Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limelaani kitendo cha Marekani cha kumpokea waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Februari 2, 2025, Netanyahu aliondoka kuelekea Marekani ili kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump na kuwa kiongozi wa kwanza wa nje kukutana na Trump tangu arejee Ikulu ya White House.
Amnesty International imelaani hatua hiyo ya serikali ya Marekani ya kumpokea, ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
![](https://globalpublishers.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1674583481856-3701921548-1024x576.jpg)
Katika taarifa yake, Amnesty imesema: “Kwa kumkaribisha Netanyahu, ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,(ICC) Marekani inaonyesha isivyojali na kuheshimu haki na uadilifu wa kimataifa.”
Taarifa hiyo imeongezea kwa kusema: “Serikali ya Joe Biden ilizikejeli juhudi zote za kimataifa za kutaka haki na uadilifu utendeke kuhusiana na Palestina, na hivi sasa kutokana na Donald Trump kushindwa kumkamata au kumchunguza Netanyahu, amemfanya mtawala wa kwanza wa kigeni kufika Ikulu ya White House tangu aingie tena madarakani na kumpa mapokezi yenye hadhi maradufu.”
Amnesty International imesisitiza katika taarifa hiyo kwamba Marekani ina wajibu chini ya Mikataba ya Geneva kuwashtaki au kuwafikisha mahakamani wale wanaotuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita.