Dar es Salaam. Wanafunzi 36 waliofeli kidato cha pili mwaka 2024 katika Shule ya Sekondari King’ongo, jijini Dar es Salaam, Wilaya ya Ubungo, wamejikuta wakishindwa kuingia darasani kusoma kwa takribani siku 22.
Hatua hiyo imetokana na kile kinachodaiwa, mkuu wa shule hiyo alitaka wakarudie darasa hilo katika shule nyingine na si King’ongo kama ilivyopaswa kuwa.
Hata hivyo, tayari wanafunzi hao wamesharejea shuleni hapo kuendelea na masomo, baada ya Diwani wa eneo hilo, Edward Laizer pamoja na uongozi wa serikali za mitaa kuingilia kati.
Januari 4, 2025, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) ilitangaza matokeo ya kidato cha pili ambapo kwenye shule hiyo ya King’ongo wanafunzi 36, kati yao 21 wavulana na 15 wasichana walipata sifuri.
Daraja la kwanza walikuwa saba. Daraja la pili 18, Daraja la tatu ni 45 na daraja la nne 217.
Tangu shule zilipofunguliwa Januari 13 hadi Jumanne Februari 4 ni siku 22 ambazo wanafunzi hao walikuwa wakisotea kurejea masomoni.
Mzizi wa yote hayo ni uamuzi wa mkuu wa shule anayedaiwa kuwakataa wanafunzi hao 36 waliopata sifuri katika mtihani wa kidato cha pili, wasirudie darasa shuleni hapo.
Badala yake, aliwaandikia barua kila mmoja ya kuhamia katika Shule ya Sekondari Saranga kwa ajili ya kurudia darasa hilo (nakala ya barua hiyo Mwananchi limeiona).
Kwa mujibu wa wazazi wa wanafunzi hao, hatua hiyo iliwafanya waandamane hadi ofisi ya serikali za mtaa wa King’ongo kushinikiza watoto wao waendelee na masomo King’ongo.
Akizungumza na Mwananchi mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Jesca Macha amesema alishangaa kuona siku kuona mtoto wake akirudi shule mapema siku ambayo shule zimefunguliwa Januari 13, 2025 na kumwambia anatakiwa kuhama shule hiyo na kwenda kurudia katika shule nyingine.
Macha anasema baada ya kupewa ujumbe huo kesho yake alifika shule na kuonana na mkuu wa dhule hiyo na kumueleza anatakiwa kumuhamisha mtoto wake akasome katika shule ya Sekondari Saranga.
“Nilikwenda mara kadhaa kumuomba mkuu wa shule mtoto wangu aendelee kusoma katika shule hiyo bila ya mafanikio na kila mtoto alipokwenda shuleni kwa ajili ya kusoma alifukuzwa,” ameeleza.
Kwa upande wake, Emmanuel Payovela ambaye pia ni mmoja kati ya wazazi hao, amesema baada ya kwenda kuongea mara kadhaa bila ya mafanikio Januri 30, 2025 alipokea barua kutoka kwa mkuu huyo wa shule ikimtaka kumuhamishia mtoto wake katika shule ya Sekondari Saranga.
“Nilifikisha barua katika shule husika lakini mkuu wa shule hiyo alinirudisha na kunieleza kuwa mtoto wangu anatakiwa kurudia katika shule ileile aliyosoma awali na kufanya mitihani yake,” anaeleza.
Anaongeza baada ya kuona muda unazidi kwenda, aliamua kuungana na wazazi wengine wenye changamoto hiyo kufikisha suala hilo katika uongozi wa mtaa na ofisi ya diwani ili kupatiwa utatuzi.
Hatua hiyo ilifanya uongozi wa mtaa pamoja na diwani wa eneo hilo, Edward Laizer kufika katika shule hiyo na kuitisha kikao cha dharura kati ya walimu na wazazi ambao watoto wao walipitia katika changamoto hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Februari 3, 2025 Laizer alitaka wanafunzi hao kurejea haraka darasani kuendelea na masomo yao ya kurudia kidato cha pili huku akiwasisitiza wazazi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuwapa mahitaji yote muhimu kwa ajili ya kusoma.
Vilevile alitoa wito kwa wazazi na walimu kuhakikisha wanashirikiana pamoja kutatua vikwazo mbalimbali vilivyosababisha wanafunzi hao kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao.
Jana, Jumanne Februari 4, 2025, akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Shule hiyo, Godfrey Kiligini amesema katika shule hiyo hajawahi kuzuia mwanafunzi yeyote aliyefeli kidato cha pili kuingia darasani.
Kiligini ameeleza kuwa baadhi ya wanafunzi hao walifika shuleni wakiwa hawana mahitaji muhimu kwa ajili ya kusoma ikiwemo madaftari, kalamu na wengine kutokamilika katika upande wa sare za shule.
Amesema changamoto hiyo kwa watoto hao ilijitokeza hata mwaka wa masomo uliopita na kujaribu kuwaita wazazi wao ili kubaini kiini cha tatizo hilo bila ya mafanikio yeyote.
“Kabla ya watoto hao kufeli nimejaribu mara kadhaa kuwaita wazazi wao waje tujadili changamoto za watoto wao bila ya mafanikio, baada ya kuwarejesha ili wakakamilishe mahitaji hayo muhimu ya shule ndio wazazi hao wamejitokeza na kudai nimekataa kuwapokea watoto wao,” amesema.