Mkutano wa TAMSTOA waibua changamoto za Malori

CHAMA cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati Tanzania(TAMSTOA), wameiomba Serikali kushughulikia changamoto wanazokutana nazo hasa kamatakamata ya malori na ufinyu wa barabara.

Akizungumza katika Mkutano wa tano wa mwaka 2024 wa chama hicho uliofanyika leo Februari 5, 2025, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAMSTOA, Shaban Chuki, alisema alisema barabara kutoka bandarini bado ni shida, hivyo kuomba kujengewa hata za vumbi.

Alisema viongozi watambue kuwa magari yamekuwa yakiongezeka lakini miundombinu bado imebaki ile ile.

Aidha alisema sehemu inayowapa kero zaidi kwa upande wa Dar es Salaam ni Wilaya za Temeke na Ubungo kutokana na ukamataji unaondelea.

“Magari yote yanayobeba mizigo kutoka nje ya nchi yanategemea bandari ya Dar es Salaam na hasa wilaya ya Temeke. Naomba Viongozi wa Temeke watambue ongezeko la malori ni fursa na neema na si karaha, imegeuzwa sasa hivi kuona malori kuwepo ni karaha, licha ya kuchangia pato la Taifa kutengeneza hizi barabara lakini hatuthaminiwi.

“Ninaomba tukae pamoja tupange tuoneshwe ni wapi tunatakiwa kubaki, wapite kwa utaratibu upi? Na tufahamu kuwa si wote wanaokuja kuchukua mizigo bandarini sio wote wana sehemu maalumu ya kupaki,” alisema Chuki.

Ameeleza kuwa vitendo vya kukamatwa bila utaratibu vimekuwa ni changamoto kubwa kwao kutokana na kusababisha uwepo wa vibaka na vishoka wanaotaka fedha kutoka kwa madereva.

Kutokana na hilo wameiomba Serikali kuwatafutia eneo maalumu la kubaki malori na kuitaka TRA kutembelea wasafirishaji na kuacha kamatakama eneo la Mikumi mkoani Morogoro ambako kumekuwa ni chanzo cha rushwa.

“Katika kipindi cha mwaka 2024 tumeweza kutatua changamoto kamatakamata malori wilayani Temeke na Ubungo mkoani Dar es Salaam, japo bado tatizo halijaisha. Tunaionba Serikali ifanyie kazi,” alisema Chuki.

Pia chama hicho kimeiomba Serikali kupitia TANROADS kupanua barabara ya Morogoro kutoka bandarini hadi Chalinze na Mbozi hadi Tunduma.

Akitoa taarifa ya chama tangu kuanzishwa kwake alisema kimefikisha jumla ya wanachama 900 ambao wanamiliki zaidi ya malori 26,000.
Alisema uwepo wa malori hayo umeweza kutoa ajira kwa watanzania 52,000 ambao ni madereva na wasaidizi.

Alisema lengo la TAMSTOA ni kusimamia na kutatua changamoto inayohusisha sekta ya usafirisha kwa njia ya barabara pamoja na kutetea maslahi ya wanachama kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.

Pia kuhamasisha wamiliki wa malori kutoa mikataba madereva kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira, ikiwamo kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki ya biashara ya usafirishaji ili kuongeza pato la Taifa.

Alieleza kuwa malori yanayomilikiwa na wanachama hao, yakipata mzigo kwa wakati mmoja yanatumia zaidi ya lita milioni 62.4 za mafuta, zinazogharimu zaidi ya sh. milioni 187 kwa siku kwa mwaka ikiwa ni zaidi ya sh trilioni mbili.

“Kwa takwimu hizo ni wazi kuwa sekta ya usafiri ina mchango mkubwa kwenye pato la Taifa na jamii kwa ujumla.

Kuhusu vita ya DR Congo, Mwenyekiti huyo amesema wanaishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuwaokoa madereva wote walikuwa katika Mji wa Goma.

Kwa upande wake mwakilishi wa mgeni rasmi katika mkutano huo, Geoffrey Silanda aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Professa , alisema TAMSTOA imekuwa na itaratibu wakufanya mkutano kuzungumzia mafanikio na changamoto zao.

Silanda amesema kwa niaba ya Serikali kupitia wizara ya Uchukuzi, wamekuwa wakishirikiana kutatua changamoto mbalimbali ikiwamo suala la upimaji wa mizigo katika mizani ambalo linatafutiwa ufumbuzi pamoja na ukamataji wa eneo la mikumi.

“Kweli kumekuwa na changamoto katika maeneo ya maegesho hapa nchini, TANROADS imeelezwa kutafuta maeneo mbadala ya maegesho”, alisema.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kufanya tathimini ya kile walichokifanya katika kipindi cha miaka 10 tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 2014.
Meneja Usalama Barabarani na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Geoffrey Silanda akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa 5 wa chama cha wamiliki wa malori nchini TAMSOA uliofanyika jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mwenyekiti wa TAMSTOA ,Chuki Shabban na Kushoto ni Mkaguzi wa Polisi Makao makuu Dumu Mwalukenge


Afisa Mauzo wa kampuni ya GF Trucks & Equipments Ltd ,Mohamed Mlula akielezea ubora wa magari yanayo tengenezawa na kiwanda cha kampuni hiyo kilichopo Kibaha,Meneja Usalama Barabarani na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Geoffrey Silanda wakati akikagua mabanda kwenye mkutano wa wamiliki wa malori wadogo nchini TAMSTOA uliofanyika jijini Dar es salaam jana

Related Posts