Mtukufu Aga Khan, anayefahamika kama Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, alijulikana kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha ustawi wa binadamu kupitia miradi mbalimbali duniani.
“Katika maisha yake, Aga Khan IV alisisitiza Uislamu ni imani inayohimiza kujitolea, uvumilivu, na utu wa mwanadamu,” inasema taarifa rasmi kutoka Ureno.
Alizaliwa Desemba 13, 1936, Geneva, Uswisi, na alikulia Nairobi, Kenya. Alipata elimu katika shule ya Le Rosey nchini Uswisi na Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, ambako alisomea masomo ya Uislamu.
Baada ya kifo cha baba yake, aliacha ndoto zake za soka na masomo ya uzamivu ili kuchukua wadhifa wa Imamu wa 49 wa madhehebu ya Shia Ismailia.
Mbali na uongozi wa kidini, alihimiza maendeleo ya jamii kupitia sekta za afya, elimu, habari, utamaduni, na ustawi wa jamii.
Alianzisha miradi kama Shule na Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (AKFED), na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), ambao umeleta maendeleo katika afya, elimu, na uchumi, hasa Afrika Mashariki.
Nchini Tanzania, mchango wake unaonekana kupitia Mwananchi Communications Limited (MCL) na Hospitali za Aga Khan, huku nchini Kenya alianzisha Nation Media Group (NMG) na viwanda kadhaa.
AKDN imeleta mafanikio katika jamii barani Afrika, Asia, na Mashariki ya Kati kwa kusaidia maendeleo katika maeneo yaliyoachwa nyuma.
Uteuzi wa Imam wa 50 na mazishi Imam wa 50 wa urithi tayari ameteuliwa, na atatangazwa rasmi baada ya wasia wa Mtukufu Aga Khan IV kusomwa katika siku zijazo. Taratibu za mazishi zitatangazwa hivi karibuni.
Kifo cha Mtukufu Prince Karim Aga Khan IV kinahitimisha enzi ya uongozi wa kipekee na huduma kwa binadamu, lakini urithi wake wa maendeleo na ustawi wa kijamii unaendelea kuhamasisha vizazi vijavyo.