hakimu mkazi, Paul Barnabas baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo pasipo shaka.

Awali, mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi, Bihemo Mayengela alieleza mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Oktoba 29, 2024 kwa kumvizia mhanga alipokuwa akiengue maembe.

Mayengela amesema siku ya tukio mhanga alikuwa ameambata na mtoto mwenzake wakiwa wanaengua maembe mshtakiwa alitumia mbinu ya kuwafuata kwa lengo la kujumuika na kuengua.

Amesema mwathiriwa na mwenzake hawakuweza kumtilia mashaka mshtakiwa kwa kuwa walikuwa wakiishi kijiji kimoja na walikuwa na mazoea.

Upande wa mashtaka umeendelea kueleza kuwa baada ya muda mshtakiwa alimshika mkono mhanga na kumpeleke kwenye migomba ambako alimbaka na kisha kumtishia akisema atamuua.

Upande wa mashtaka uliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za kubaka watoto walio chini ya miaka mitano.

Kufuatia maelezo yaliyotolewa na upande mashtaka ukiwepo ushahidi wa daktari kuthibitisha mtoto huyo kuingiliwa kimwili pasipo shaka ndipo hakimu, Paul Barnabas alimhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha maisha jela.

Hakimu Barnabas amesema hukumu hiyo imezingatia kifungu cha sheria 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (e) na kifungu kidogo cha 131 kifungu kidogo cha kwanza vyote vya sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Hata hivyo mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea , aliomba mahakama impunguzie adhabu ombi ambalo lilitupiliwa mbali.

Mkazi wa mtaa wa mikoroshini Wilaya ya Kyela, Anna Sanga ameomba vyombo vya dola kukazia sheria kwa kuweka adhabu kali ili kuwa fundisho kwa vijana wenye tabia za kujihusisha na matukio ya ubakaji na ulawiti.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amelieleza Mwananchi Digital kuwa kwa kipindi cha Januari, 2025 kesi 979 zimefikishwa katika mahakama mbalimbali.

Amesema kati ya kesi hizo, 186 zimepata mafanikio kwa watuhumiwa kuhukumiwa vifungo na kulipa faini huku kesi 673 ziko kwenye hatua mbalimbali.

Related Posts