Rais Samia: Hatupaswi kubweteka, kuwadharau wapinzani

Dar/Dodoma. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, amesema pamoja na ukubwa wa chama hicho na matumaini ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, wanachama hawapaswi kubweteka.

Si kubweteka pekee, amesema kuwa ukubwa wa chama hicho haupaswi kuwafanya wanachama wake wawe na kiburi cha kuwadharau wapinzani, wala kuingiwa na hofu ya kuwaogopa.

Kauli hiyo ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia, inapigia msumari hoja iliyotolewa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Januari 18, 2025, katika mkutano mkuu wa chama hicho jijini Dodoma aliposema pamoja na ukubwa na nguvu iliyonayo CCM, hakipaswi kujiamini kupita kiasi na kubweteka, bali ni muhimu kijipange kwa ushindani dhidi ya vyama vingine.

Hata hivyo, hoja ya Rais Samia kuhusu kutowadharau wapinzani inakuja wakati ambapo vyama vya upinzani vipo katika hatua mbalimbali za kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu wa wabunge, madiwani na Rais, Oktoba 2025.

Mathalani, ACT-Wazalendo tayari mgombea wake wa urais kwa upande wa Zanzibar, Masoud Othman, alishatia nia, na kwa upande wa Bara, Dorothy Semu ameshajitokeza kuomba ridhaa.

Kwa upande wa Chadema, mbali na kujihuisha kwa kuwa na sekretarieti mpya, chama hicho kilikuwa mafichoni Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, kwa kikao cha kuweka sawa mambo yake kuelekea uchaguzi huo.

Ingawa Chadema kilishatangaza shinikizo la kutofanyika kwa uchaguzi iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya kisera na kisheria kuhusu uchaguzi huo, hakijafunga pazia la wagombea kujitokeza kutia nia.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia, amesema hayo leo, Jumatano, Februari 5, 2025, alipohutubia wanachama wa CCM katika hafla ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho, yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

CCM ilizaliwa Februari 5, 1977, baada ya Chama cha ASP visiwani Zanzibar na Tanu cha Tanganyika kuungana.

Maadhimisho hayo yalitumika kumtambulisha Rais Samia kama mgombea urais wa CCM kwa Tanzania, Dk Hussein Mwinyi kama mgombea urais wa Zanzibar, na Dk Emmanuel Nchimbi kama mgombea mwenza wa Samia.

Tusibweteke, tusidharau wapinzani

“Pamoja na hali hiyo, tusibweteke. Ndugu zangu, pamoja na hali hiyo ya kujiamini na kwamba CCM ndicho chama kikubwa na tuna matumaini makubwa kwenye uchaguzi ujao, tusibweteke,” ameeleza.

Kwa kuwa chama hicho kinatimiza miaka 48 katika mwaka wenye vuguvugu la uchaguzi, amesema hawapaswi kuruhusu kunyemelewa na kiburi cha kuwadharau wapinzani, kadhalika wasiingiwe na hofu ya kuwaogopa.

Amesema chama hicho kinapaswa kuendelea kulinda heshima na thamani waliyopewa na wananchi ya kuwaongoza na kuonyesha uthabiti kwa ustawi wa wananchi.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, demografia ya nchi na mabadiliko ya teknolojia yanaonyesha kukubalika kwa CCM, na hatima ya kesho yake itategemea si tu ilichowahi kukifanya zamani, bali inachokifanya leo.

“Japo historia yetu ina nafasi kubwa sana, lakini haitakuwa kete peke yake ya kutufanya tuendelee kuchaguliwa. Huko tuendako, inatupasa kujipanga kupimwa kwa sera, mipango na kazi nzuri tunazozifanya na namna tunavyoleta matumaini kwa wananchi,” amesema.

Amesema mwelekeo wa chama hicho utategemea na uwezo wake wa kubaini changamoto mpya na kunyumbulika katika kuzitatua.

Maelezo yake yalitanguliwa na ufafanuzi kuwa CCM imeendelea kuwa na msingi wa amani na mshikamano, hali iliyokifanya kiendelee kuaminiwa na kutumainiwa ndani na nje ya nchi.

Kupitia imani kuwa binadamu wote ni ndugu na Afrika ni moja, amesema CCM imeendelea kuwa tumaini kwa Waafrika wote na kwamba haitabadili itikadi hiyo ya kuwatumikia watu wote.

“Kuaminika kwa CCM hakujatokea tu, bali ni jitihada za kushughulikia matatizo ya wananchi zilizowekwa katika Ilani zake za Uchaguzi,” amesema.

Rais Samia amesema chama hicho kimekuwa kikitekeleza ahadi zake na wakati mwingine katika mazingira magumu, vikiwemo vita vinavyoendelea.

