Mabosi wa Yanga walishtushwa na uamuzi wa ghafla wa kocha Sead Ramovic ambaye aliomba kuvunja mkataba wake kisha jana Jumanne, Februari 4, 2025 akawaaga wachezaji na maofisa wengine wa timu akiwatonya kuwa amepata ofa nono huko Algeria.
Baada ya kuzungumza naye walibaini kuwa CR Belouizdad ya Algeria imempa ofa nono ya mshahara zaidi ya mara mbili ya ule wanaomlipa hivyo wakashindwa kumzuia na kumruhusu aende.
Katika kufanya tathmini yao kwa haraka wakagundua kuwa kocha ambaye anaweza kubeba mikoba ya timu hiyo kwa haraka ni Hamdi Miloud wa Singida Black Stars hivyo wakafanya mawasiliano na kigogo mwenye uamuzi wa mwisho ndani ya timu hiyo ambaye alimruhusu kocha huyo kujiunga na Yanga ambayo naye ana mahaba nayo.
Haraka Miloud akatangazwa Yanga ambayo baadaye ilianika hadharani wasifu wake ambao ulionyesha kuwa Mualgeria huyo ana leseni daraja A iliyotolewa na Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa).
Kama Bodi ya Ligi Kuu Tanzania na idara ya ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) watasimamia vyema kanuni za Ligi Kuu msimu huu, hakuna namna Miloud atalazimika kushushwa cheo na kuwa kocha msaidizi kwa daraja lake la leseni halitoshi kumfanya awe kocha mkuu wa timu inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC na badala yake anapaswa kuwa msaidizi.
Kanuni ya 77 ya Ligi Kuu imefafanua sifa za kocha mojawapo ikiwa ni hadhi ya leseni inayofafanua kuwa kocha mwenye leseni kutoka nje ya Afrika anapaswa kuwa na ngazi ya Pro Diploma ambayo kwa Afrika ni sawa na Diploma daraja A.
“(1) Kila klabu inapaswa kuajiri Kocha Mkuu na wasaidizi wenye sifa na ujuzi kwa timu ya kwanza (wakubwa) na za vijana (U20 na U17) wanaokubalika kwa mujibu wa taratibu za TFF na mikataba yao kusajilia TFF.
“(2) Kocha toka nje ya nchi atathibitishwa kwanza na TFF kwa kuzingatiwa pia kupatikana kwa kibali stahili cha kuishi na kufanya kazi chini kabla ya kuingia mkataba na klabu.
“(3) Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na angalau Diploma A ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya mabara mengine yanayotambuliwa na FIFA. Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na angalau Diploma B ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya mabara mengine yanayotambulia na FIFA.
“3.1 Kocha mkuu wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau Pro Diploma au inayolingana nayo. 3.2 Kocha msaidizi wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau A Diploma au inayolingana nayo.
“Kocha wa timu ya Ligi Kuu kutoka nje ya Tanzania ni lazima awe amefundisha klabu ya Ligi Kuu au timu ya Taifa katika nchi yoyote ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita,” inafafanua kanuni hiyo.
Wakati kanuni zikimbana Miloud, kocha msaidizi Abdihamid Moalin yeye ana sifa stahiki za kuliongoza benchi la ufundi la Yanga kwa vile ana leseni daraja A inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).