Sera ya kikanda inayosimamia usalama wa bahari mbioni

Dar es Salaam. Nchi tisa kutoka Bara la Afrika zinatarajiwa kuja na sera ya pamoja ya kikanda ambayo inalenga kusimamia usalama wa uendeshaji vyombo baharini pamoja na ulinzi na usalama wa bandari zinazopatikana katika nchi hizo.

Hili linafanyika ili kuboresha ufanisi wa nchi hizi katika kuhudumia meli nyingi za mizigo na abiria zinazopita katika maeneo yao hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na uharamia wa meli katika baadhi ya maeneo ya Bahari Nyekundu ambayo yamekuwa yakiathiri shughuli za usafirishaji.

Sera hii ambayo inatarajiwa kukamilika mapema mwakani inaandaliwa kupitia program ya Port Security and Safety of Navigation (Usalama wa Bandari na Usalama katika uongozaji vyombo majini) katika nchi za Afrika ya Mashariki, Kusini mwa Afrika na Bandari ya Hindi (EA-SA-IO) ambapo ndani yake ipo Tanzania, Angola, Comoro, Kenya, Madagascar, Mauritius, Mozambique, Namibia na Seychelles.

Akizungumza katika mkutano huo, leo Jumatano, Februari 5, 2025, Ofisa msimamizi kutoka Indian Ocean Commision (OIC), Raj Mohabeer amesema upo umuhimu kwa nchi katika ukanda huu kushirikiana kwani kuimarisha usalama katika nchi moja kunaweza kusababisha meli nyingi kuwa na uelekeo katika bandari chache.

“Hivyo tunalenga kutengeneza sera ya kikanda kuhusu usalama wa bandari na usalama wa baharini, kuhakikisha kunakuwa na usawa katika hili kwa mataifa yote linapokuja suala la utoaji wa huduma,” amesema.

Amesema hili linafanyika kwa sababu moja ya changamoto inazokabili nchi hizo ni usalama wa bandari jambo ambalo linafanya jumuiya za kimataifa kuona bandari si salama kwa sababu ya kutofuata ipasavyo kanuni za kimataifa kama vile Kanuni za ISPS, SOLAS na mikataba mingineyo.

Mkurugenzi wa Usalama wa Usafiri na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi, Stella Katondo amesema umuhimu wa sera hiyo ni kufanya kuwapo kwa usafirishaji salama na endelevu katika ukanda wa nchi wanufaika.

“Baharini ni muhimu kwa sababu ndiyo namna rahisi katika usafirishaji mizigo duniani kote lakini kila nchi ikiwa na viwango vyake inachelewesha kufikia malengo kusudiwa kama kanda,” amesema Stella ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara.

Amesema jambo hilo ndiyo linafanya kuwapo kwa uhitaji wa sera ya kanda huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoitamani zaidi kwa sababu itaweka viwango sawa vya ulinzi na usalama vya usafirishaji baharini pamoja na ulinzi na usalama wa bandari katika ukanda mzima.

“Kunapowekwa sera ya pamoja itasaidia kuwapo kwa viwango sawa katika masuala ya usalama, hili itafanya wote wanaotumia eneo hili kujua usalama ulivyo, kuwa na uhakika wa kiwango cha ukaguzi kinachokuwapo hivyo kufanya hata mlaji wa mwisho anakuwa na uhakika wa kupata kitu kwa gharama nafuu,” amesema Stella.

Mkurugenzi wa Shirika la Usafirishaji Majini (Tasac), Mohamed Salum amesema kwa sasa Bara la Afrika hili linapitisha meli nyingi kufuatia mapigano katika Bahari Nyekundu hali inayofanya bidhaa zinazokwenda nchi za magharibi kubadilisha njia.

Hiyo inafanya sasa meli zinapotoka nchi za Asia kupitia njia ya Afrika kusini ili ziweze kwenda Ulaya jambo ambalo linaweka ulazima kwa nchi hizo kuboresha usalama.

“Kunakuwa na suala la usalama wa vyombo ambapo tunaangalia namna ya kudhibiti uharamia wa meli, pia tunaangalia vyombo vinavyobeba bidhaa ni salama kiasi gani na si kusafirisha binadamu au dawa za kulevya, wanyama au kuvua kinyume na sheria. Lakini tunataka kuhakikisha tunasimamia uongozaji wa meli unapokatisha katika eneo lako,” amesema.

Mradi huu wa usalama wa bandari ulianza kutekelezwa mwaka 2019 na unatarajiwa kufikia tamati mwaka 2026.

Related Posts