KWA dau hili hata ungekuwa ni wewe usingebaki. Ndio, imefichuka kwamba aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Sead Ramovic aliye mbioni kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria atavuta mshahara wa kibosi, tofauti na ule aliyokuwa akilipwa na Yanga.
Kocha huyo raia wa Ujerumani, aliyejiunga na Yanga katikati ya Novemba mwaka jana akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini na kuiongoza timu hiyo katika mechi 11 tofauti zikiwamo sita za Ligi Kuu Bara, sita nyingine za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho (FA), ameachana na klabu hiyo kutokana na dili la pesa ndefu alilonasa huko Algeria.
Duru za kispoti, zinasema kuwa mara atakapotua CR Belouizdad inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria (Ligue 1) kama alivyoiacha Yanga katika Ligi Kuu Bara nyuma ya Simba, atakuwa akilipwa mshahara wa Dola 40,000 (karibu Sh102 milioni) kwa mwezi, ikiwa ni karibu mara tatu ya kile alichokuwa akipata Jangwani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyanzo mbalimbali, Yanga ilikuwa inamlipa Ramovic Dola 15,000 (Sh38 milioni) kwa mwezi, kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na kile atakachopokea huko Algeria.
Mjerumani huyo aliyejulikana kama ‘Germany Mashine’, alikubaliana na ofa ya CR Belouizdad na alitarajiwa kutua Algeria kuanzia leo Jumatano kwa ajili ya kutambulishwa rasmi kama kocha mpya wa timu hiyo.
Ramovic atachukua nafasi ya Abdelkader Amrani, aliyekuwa akiongoza timu hiyo, lakini alijiuzulu kutokana na matokeo mabaya yaliyosababisha timu yake kushindwa kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Ramovic naye alikwama kuivusha Yanga kutinga robo fainali katika michuano hiyo.
Ripoti kutoka Algeria zinaeleza, baada ya kumalizana na Yanga, Ramovic na msaidizi wake, Mustafa Kodro, walianza mara moja taratibu za safari kwani tayari walikuwa na tiketi za ndege.
Hata hivyo, CR Belouizdad imeilipa Yanga fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wa kocha huyo, ambapo inasemekana wametoa zaidi ya dola 50,000 (zaidi ya Sh127 milioni) kama fidia hiyo.
Taarifa kutoka kwa gazeti la An-Nahar zinaeleza kuwa hatua ya kumshawishi Ramovic kuhamia CR Belouizdad ilianza wiki chache ziliyopita, baada ya kocha aliyepita kushindwa kuiongoza timu hiyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii ni baada ya CR Belouizdad kushika nafasi ya tatu katika kundi C, ikiwa na pointi tisa, nyuma ya Al Ahly (pointi 10) na Orlando Pirates (pointi 14).
Kwa sasa, CR Belouizdad inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ya Algeria, ikiwa na pointi 26, nyuma ya Mouloudia Algiers kwa tofauti ya pointi mbili tu.
Ramovic anatarajiwa kuongoza benchi la ufundi la CR Belouizdad katika mchezo wa fainali ya Super Cup dhidi ya MC Alger wikiendi ijayo.