Mtukufu Aga Khan IV afariki dunia

Mwanza. Kiongozi Mkuu wa 49 wa Madhehebu ya Shia Ismailia na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Mtukufu Aga Khan, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Mtukufu Aga Khan anayefahamika kama Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, alifariki dunia jana Jumanne Februari 4, 2025, jijiji Lisbon, Ureno akiwa amezungukwa na familia yake.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kwa umma, baada ya kifo cha mfalme huyo, Imamu wa 50 wa madhehebu ya Shia Ismailia atatangazwa kurithi mikoba ya Aga Khan IV.

Enzi za uhai wake, Mtukufu Aga Khan alifahamika kutokana na mchango wake kwenye shughuli zinazochangia kuimarisha ustawi wa maisha ya binadamu katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

“Kipindi chote cha uhai wake duniani, Aga Khan IV alikuwa akisisitiza Uislamu ni fikra na imani inayohitaji kujitoa na uhimilivu, na kuendeleza utu wa mwanadamu,” imesema taarifa rasmi kutoka nchini Ureno.

Kiongozi huyo alizaliwa Desemba 13, 1936, jijini Geneva, Switzerland katika familia ya Aly Khan na Joan Yarde-Buller, ambaye ni mzaliwa wa Uingereza. Karim, aliishi maisha yake ya utoto jijini Nairobi nchini Kenya.

Kutokana na kuishi katika ukanda wa Afrika Mashariki, mchango wake ulionekana kwa kuanzisha kwa Taasisi za Aga Khan zilizoleta tija na manufaa mbalimbali kwa umma katika ukanda huo.

Kutokana na shughuli za kielimu, Aga Khan alijikuta nchini Switzerland, ambako alipata elimu ya dini katika Shule ya Le Rosey, kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard kilichopo nchini Marekani.

Wakati baba yake anafariki dunia, Karim alikuwa masomoni akibobea katika Imani ya Kiislamu katika chuo hicho.

Huku akiwa mrithi wa 49 wa nafasi ya Imamu wa madhehebu ya Ismailia, Karim katika umri mdogo alikatisha ndoto yake ya kuwa mchezaji wa soka na kuendelea na elimu katika ngazi ya Uzamivu (PhD), chuoni Harvard.

Alilazimika kukatisha ndoto hizo baada ya kuteuliwa kurithi mikoba ya uongozi wa kiroho wa mamilioni ya waumini wa madhehebu hayo ambayo kwa wakati huo yalikuwa yamesambaa maeneo mengi uliwenguni, hususan India, Kenya, Pakistan, Bangladesh, Misri, Canada na Jumuiya ya Kisovieti (Urusi).

Akiwa kiongozi wa kiroho, alitwishwa jukumu la kuwa Imamu wa 49 wa madhehebu ya Shia Ismailia, wadhifa ambao aliutumikia kwa udi na uvumba.

Hata hivyo, wajibu wake haukuishia kuwa kiongozi wa kidini, bali alikuwa mwanzilishi wa shughuli mbalimbali zilizoleta mabadiliko ulimwenguni, hususan kwenye sekta ya afya, utamaduni, elimu, habari na maendeleo ya jamii katika kanda zote duniani.

Maeneo mengine aliyoyagusa moja kwa moja ni pamoja na sekta ya uwezeshaji kiuchumi ambako aliibua mikakati ya kuongeza ustawi katika jamii.

Mtukufu Aga Khan ameacha nembo isiyofutika maeneo mbalimbali duniani hususan nchini Kenya na Tanzania ambako alianzisha taasisi mbalimbali zilizoleta mchango mkubwa katika maisha ya raia wa nchi hiyo.

Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Shule za Aga Khan, Chuo Kikuu cha Aga Khan, vyote vilianzishwa ikiwa ni ishara ya kujitoa kwake kuikomboa jamii ya eneo husika.

Pia alianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (AKFED), mfuko huo ulichochea maendeleo endelevu huku ukitumia kauli yake: “AKFED hailengi kutengeneza faida ila ni mpango wa maendeleo ya kesho.”

Pia ni mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ambao umeleta tija maeneo mbalimbali hususan katika sekta ya afya, elimu na utamaduni hususan uwezeshaji kiuchumi maeneo ya vijijini nchini Tanzania na Kenya.

Uwepo wa Aga Khan nchini Tanzania unaonekana kupitia uanzishwaji wa kampuni mbalimbali ikiwemo ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Hospitali za Aga Khan na miradi mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.

Nchini Kenya, mchango wake unaonekana kupitia taasisi na kampuni mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo Kampuni ya Nation Media Group (NMG) na viwanda mbalimbali ikiwemo Industrial Promotion Services (Kenya) Ltd, Allpack Industries Ltd, Farmer’s Choice Ltd, Premier Food Industries Ltd na Tourism Promotion Services Eastern Africa Ltd na vingine.

AKDN pia imeleta mchango katika jamii za maeneo mbalimbali hususan barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati kwa kuzifikia jamii zilizosahaulika katika maeneo hayo.

Related Posts