Siasa zinavyochangia Sheria ya Barabara kuvunjwa-2

Dar es Salaam. Licha ya Sheria ya Barabara kuzuia shughuli zozote za biashara, ikiwemo zinazohusisha moto, kufanyika kwenye hifadhi za barabara, utekelezaji wa katazo hilo unaonekana mgumu nchini hususan jijini Dar es Salaam.

Kifungu cha 51 cha Sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2007 m,bali na kuzuia kuwasha au kuanzisha moto barabarani bila ruhusa ya mamlaka, pia kinaeleza ni kosa kufanya biashara au shughuli zozote zinazoweza kusababisha msongamano au kuzuia barabara kupitika kwa urahisi. 

Kwa mujibu wa sheria hiyo, atakayebainika kufanya kosa hilo adhabu yake ni kifungo mwaka mmoja au faini isiyopungua Sh300,000 au vyote kwa pamoja.

Hata hivyo, hakuna rekodi ya kuwepo mtu yeyote aliyechukuliwa hatua kwa sababu ya kosa hilo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam umebaini kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria hiyo huku mamlaka zikishindwa kuchukua hatua kwa wanaovunja sheria hiyo.

Katika toleo la jana Jumatatu, Februari 3, 2025 tuliangazia sheria hiyo inavyovunjwa na jinsi mamlaka, mathalan Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linavyopambana na hali hiyo.

Katika maeneo 10 yaliyotembelewa ya Buguruni, Mbezi, Tegeta, Gongo la Mboto, Mbagala, Tandika na Kongowe Mwananchi ilishuhudia wachuuzi wakifanya biashara ya vyakula kwenye hifadhi ya barabara ambayo inahusisha matumizi ya moto katika maandalizi yake.

Eneo la Buguruni, pembeni mwa barabara inayoelekea kwa Mnyamani, inapofika jioni kuanzia saa 12 jioni wafanyabiashara wanaanza kuandaa majiko kwa ajili ya kukaanfa chipsi, nyama za kukun na vyakula vingine.

Katika eneo lenye urefu wa mita kati ya 50 hadi 70 kuna majiko 15 yenye moto mkali yaliyobeba makarai ya mafuta yanayokaanga chipsi na kuku. 

Moto kutawala katika eneo hilo haina maana shughuli nyingine zinasimama, vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara hutembea kwa tahadhari kuukwepa moto huo.

Akizungumza na Mwananchi mfanyabiashara wa matunda katika eneo hilo, Rashid Lazaro amesema mara kadhaa kumekuwa na kukwaruzana kwa pikipiki na magari kwa sababu ya kukwepa majiko yaliyojipanga barabarani. 

“Yaani hapo unaona barabara ni nyembamba halafu huku pembeni ndiyo kama hivyo, majiko ya moto yamejipanga, sasa ikitokea magari hayatembei kwa sababu ya foleni, hutokea mikwaruzano ya hapa na pale kati ya magari, bodaboda na bajaj.

“Kinachotokea ni kwamba kwa sababu barabara ni finyu magari yanafunga pande zote mbili, na kama tunavyofahamu bodaboda huwa hawana muda wa kusubiri watapenyapenya matokeo yake wanatokea kwenye majiko ili kuyakwepa wanarudi kukwanguana na magari na bajaj,” alisema Lazaro. 

Maulid Mbonde ambaye ni mmoja wa wenyeji wa Buguruni, amesema awali barabara hiyo haikuwa na biashara kama ilivyo sasa, shughuli hizo zilianza taratibu takribani miaka 10 iliyopita na wafanyabiashara walinza kusogea kidogo kidogo.

“Hapa hapakuwa na vurugu kama ilivyo sasa, wafanyabiashara walianza kidogo kidogo lakini imekuwa msaada kwa wakazi wa Buguruni, ukitoka zako huko unapitia hapa kuchukua kitoweo. Kadiri siku zinavyozidi kwenda inakuwa kero, huwezi hata kumtuma mtoto, maana msongamano wa magari, bodaboda na hayo majiko ya moto vinatishia usalama,” amesema Mbonde. 

