Tangazo la Trump kuichukua Gaza lazua hofu

Washington. Mpango wa Rais Donald Trump kuiwezesha Marekani kuchukua udhibiti wa eneo la Gaza na kuibadilisha kutoka magofu kuwa ‘Riviera’ yaani Pwani ya utalii ya Mashariki ya Kati, unazua hofu miongoni mwa wataalamu wa sera za kigeni, wakionya huenda ukasababisha uvamizi wa umwagaji damu.

Kauli za Trump kuhusu suala hilo, ikiwemo kupeleka wanajeshi ikiwa italazimu, zimezua mjadala miongoni mwa wabunge na wachambuzi, wakihofia kwamba zinaweza kuitumbukiza nchi katika jukumu gumu la kuwa mamlaka inayokalia eneo hilo kwa mabavu, katikati ya mzozo mgumu kutatuliwa.

Trump aliyasema hayo jana Februari 4, 2025 katika Ikulu ya White House alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Israel.

Trump alivyoulielezea, mpango huo ungehusisha ujenzi mkubwa wa miundombinu na fursa za ajira.

“Sitaki kuonekana mjuaji, lakini Riviera ya Mashariki ya Kati… hili linaweza kuwa jambo la ajabu sana,” alisema Trump.

Hata hivyo, maoni ya Trump hayakugusia moja kwa moja hatari za kimwili zinazoweza kuambatana na utekelezaji wa mpango huo kutoka kwa mabomu ambayo hayajalipuka, hadi kwa upinzani mkali kutoka kwa Wapalestina wanaoiona Gaza kama nyumbani kwao, licha ya wito wa Trump wa kuwahamishia kwenye mazingira bora zaidi mahali pengine.

“Tutamiliki eneo hilo na tutakuwa na jukumu la kuondoa mabomu yote hatari, ambayo hayajalipuka na silaha nyingine, kulisawazisha na kuondoa majengo yaliyoharibiwa,” alisema Trump.

Aliongeza kuwa Marekani itaunda “mpango wa maendeleo ya kiuchumi, ambao utatoa nafasi za ajira zisizo na kikomo na makazi kwa watu wa eneo hilo.”

Trump alisema “mradi huo utafanywa kwa viwango vya kimataifa” na alipoulizwa ni nani angeishi huko, alisema “watu wa dunia,” kisha akaongeza kuwa Wapalestina pia wangekuwa sehemu yake.

Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Netanyahu alionekana akitabasamu huku Trump akiongoza mazungumzo.

“Trump analipeleka hili katika kiwango cha juu zaidi,” amesema Netanyahu, akionyesha kuunga mkono pendekezo hilo.

Timu yake ililitangaza kama njia ya kuvunja hali ya sasa. “Maana halisi ya wazimu ni kufanya jambo lilelile na kutarajia matokeo tofauti. Amani—amani ya kweli na ya kudumu—ndilo lengo kuu na inaweza tu kupatikana kupitia Rais huyu,” ameandika mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu, Steven Cheung.

Muda mfupi baada ya tamko hilo, minong’ono ilianza, humo humo ndani ya East Room ya Ikulu ya White House.

 “Hili ni la kipumbavu,” alisema mwandishi mmoja baada ya Trump kulitangaza.

Ingawa Trump mwenyewe alikiri uharibifu mkubwa uliopo Gaza na majengo yaliyoporomoka, kauli zake hazikuangazia changamoto kubwa za kiusalama wala kiwango kikubwa cha juhudi za ujenzi upya zinazohitajika.

Ingawa Trump amedai kuwa viongozi wa Mashariki ya Kati wanapenda wazo hilo na kwamba Wapalestina milioni 1.8, ambao alikadiria wangepangishiwa makazi katika nchi nyingine, wangelikubali, kulikuwepo na dalili kwamba pendekezo hilo halikuwa limepangwa kikamilifu hadi alipolizungumza na waandishi wa habari.

“Nadhani kila mtu anataka kuona amani katika kanda,” Steve Witkoff, mjumbe maalumu wa Marekani kwa Mashariki ya Kati, aliambia Fox News.

“Amani katika kanda inamaanisha maisha bora kwa Wapalestina. Maisha bora hayahusiani tu na mahali ulipo leo. Maisha bora yanahusu fursa bora, hali bora za kifedha na matumaini bora kwa ajili yako na familia yako.”

Mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, Aaron David Miller, ambaye amewashauri mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani chini ya tawala mbalimbali za vyama vyote viwili, amesema mwitikio wa haraka miongoni mwa Wapalestina na viongozi wa kanda hiyo ulikuwa wa machukizo.

“Swali ni je, huu ni usumbufu wa Trump tu, au ni sehemu ya mkakati halisi? Na nadhani hili ni jambo linaloonyesha tabia ya mtu asiye makini kabisa,” Miller ameambia DailyMail.com.
 

“Anawaza kwa mtazamo wa mfanyabiashara wa mali isiyohamishika anayefuata fursa za binafsi.”

Hata washirika wa kisiasa wa Trump, kama Seneta wa Republican wa South Carolina Lindsey Graham, alitoa pongezi hafifu kwa pendekezo hilo akilieleza kama “wazo la kuvutia” – licha ya yeye kuunga mkono uteuzi wake tata wa Baraza la Mawaziri hapo awali.

“Nadhani watu wengi wa South Carolina huenda wasifurahie sana wazo la kuwatuma Wamarekani kuchukua udhibiti wa Gaza. Huenda hilo likawa tatizo,” Graham amesema, akinukuliwa na Jewish Insider.

Trump alitoa pendekezo hilo saa chache tu baada ya kulaani gharama kubwa ya damu na mali ambayo Marekani ilipoteza katika Vita vya Iraq – moja ya hoja kuu katika kampeni zake za uchaguzi.

Miongoni mwa waliolidharau wazo hilo alikuwa Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, ambaye alirejelea jinsi Trump alivyolitaja eneo hilo kuwa fursa ya kuunda “kipande kizuri, kipya na cha kuvutia cha ardhi” kilicho kwenye pwani ya Mediterania.

“Kwa wale wanaotaka kuwapeleka Wapalestina mahali pazuri na penye furaha, basi warudishwe kwenye makazi yao ya asili ndani ya Israel,” alisema Mansour.

Mchambuzi wa CNN Fareed Zakaria alifafanua mpango huo akisema: “Marekani italazimika kuivamia Gaza, kuwafukuza Hamas, na kufanya operesheni za kupambana na waasi. Hii ni vita nyingine katika Mashariki ya Kati.”

Israel, katika siku chache baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, ilielekeza umakini kwenye mtandao mkubwa wa handaki ambao Hamas ilijenga chini ya ardhi huko Gaza ili kuficha silaha na baadaye kuwateka nyara mateka kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku wengi wao bado wakingoja kuachiwa katika makubaliano ya hatua ya pili.

Athari za pendekezo la Trump kwenye mazungumzo hayo tete, zilikuwa bado zinatathminiwa Jumanne usiku na Jumatano asubuhi.

“Nadhani anabuni mambo tu bila mpangilio wowote. Hakika hakuna mpango wowote nyuma ya hili,” alisema Brian Katulis, mshiriki mkuu wa sera za kigeni za Marekani katika Mashariki ya Kati alipozungumza na Reuters.

“Hata kama kuna mpango wowote, hauhusiani kabisa na uhalisia wa Mashariki ya Kati wa leo na hakika haujashirikisha mashauriano yoyote na Wapalestina au nchi jirani kama Misri na Jordan.”

Gaza kwa muda mrefu imechukuliwa kuwa sehemu muhimu ya suluhisho lolote la mzozo wa muda mrefu, kama sehemu ya taifa la baadaye la Palestina ambalo lingejumuisha Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel.

Viongozi wa Hamas, licha ya kupata hasara kubwa baada ya kushambuliwa kufuatia mashambulizi ya kikatili ya Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel, walikosoa vikali pendekezo hilo wakiliita “la kibaguzi” na kichocheo cha “machafuko.”

Ofisa mwandamizi wa Hamas, Sami Abu Zuhri, aliiambia shirika la habari la Shehab News Agency lenye makao yake Gaza kwamba mpango huo ni “kichocheo cha machafuko na mvutano wa kikanda.”

Amesema wakaazi wa Gaza hawataruhusu mipango kama hiyo kutekelezwa na kusisitiza kuwa, “kinachohitajika ni kukomeshwa kwa ukaliaji wa mabavu na mashambulizi dhidi ya Wapalestina, si kuwafukuza kutoka katika ardhi yao.”

Related Posts