Bao la dakika za jioni la Jentrix Shikangwa dhidi ya Ceasiaa Queens kwenye Uwanja wa KMC Complex jana lilitosha kuipa Simba Queens ushindi wa bao 1-0 ambao uliifanya iendelee kutamba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake ikifikisha pointi 34.
Shikangwa alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha faulo iliyochongwa na Asha Djafar katika dakika ya kwanza ya nyongeza kati ya sita zilizoamriwa na refa Florentina Zabron na kuipa Simba Queens ushindi huo muhimu dhidi ya Ceasiaa ambayo ilionyesha kiwango bora cha kujilinda kwenye mechi hiyo katika dakika zote 90 za mchezo.
Nafasi nyingi zilipotezwa na washambuliaji wa Simba katika mchezo huo ambao kama wangekuwa makini, timu yao ingeweza kuibuka na ushindi.
Akizungumza baada ya mchezo, kocha wa Simba Queens, Bashir Siagi alisema kuwa amefurahishwa na ushindi ingawa timu yake imepoteza nafasi nyingi leo.
“Nilikuwa na presha kiasi. Wapinzani wetu walikuwa wagumu kwenye ulinzi na ikawa ngumu kwetu kufunga mabao. Walicheza kwa ari ya juu kuhakikisha hawafungwi mabao mengi.
Sasa natakiwa nirekebishe kidogo mbinu mazoezini ili tuweze kulinda uongozi wetu wa ligi,” alisema Siagi.
“Niliangalia uimara wao uko wapi na udhaifu wao uko wapi na tukaufanyia kazi. Naona kuna kuimarika kwa timu. Kuna mapumziko hapa ya mwezi mmoja naamini yatatusaidia sana,” alisema Chobanka.
Katika Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha TFF, Kigamboni, JKT Queens iliibuka na ushindi mnono wa mabao 12-0 mbele ya Mlandizi Queens.
Stumai Abdallah alifunga mabao saba, Winfrida Gerard akipachika matatu na Donisia Minja na Jamila Rajabu kila mmoja alipachika bao moja.
Mabao hayo saba ya Stumai yamefanya awe kinara wa kufumania nyavu kwenye ligi hiyo akifikisha mabao 18 huku nafasi ya pili akiwepo Shikangwa mwenye mabao 17.
Ushindi huo umeifanya JKT Queens izidi kujikita kwenye nafasi ya pili ikifikisha pointi 29
Katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Yanga Princess iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa Queens.
Matokeo hayo yameifanya Yanga Princess kusalia katika nafasi ya tatu ikifikisha pointi 18.