LICHA ya kuondoka kwa kocha Sead Ramovic, moto wa Yanga katika Ligi Kuu Bara haujapoa baada ya jioni ya leo kuinyoosha bila huruma KenGold iliyofanya usajili wa maana kupitia dirisha dogo kwa kuifumua mabao 6-1, huku ikishuhudiwa na kocha mpya, Hamdi Miloud aliyekuwa jukwaani.
Ushindi huo ndio mkubwa zaidi katika ligi hiyo kwa msimu huu hadi sasa na ulipatikana kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam, huku washambuliaji Prince Dube na Clement Mzize kila moja akifunga mabao mawili na kuifanya Yanga katika mechi saba mfululizo kufunga jumla ya mabao 28.
Ushindi huo wa 15 umeifanya Yanga irejee kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 45 baada ya mechi 17.
KenGold iliyoshindwa kuwatumia baadhi ya nyota wapya iliyowasajili katika dirisha dogo akiwamo Bernard Morrison, Obrey Chirwa na wengine, ilijikuta ikishindwa kuonyesha mbwembwe ilizokuwa nazo kabla ya mchezo huo kwa kuburuzwa katika dakika zote 90 za pambano hilo.
Matokeo ya mchezo huo ni kama salamu kwa timu nyingine zitakazokutana na Yanga kwa namna ilivyo na uwezo mkubwa wa kufunga mabao, kwani katika mechi saba zilizopita sasa imefunga jumla ya mabao 28-3.
Yanga ilionyesha kwamba kazi ya kukusanya pointi tatu imeisha mapema baada ya kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.
Katika mabao hayo, dakika sita za kwanza Yanga ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Prince Dube (dk 2) na Clement Mzize (dk 6) huku mpishi wao akiwa Stephane Aziz Ki aliyetoa asisti zote mbili za kwanza na hivyo kufikisha asisti saba akibakisha moja tu kuifikia rekodi yake binafsi ya msimu uliopita aliofikisha asisti nane.
KenGold iliyofanya usajili wa wachezaji 24 katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15, 2025 na kuwaacha wengine 11, ilionekana kuwa haijatulia na kujikuta ikifanya makosa mengi.
Katika dakika ya 38, Pacome Zouzoua aliifungia Yanga bao la tatu baada ya kumpiga chenga kipa Castor Mhagama akimalizia pasi ya Dube kisha Mzize akaongeza la nne katika dakika ya 42 akitumia makosa ya kipa huyo kushindwa kudaka krosi iliyopigwa na Chadrack Boka.
Kipindi cha pili kilianza kwa Dube kufunga bao la tano la timu hiyo akimalizia krosi ya beki Chadrack Boka sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi hicho. Dube alifunga kwa kichwa likiwa bao la saba kwake kabla ya makocha wa timu zote kufanya mabadiliko ya wachezaji na kuongeza kasi ya mchezo.
Duke Abuya aliyetokea benchini aliiandikia Yanga bao la sita katika dakika ya 85 na dakika moja baadaye wakati wa kuanzishwa kwa mchezo huo baada ya bao hilo na mtokea benchini Seleman Bwenzi wa KenGold alifunga bao la ajabu lililokuwa gumzo uwanjani.
Bwenzi alianzisha mchezo huo kwa kupiga moja kwa moja mpira mrefu uliomshinda kipa Diarra Djigui aliyekuwa kasogea mbele kidogo na lango na kujikuta akiuzamisha mpira huo nyavuni mwake.
Bao hilo lililokuwa la kushtukiza lilimtibua Diarra aliyekuwa akimfukuzia kipa wa Simba, Moussa Camara katika clean sheet, kwani imemfanya asaliwe na nane tu, wakati mwenzie anazo 13.
Imeshuhudiwa katika mchezo huo mabenchi yote ya ufundi yakiwa hayana makocha wakuu kitu ambacho ni mara ya kwanza kutokea katika ligi msimu huu ambapo wamelazimika kukaa jukwaani.
Yanga ambayo siku moja kabla ya mchezo huu ilitangaza kufikia makubaliano ya kuachana na kocha Sead Ramovic huku ikimtambulisha Hamdi Miloud, kikosi chao kimeongozwa na Abdihamid Moallin ambaye wakati anatua Yanga Novemba 18, 2024 alitambulishwa kama mkurugenzi wa ufundi.
KenGold ambayo kocha wake mkuu ni Mserbia, Vladislav Heric, kikosi chao kimeongozwa na kocha msaidizi Omary Kapilima huku ikielezwa mkuu wake amekosa vibali.
YANGA KILELENI, MZIZE KATISHA
Ushindi huo umeifanya Yanga kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, angalau kwa saa 24, ikifikisha pointi 45 baada ya kucheza mechi 17 huku KenGold ikibaki na pointi sita ikiburuza mkia. Simba yenye pointi 43 inacheza mechi yake ya mkononi Alhamisi dhidi ya Fountain Gate na endapo itashinda itarejea kileleni.
Wakati Yanga ikiwa kileleni, Mzize amefikisha mabao tisa na kuongoza chati ya ufungaji akimzidi Elvis Rupia wa Singida Black Stars mwenye manane.
Pacome naye amefikisha mabao saba kama ilivyo kwa Prince Dube na nyota wawili wa Simba, Jean Charles Ahoua na Lionel Ateba.
Katika mechi ya mapema Tabora United ilishinda 2-1 dhidi ya Namungo.
Yanga: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Ibrahim Hamad, Dickson Job, Khalid Aucho, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Prince Dube na Aziz Ki.
KenGold: Castor Mhagama, Tungu Robert, Bilali Abdi, Ambokise Mwaipopo, Komanje Sandale, Masoud Abdallah, James Msuva, Zawadi Mauya, Emmanuel Mpuka, Gradi Lassa na Herbet Lukindo.