LICHA ya kupeleka ombi la kuvunja mkataba ili aondoke klabuni kwa kilichoelezwa amepata ofa nono kutoka CR Belouizdad ya Algeria, lakini kuna mambo kadhaa nyuma ya pazia katika dili la kocha Sead Ramovic kusepa Yanga ikiwa ni siku 82 tangu alipojiunga nayo Novemba 15, mwaka jana.
Ramovic aliyejiunga na Yanga kutoka TS Galaxy ya Afrika Kusini anakuwa kocha wa pili kuondoka Jangwani baada ya Miguel Gamondi aliyesitishiwa mkataba ndani ya msimu huu na kuridhiwa na Mjerumani huyo ambaye naye amesepa ndani ya muda mfupi.
Mwanaspoti lilishawahi kuweka bayana juu ya mipango ya chini chini waliyokuwa nayo mabosi wa Yanga dhidi ya kocha huyo baada ya timu hiyo kushindwa kuvuka kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, ofa iliyoelezwa ndio imemng’oa Ramovic ghafla kutoka Yanga ni kama kocha huyo amewawahi maosi wake, kwani kuna mambo matano yaliyokuwa yamng’oe kama ilivyokuwa mtangulizi wake, Gamondi.
Hapa chini ni mambo yanayodaiwa yalikuwa yale kichwa cha Ramovic kabla ya dili hilo kutoka CR Belouizdad inayoelezwa itamfanya awe analipwa mshahara mnono wa Dola 40,000 (zaidi ya Sh 101 milioni) tofauti na ule aliokuwa akiupokea Yanga, mbali na yeye kuilipa Yanga fedha za kuvunja mkataba.
Tukio la kwanza ambalo lilianza kumtibulia Ramovic lilijiri pale Algeria ambapo wakati timu yake inajiandaa na kikao cha mwisho kuelekea mechi dhidi ya MC Alger alimuondoa Clatous Chama kwenye kikosi kinachoanza.
Chama aliondolewa baada ya kuchelewa kwenye lifti kwa dakika zisizozidi mbili, basi jamaa akamuondoa kwenye kikosi kinachoanza wakati tayari alishapanga na kikosi kizima kilishajua kwamba kiungo huyo anaanza.
Hatua hiyo iliwakera wachezaji wakiamini Chama alistahili kuanza mechi na si wachezaji tu, bali hata viongozi na baadaye Yanga ikapoteza kwa mabao 2-0.
Yanga haikuwa na imani sana na Ramovic tangu timu hiyo iyumbe kwenye mechi sita za makundi alizoanza kuzitumikia ndani ya klabu hiyo, kocha huyo akipoteza mbili za kwanza, akashinda mbili na sare mbili.
Mechi hizo namna Yanga ilivyoangusha pointi 10 ziliwapa shida mabosi na kuanza kujengea wasiwasi kwenye maisha yake, huku wakiendelea kumuwinda taratibu ambapo ilikuwa inatafutwa sababu tu kumuondoa kwa sababu waliamini ni kama hatoshi sana kuipa makali timu.
Kocha huyo amekaa ndani ya nyumba aliyopewa kwa siku chache, ambapo kila alizokuwa anapelekwa Masaki kule kwa wakubwa alizigomea akisema hazina hadhi na hata alipopewa jukumu la kujitafutia nyumba anayotaka ilikuwa ngumu kupata.
Badala yake akaondoka kwenye nyumba aliyokuwa anakaa na kuhamia hoteli moja kubwa pale Posta ndio aliyokuwa anaishi na familia hilo lilikuwa gumu kwa Yanga kulikubali kutokana na gharama kubwa hatua ambayo ilizidi kuwapa shida mabosi wa klabu hiyo.
MISIMAMO YA KIIMANI VS WADHAMINI
Tangu ametua Yanga Ramovic, hakuwahi kuvaa nguo yenye jina la mdhamini mkuu wa klabu hiyo SportPesa, akidai udhamini huo upo kinyume na Imani yake, ambapo badala yake akiwa mazoezini alikuwa akibandika plasta kwenye eneo la mdhamini.
Kwenye mechi ndio akawa anavalia suti safii lakini ndani yake ilikuwa ni kukwepa kuvaa sare ya mdhamini huyo mkuu, hii ilizidi kumletea shida ndani ya klabu hiyo.
Yanga ilikuwa inataka wachezaji wakae kambini kuanzia siku tatu kabla ya mchezo, lakini Ramovic alikubaliana nalo wakati anafika na baadaye akabadilisha gia angani, akiwapa uchaguzi wachezaji wake kwamba watachagua ni siku ngapi, lakini siku moja kabla ya mchezo lazima kila mchezaji awe kambini.
Hilo liliwatibua sana mabosi wa Yanga wakiona kama jamaa anawachukulia poa,kwenye mambo ambayo wanaku-baliana.