Miili ya wachimbaji wawili waliofukiwa na kifusi Kahama yaagwa

Kahama. Miili miwili ya wachimbaji wa madini ya dhahabu waliofariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi katika mgodi wa Nkandi eneo la Mwime Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imeagwa leo Jumatano, Februari 5, 2025 huku kukatika umeme mara kwa mara ikitajwa kukwamisha uokoaji.

Miili hiyo ni miongoni mwa wachimbaji watatu waliofukiwa na kifusi Februari Mosi, 2025 wakati wakiendelea na shughuli zao katika duara namba saba la mgodi huo, jitihada za kumtafuta mchimbaji mmoja zikiendelea.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga, Thomas Majuto amesema miili hiyo ni ya Charles Kinguru anayekadiriwa miaka kati ya 30 hadi 35 na Robert Henry mwenye miaka kati ya 25 hadi 30.


Miili ya wachimbaji wawili waliofukiwa na kifusi Kahama yaagwa

Akiongoza waombolezaji kuaga miili hiyo, leo Jumatano Februari 5, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amesema wakati jitihada za kumpata mchimbaji aliyesalia ardhini zikiendelea, Serikali imeona ni vyema waliopatikana wapewe heshima zao za mwisho ili wapumzishwe kwenye nyumba zao za milele.

Amesema chanzo cha vijana hao kufikwa na mauti ni changamoto ya hali ya hewa sambamba na ardhi ya eneo hilo kufyonza maji hivyo, kusababisha ajali za namna hiyo mara kwa mara, akieleza Serikali ya wilaya hiyo inaendelea kuchukua tahadhari kutokana na hali hiyo ya hewa.

“Walikuwa kwenye harakati za kujitafutia riziki, ni changamoto ya mazingira ya hali ya hewa ndiyo imepelekea ajali hii kama ambavyo imekuwa ikijitokeza wakati mwingine, pindi hali ya hewa kama hizi zinapojitokeza,” amesema Mhita.

Meneja wa mgodi wa Nkandi, Mdaki Shabani amesema shughuli ya kumtafuta mchimbaji mmoja anayesadikiwa kusalia chini ya kifusi zinaendelea lakini changamoto kubwa ni kukatika kwa umeme mara kwa mara hali inayosababisha kusimama kutokana na maji kujaa kwenye maduara.

“Wenzetu Tanesco kwenye eneo hilo bado wanakatakata sana umeme, maana yake wanatukwamisha kufanikisha zoezi kwa haraka, kwa hiyo niwaombe Tanesco kupitia hii changamoto tuna uhitaji sana wa umeme kuliko kitu kingine ili tukamuokoe mwenzetu ambaye anasadikiwa yupo katika eneo la kina kirefu,” amesema Mdaki.

Hata hivyo, Meneja wa Tanesco wilayani Kahama, Kisika Elia akizungumza kwa simu amesema hana taarifa za kuwepo kwa changamoto hiyo katika eneo la hilo.

“Mimi sina taarifa, taarifa ambayo ipo labda kama umeme umekatika kote tunashughulikia unarudi, taarifa ya kukosekana umeme pale sina” amesema Kisika.

Penina Nyagwaswa mmoja wa ndugu wa marehemu ameishukuru Serikali pamoja na uongozi wa mgodi kwa ushirikiano waliouonesha tangu mwanzo kufanikisha kuwapata ndugu zao.

Hilo siyo tukio la kwanza la wachimbaji kufukiwa na kifusi wilayani Kahama ambapo, mwaka 2015 wachimbaji 11 wa dhahabu waliokolewa kwenye mashimo yaliyopo Nyangarata, baada ya mashimo hayo kutitia mara mbili, huku mmoja akifariki dunia.

Related Posts