Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kufuatia kifo cha Mtukufu Aga Khan, kiongozi wa madhehebu ya Ismailia duniani.
Mtukufu Aga Khan anayefahamika kama Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, alifariki dunia jana Jumanne Februari 4, 2025, jiji Lisbon, Ureno akiwa na umri wa miaka 88. Alifariki akiwa amezungukwa na familia yake.
Akitoa salamu hizo leo Jumatano Februari 5, 2025, Rais Samia ameandika: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwana Mfalme Karim Al-Husseini, Aga Khan IV, kiongozi mkuu wa kiroho wa dhehebu la Kiislamu la Ismailia ulimwenguni na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan.
Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa salamu za pole kwa familia ya mwana mfalme Aga Khan, Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan na Jumuiya ya Waislamu wa Ismailia.
“Tunaungana nanyi kuomboleza kuondokewa na kiongozi mkubwa na mwenye maono, ambaye kazi yake imegusa maisha ya mamilioni ya watu duniani,” ameandika Rais Samia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Mbali na Rais Samia, Rais wa Kenya, Dk William Ruto naye ametoa salamu za pole kufuatia kifo hicho.
Dk Ruto ameandika kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) kuwa: “Dunia imempoteza kiongozi mkubwa ambaye alienda mbali kwa kufanya yaliyodhaniwa kuwa hayawezekani, aliyafanya kwa kusaidia jamii iliyokuwa hatarini, kupitia shughuli za kujitolea na misaada kupitia ujenzi wa shule na hospitali.
“Tumesikitishwa sana na kifo cha Mtukufu Aga Khan, kiongozi wa kiroho wa Waislamu wa Ismailia… Tuko pamoja na familia ya Mtukufu na jamii pana ya madhehebu ya Ismailia.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres ameeleza kumkumbuka Mwana Mfalme, Karim Al-Hussaini (Aga Khan IV) kama kiongozi wa kiroho ulimwenguni na mhamasishaji wa amani, maendeleo na mshikamano.
“Kwa miongo kadhaa Aga Khan amekuwa akijitoa kuboresha ustawi wa maisha ya watu duniani, hususan walioko hatarini kukosa huduma za kibinadamu kwa kusaidia upatikanaji wa elimu na misaada ya kiutamaduni,” amesema Guterres kupitia msemaji wa UN, Stéphane Dujarric.
“Uongozi wa Taasisi ya Aga Khan ulienda mbali zaidi ya imani ya madhehebu ya Shia Ismailia, ukisema Mtukufu Aga Khan alikuwa daraja la kutuelimisha kati ya utamaduni na maendeleo ya dunia. Jitihada zake za kupambana na umaskini, kuleta usawa wa kijinsia na kuchochea maendeleo endelevu ni miongoni mwa alama alizotuachia,” ameongeza.
Guterres amesema UN, inamtambua na itamkumbuka Aga Khan kwa mchango wake kwenye kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s) na ushirikiano wake na UN katika kufikia malengo hayo.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amesema Mtukufu Aga Khan alijitoa kutumia maisha yake kuleta amani na upendo kwa watu wote.
Trudeau amesema kiongozi huyo alifanya kazi katika mabara yote kutatua changamoto za kibinadamu, ukiwemo umaskini, elimu na usawa wa kijinsia.
Pia amesema alikuwa mtu wa imani na upendo na atamkumbukwa kupitia maisha ya watu aliowagusa.
“Kufuatia kifo hiki, familia yangu na jamii ya Canada, tunatoa salamu za pole kwa familia ya Mwana Mfamle Aga Khan, marafiki zake na Jumuiya ya waumini wa mahehebu ya Shia Ismailia nchini Canada na duniani kwa ujumla.”
Mtukufu Aga Khan ni mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan
(AKDN) ambao umeleta tija maeneo mbalimbali, hususan katika sekta ya afya, elimu na utamaduni na uwezeshaji kiuchumi maeneo ya vijijini nchini Tanzania na Kenya.
Uwepo wa Aga Khan nchini Tanzania unaonekana kupitia uanzishwaji wa kampuni mbalimbali ikiwemo ya
Limited (MCL) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, Hospitali za Aga Khan na miradi mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.
Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika.