Mfanyakazi Mgodi wa Mwadui adaiwa kujinyonga, aacha ujumbe ukisomeka…

Shinyanga. Mkazi wa Mtaa Mwamala, kata Masekelo mkoani Shinyanga, Andrea Kisandu (43) inadaiwa amejinyonga hadi kufa nje ya nyumba yake katika mti, huku ukukitwa ujumbe kwenye mfuko wa shati alilokuwa amevaa.

Tukio hilo la kifo cha Kisandu ambaye alikuwa mfanyakazi wa Mgodi wa Willingson Mwadui, limetokea jioni ya jana Jumanne, Februari 4, 2025.

Leo Jumatano, Februari 5, 2025, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na Mwananchi amesema baada ya kupata taarifa na kufanya uchinguzi wakagundua kwenye kitabu chake cha kumbukumbu ameandika:”Ameamua kwa hiari yake na mali alizochuma yeye na mkewe wapewe mke na watoto wake watatu.”

Kamanda Janeth ametoa wito kwa wananchi warejee imani zao na kuacha kujichukulia sheria mkononi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwamala, Juma Maswa amesema namna alivyopokea taarifa hizo za kusikitisha na kushangaza katika mtaa wake.

Amesema alikuwa ofisi ya mtendaji kwa ajili ya upokeaji wa miti kugawia wananchi waipande, wakati anarudi nyumbani alikutana na kijana mmoja akamweleza kuna mtu kajinyonga na kuamua kwenda eneo la tukio na kweli alikuta kajinyonga.

“Ikabidi nimpigie mtendaji wa kata na Polisi kata wakaja na kumtoa tukagundua kwenye shati alilokuwa amevaa kuna ujumbe aliandika “msimuhusishe mke wangu nimeamua kufanya hivi mwenyewe” tukampigia baba wa marehemu,” amedai Maswa.

Kwa upande wake, Bena Kisandu, baba mdogo wa marehemu akizungumza na Mwananchi amesema alipigiwa simu kujulishwa mwanaye kudaiwa kujinyonga na moja kwa moja na alipofika akakuta mwili umepelekwa monchwari.

“Sijajua ni nini hasa kimetokea, isipokuwa waliwahi kupishana kauli mwaka jana lakini mwezi wa 10 na mwenzake, lakini walikuja nyumbani tukakaa kikao tukazungumza yakaisha wakawa wanaishi vizuri, sasa sijui nini kimebadilika. Alikuwa ameajiriwa Mgodi wa Willingson Mwadui,” amesema Kisandu.

Pia jirani wa familia hiyo, Salome Godfrey amesema namna walivyokuwa wakiishi na familia ya marehemu: “Nasikitishwa na msiba huu kwa sababu si kawaida katika mtaa wetu, ni mtu ambaye alikuwa mchangamfu kwa kila mtu hata familia yake alikuwa anaihudumia vizuri, hajawai kumpita mtu bila kumsalimia sijui ni nini kilimkuta akashindwa kushirikisha watu.”

Related Posts