Kwa kuwa CCM inatekeleza ahadi zake, tangu ulipoanza mfumo wa vyama vingi, amesema wananchi wameendelea kukipa imani chama hicho kuiongoza nchi.

Ameeleza kuwa kwa kazi zilizofanywa, hana shaka chama hicho kitaendelea kuaminiwa na kupewa nafasi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa upande wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Zanzibar, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, amesema mafanikio ya CCM tangu kuasisiwa kwake ni kielelezo muhimu cha kujipambanua kwa vyama vingine vya siasa vya ndani na nje ya nchi.

“CCM imeonyesha ukomavu wa kiuongozi na demokrasia. Ni dhahiri wote tunawajibu wa kudumisha mafanikio yetu kwa kuimarisha umoja na mshikamano, ambayo ni misingi mikuu ya mafanikio tunayopata,” amesema.

Dk Mwinyi amesema kwa kuzingatia kuwa wanakabiliwa na uchaguzi wa dola baadaye mwaka huu, wanachama wa chama hicho hawana budi kuendelea kudumisha misingi hiyo ili kukiimarisha chama hicho kiweze kushika dola pande zote za Tanganyika na Zanzibar.

“Ili kufanikisha azma hii, tunao wajibu wa kuhakikisha wanachama wetu wanajiandikisha katika daftari la wapigakura na wakati ukifika wahakikishe wanakwenda kukipigia kura chama chetu,” amesema.

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25 kwa pande zote mbili ni dhamana tosha ya kuwafanya Watanzania kuendelea kukiamini na kukichagua chama hicho kiendelee kuongoza nchi.

“Nitoe wito kwa wana-CCM, kila mmoja kwa nafasi yake kuyatangaza mafanikio na kuwashawishi Watanzania wote kuendelea kukiunga mkono chama chetu ili nchi yetu ipige hatua kimaendeleo,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, amesema chama hicho kiliasisiwa katika Uwanja wa Amani, Visiwani Zanzibar, mwaka 1977, baada ya kuungana kwa vyama viwili—Tanu na ASP—vilivyofanya kazi kubwa kufikia demokrasia ya kweli.

“Baada ya kazi nzuri tangu mwaka 1961, 1964 hadi 1977, vyama hivi viliona havina sababu ya kuwa na vyama viwili, ila tuwe na chama kimoja kitakacholiunganisha Taifa nzima,” amesema.

Dk Nchimbi, ambaye ni mgombea mwenza wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao mwaka huu, amesema kwa utaratibu wa kawaida wa chama hicho, Halmashauri Kuu ya CCM iliamua sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwake zifanyike kila baada ya miaka mitano kwa ngazi ya kitaifa.

“Sherehe hizi zilitakiwa zifanyike mwaka 2027, lakini Kamati Kuu, baada ya kupokea maombi kutoka kote nchini ikieleza uzito wa mwaka huu na kazi zilizofanywa na Serikali ya CCM, iliridhia zifanyike mwaka huu,” amesema.

Amesema kaulimbiu za maadhimisho hayo ni ‘Shiriki uchaguzi kwa uadilifu na kazi iendelee’, na mkutano mkuu wa chama hicho, chini ya Mwenyekiti wake na Rais Samia, ulisisitiza: Uchaguzi wa uadilifu.

“Kwa kweli, tungependa wana-CCM wote watuelewe tukisema hivyo. Mwenyekiti anamaanisha, Kamati Kuu inamaanisha na Halmashauri Kuu ya Taifa inamaanisha tunataka chama kisafi ambacho kiko tayari kuwatumikia wananchi,” amesema.

Balozi Nchimbi, katika maelezo yake, amesema sherehe hizo zilizinduliwa Januari 28, mwaka huu, na kufanyika katika mikoa mbalimbali, huku kilele chake kikihitimishwa jijini Dodoma. Sherehe hizo zilitanguliwa na shughuli mbalimbali zilizofanywa na jumuiya za chama hicho, ikiwemo marathoni, kongamano na mafunzo.

Amesema wanaposherehekea miaka hiyo, wanaangalia nguvu ya chama chao, ambazo hupimwa kwa kuangalia idadi ya wanachama wake, kujipanga safu za uongozi wake, na alama muhimu za chama hicho.

“Wakati CCM kinaanzishwa, kilikuwa na jumla ya matawi 6,424. Leo tunavyoongea, kina matawi 23,430. Na wakati vyama vinaungana, vilikuwa na wanachama 103,923. Leo CCM kina jumla ya wanachama milioni 12.2,” amesema.

Imeandikwa na Juma Issihaka, Tuzo Mapunda (Dar), na Habel Chidawali (Dodoma).

Related Posts