Hali kama hiyo inaonekana katika eneo la Gongo la Mboto, kuna msongamano wa watu na magari na kwa kuwa barabara hiyo inajengwa njia za mwendo wa haraka, eneo linazidi kuwa finyu.

Lakini kwa wauza kuku na wachoma nyama, biashara yao inaendelea kama kawaida, wakiwasha moto wa gesi na mkaa bila kujali msongamano iliopo.

Hali hii inaonekana pia Mbagala Rangi Tatu ambapo kutokana na Barabara ya Kilwa na miundombinu ya mabasi ya mwendo kasi, wachuuzi wamejibana kwenye kituo cha daladala na kusababisha mwingiliano mkubwa kati yao na abiria.

Kwenye sehemu ndogo ambayo imebaki kama hifadhi ya barabara wachuuzi hao wametafuta namna ya kujipachika na kuendelea na shughuli za kuandaa vyakula wanavyouza kwa abiria na wapitia njia. 

Erick Daniel anayeuza kuku wa kukaanga eneo la Gongo la Mboto, amesema hakuna mamlaka iliyowahi kuwazuia kuwasha moto eneo hilo. 

“Haya maeneo tunakodishwa na watu binafsi na huwa tunatoa ushuru wa usafi wa Sh200 hadi Sh500, lakini hakuna anayezuia kuwasha moto,” amesema.

Naye Rashid Abdallah ambaye pia anafanya shughuli zake Gongo la Mboto alipoulizwa kuhusu matumizi ya moto barabarani amesema: “Hapa biashara yetu ni lazima kuwasha moto, kwa sababu wateja wanataka nyama ya moto huwezi kuandaa nyama nyumbani kwako halafu uje kuiza hapa, watu wanataka kile kinachotoka jikoni.”

Wakili Bashiru Yakub amesema kinachosababisha sheria hiyo isitekelezeke ni mchangamano kati ya sheria na masuala ya kisiasa, hali inayosababisha watendaji na watalaamu washindwe kutekeleza majukumu yao. 

“Hiyo sheria ipo lakini inavunjwa na huwezi kuwalaumu wananchi kwa sababu siasa inachukua nafasi kubwa, hivyo lawama zinapaswa kwenda kwa mamlaka kwa sababu wao ndiyo wasimamizi wa barabara. 

“Kilichopo ni kwamba sheria za aina hii utekelezaji wake ni mgumu kwa sababu wanasiasa wanataka kuonyesha wema wao kwa wananchi, hii inasababisha watendaji washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Inawezekana kabisa Tanroads wakawa na nia njema ya kuweka barabara zao vizuri. lakini pale kuna wafanyabiashara ambao ndiyo wapiga kura na wanasiasa wanaona huo ndiyo mtaji wao,” amesema Yakub.

Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa Gongo la Mboto, Said Chanzi amesema: “Kama moto una shida kwa magari na wapita njia, trafiki wako pale, mbona hawajawahi kuwaondoa? Hakuwezi kuwa na mlipuko pale. 

“Kama kungekuwa na shida, kuna viongozi wakubwa wanapita ile njia wangeshaiona. Sisi tulichoambiwa ni kwamba wafanyabiashara watapangwa na walishapangwa. Sasa uje uwaondoe wale watu pale ambao ni wapigakura wa CCM uwapeleke wapi na uchaguzi unakuja, wale watu wanatafuta maisha, wanasomesha, unapowaondoa utaonekana kiongozi wa aina gani?” 

Hoja hiyo imeungwa mkono na mmoja wa watumishi wa Manispaa ya Temeke ambaye hakutaka jina lake liandikwe kuwa kinachokwamisha kuwaondoa wafanyabiashara hao ni siasa, wanasiasa wanashindwa kufanya uamuzi kwa kuhofia kupoteza wapigakura. 

