Serikali haijatoa mwongozo posho za watumishi walio pembezoni

Dodoma. Serikali imesema haijatoa mwongozo mahususi wa kulipa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa kada ya walimu na watumishi wengine wanaopangiwa vituo vya kazi katika mikoa ya pembezoni kutokana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wake.

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Sangu ameyasema hayo leo Februari 5, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Muleba (CCM), Oscar Kikoyo.

Mbunge huyo amehoji Kusini(CCM), Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia posho ya mazingira magumu wafanyakazi hasa walimu wanaopangiwa kazi Mikoa ya pembezoni.

Akijibu swali hilo, Sangu amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za kuishi watumishi wa umma hususan, walimu na watumishi wa kada za afya katika mamlaka za Serikali za mitaa, kujenga na au kukarabati miundombinu ya barabara; kuboresha huduma za jamii kama vile, elimu, afya, maji, nishati ya umeme na mawasiliano ya simu.

Aidha, Sangu amesema huduma hizo zinawanufaisha watumishi wa umma wote pamoja wakiwemo wanaofanya kazi katika mikoa ya pembezoni.

“Hata hivyo, Serikali haijatoa mwongozo mahususi wa kulipa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa Kada ya walimu na watumishi wengine wanaopangiwa vituo vya kazi katika mikoa ya pembezoni kutokana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wake,” amesema. 

Related Posts