Siri kupungua vifo vitokanavyo na uzazi Tanzania

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali, namna zilivyochangia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80 kutoka 556 mwaka 2016/2017 mpaka kufikia vifo 104 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 100,000.

Dk Mpoki Ulisubisya ndiye alianza kuelezea hatua hizo, akirejea alipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuanzia mwaka 2016.

Dk Ulisubisya ambaye kwa sasa ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alielezea hayo jana Jumanne, Februari 4, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhiwa kwa tuzo ya ‘The Gates Goalkeepers Award’ kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, iliyotokana na mafanikio hayo.

Amesema kabla ya hatua kuanza kuchukuliwa, kulikuwa na vifo vingi vitokanavyo na uzazi nchini vilivyotokea hasa maeneo mengi ya vijijini, kwakuwa baadhi ya wanawake waliishi mbali na vituo vya afya pamoja na vituo vilivyopo kukosa huduma za dharura wakati wa kujifungua.

“Tulitafuta ufadhili ili kuirekebisha hiyo hali, tulijenga vituo zaidi ili kuweka huduma karibu pamoja na kuboresha vituo vya afya vyote kutoa huduma za dharura za upasuaji.  Lakini hicho si peke yake tulifanya ni pamoja na kuongeza rasilimali watu katika huduma,” amesema.

Profesa Ulisubisya amesema Serikali iliajiri watoa huduma wa afya wabobezi kuanzia madaktari, wauguzi na wakunga, wakiwa sambamba na Rais Samia Suluhu Hassan wakati huo akiwa Makamu wa Rais.

“Alipokuwa Rais mwaka 2021 niliona kuna mwelekeo sasa, alishirikisha kumbukumbu mbalimbali na uzoefu wake kuonyesha umuhimu wa kutumia wakunga, wakati huo wakunga waliokuwepo walikuwa wakifanya kazi inavyotakiwa…

“Huduma ya mama na mtoto ilipewa kipaumbele, na baada ya kuweka nguvu zote huko mafanikio yameonekana,” amesema Dk Ulisubisya.

Mkurugenzi wa huduma za mama na mtoto Wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani amesema Tanzania ilihitaji kuwa na utashi wa kisiasa katika hilo Wizara ilianzisha kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama, na waliweza kumpata Rais Samia wakati huo akiwa Makamu wa Rais.

Amesema walianza kampeni hiyo wakiwa sambamba na Rais na aliyekuwa Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu) bajeti na kwa wakati huo amesema bajeti haikuwa nzuri hivyo ilibidi kutafuta zaidi rasilimali fedha.

“Tulipoanza tulikuwa na vifo 556 tualianza katika ngazi za chini, wakati huo masuala ya kisiasa yalikuwa yakiingilia kati lakini tulianza Rais alisimama pamoja na sisi.

“Tualianza katika namna ambayo haikuwa rahisi, na wakati huo Waziri alikuwa muwajibikaji, hii ilisaidia kupunguza vifo vingi vilivyotokana na uzazi kwa asilimia 80,” amesema Dk Makuwani.

Meneja mradi Thamini Uhai na Rais wa Agota, Dk Sunday Dominico amesema usimamizi mkubwa wa taarifa ambazo zilikuwa zikitolewa zilisaidia kwa kiasi kikubwa kujua maeneo yenye changamoto na kuyafanyia kazi.

“Nilikuwa eneo la takwimu nyakati zote tuliulizana na kupeana ushirikiano na hii imesaidia, pia vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa kiasi kikubwa, hii ilitokana na uwekezaji wa vifaa mbalimbali vya huduma ya mama na mtoto.

“Uwekezaji wa vifaa kwa ajili ya matunzo ya watoto wachanga nayo ilisaidia na tulihakikisha upatikanaji wa huduma sahihi. Tumekuwa na miradi mingi kuzuia vifo baada ya uzazi pia,” amesema Dk Dominico.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa AAPH, Dk Mary Mwanyika Sando amesema kutoa dozi ya madini ya calcium imesaidia jitihada hizo na ina faida kubwa kuliko afua zingine, hii imesaidia kwa kiasi kikubwa.

“Kutoa madini chuma na folic kwa kinamama wajawazito, ushahidi umeonesha unapotoa haya madini inasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ambayo ni chanzo kikubwa cha vifo hivyo.

“Ni muhimu kuleta ufumbuzi ili tuwe na ujasiri kusema inawezekana kufanya na juhudi tulizozianzisha ziendelee,” amesema Dk Sando.

Mkurugenzi wa huduma ya mama na mtoto Gates Foundation, Dk Rassa Izadnegahdar amesema amesema utashi wa kisiasa umefanikisha mafanikio hayo.

Dk Makuwani anasema ili kupunguza vifo vya wajawazito ni muhimu kuweka mkazo kwenye vitendea kazi na kuweza kumfikia mtu wa mwisho katika maeneo ya vijijini na hiyo wameona katika baadhi ya miradi iliyofanikisha.

“Kama tunaweza kuvunja huo ukuta pale juu itawezekana, kama tutakua na uwezo kuhakikisha kila hospital ya wilaya ina vifaa vinavyotakiwa, na bidhaa za afya zinazowezesha ili mtoto aweze kukua ikiwa tu tutakuwa tunahitaji kuweka shabaha tunaweza kufanikisha kupunguza zaidi vifo hivi,” amesema Dk Makuwani.

Dk Sunday amesema suala la watendakazi ni gumu na kwamba hilo ndilo changamoto, lakini vitu muhimu kuzungumza ni mawasiliano.

Dk Sando amesema changamoto mbalimbali za utekelezaji zinatakiwa zitatuliwe kwa ugunduzi wa vitu vingi tuvitumie kama programu mpya pamoja tafiti zaidi eneo hilo.

Related Posts