“Si kwamba haifahamiki kwamba kufanya shughuli yoyote kwenye hifadhi ya barabara ni kosa, inafahamika vizuri tu lakini pale watalaamu wanapojaribu kuchukua hatua au kushauri nini kifanyike, wanasiasa wanaingilia kati kwa kuhofia kitakachotokea kwa wapigakura wao.

Kwa ninavyofahamu masuala ya kitaalamu hayapaswi kuingiliwa na siasa lakini wakati mwingine tunalazimika kuacha mambo yafanyike kisiasa, ilimradi tunahakikisha tunatoe elimu kupunguza uwezekano wa kutokea madhara,” amesema.

Hata hivyo, Chanzi amesema kutokana na matengenezo yanayoendelea katika barabara hiyo, wanahitaji kuwapanga tena ili wakae katika mpangilio unaoeleweka.

“Ni kweli kwamba kuna changamoto ya maeneo ya kufanyia biashara, ndio maana Serikali imesema itajenga soko kubwa na ramani imeshachorwa, mchanga umechukuliwa kwenda kupimwa, hivyo tunatarajia wafanyabisahara watapata nafasi ya kutosha.” 

Akizungumzia hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo amekiri kutambua uwepo wa watu wanaovamia barabara na kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo zinazohusisha moto, jambo ambalo amesema ni kosa kisheria.

“Hakuna kibali ambacho kimewahi kutolewa, hawa hawatakiwi kuwepo kwenye maeneo ya barabara na ndiyo maana tumeanza zoezi la kuwatoa vinapita vikosi vyetu kwenye barabara mbalimbali kuwatoa na sio hao wanaotumia moto pekee, bali na wengine wengi wanaovamia barabara. 

“Pia tunatoa elimu wajue na kuheshimu matumizi ya hifadhi za barabara. Hili suala ni mtambuka, jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha barabara zinakuwa salama,” amesema Mkumbo.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, Godfrey Mkinga amesema kama sheria inavyoelekeza hakuna kibali kilichotolewa kwa ajili ya kuwasha moto na kupika barabarani isipokuwa wanatambua kuwa ipo mitaa ambayo watu hufanya biashara usiku. 

“Hatutoi vibali vya kuwasha moto kwenye barabara, ila kuna mitaa inayoruhusu watu kufanya biashara usiku na huko haturuhusu moto uwekwe kwenye lami, lazima uwe pembeni.

“Kama kuna wanaofanya barabarani tutafuatilia maana hairuhusiwi kuweka jiko kwenye barabara kwa sababu kwa asili lami haitaki moto, ikishika moto kuna uwezekano wa kuwaka na kusababisha mlipuko utakaoleta madhara,” amesema. 

Mbali na hilo, Mkinga amesema uwepo wa biashara barabarani unaweza kusababisha madhara kwa watumiaji wa barabara hizo, ikiwemo uwezekano wa magari kukosea njia na kuwasomba watu. 

Amesema mara kadhaa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na halmashauri wamekuwa wakifanya operesheni za kuwaondoa wafanyabiashara wanaovamia hifadhi za barabara na kama kuna waliorejea watafanya tena operesheni hiyo.

“Hili suala linahitaji ushirikiano wa jamii nzima, tunaweza kuwa tunatoea elimu na kufanya ufuatiliaji lakini ni vigumu kufika maeneo yote, ndiyo maana tunaomba na vyombo vya habari mtusaidie kutoe elimu, hao wafanyabiashara na wanunuzi wajue ni hatari kwa biashara kufanyika barabarani,” amesema. 

Amesema katika mpango wa elimu kwa umma wanaendesha kampeni ya ‘Safisha Pendezesha Jiji la Dar es Salaam’ ambayo inalenga kulipa jiji hilo taswira nzuri ikiwemo kuwaweka wafanyabiashara katika maeneo wanayopangiwa na kuziacha wazi barabara.

Related Posts